Jina hilo la 'ubatizo' wamekuwa wakipachikwa Masheikh wanaokwenda kinyume na maslahi ya Waislamu na kuelemea zaidi katika maslahi ya serikali na vyama vya kisiasa hasa chama tawala.
Aidha, kutokana na Waislamu kuvishutumu baadhi ya vyama vya kisiasa ambavyo vimekuwa vikiuhujumu Uislamu Masheikh hao wamejitokeza kukemea mwenendo huo wakidai kwamba huko ni kuudhalilisha Uislamu.
Hoja yao kubwa ni kwamba kukiandama chama itakuwa sawa na kukipambanisha na Uislamu wakati Uislamu upo juu ya vyama. Ni dini ya Allah.
Uislamu toka awali kuanzia kwa Adam, Nuh, Ibrahim, Musa na kadhalika, umekuwa ukiwaita watu waache mifumo batili ya maisha na wakati huo huo kupambana na nguvu au vikwazo vyovyote vya kuwazuilia watu na dini ya Mwenyezi Mungu.
Uislamu kwa umbile lake na mafundisho yake haukubali dhulma wala uonevu. Ukidhulumiwa hata kama kwa wakati ule huna ubavu wa kuiepuka dhulma hiyo; basi angalau uitambue; uichukie na utoe kauli ya kutokuridhika.
Na kwa vile Waislamu ni waadilifu hawawezi kwa mfano wakaishutumu CHADEMA au TLP endapo haijawakwaza katika UIslamu wao kwa kauli au vitendo.
Lakini kwa mfano kama chama kitasimamia kutekelezwa kwa sera ambazo zinawakandamiza Waislamu na kuwanyima haki zao za msingi, Waislamu wana haki ya kidini ya kukiambia chama hicho kwamba hakitendi haki na kisipokoma itabidi Waislamu wapambane kwa mbinu mbalimbali kuiondoa dhuluma hiyo.
Na hiyo haiwezi kutafsiriwa kwamba Waislamu badala ya kufanya dini wanapambana na chama. Uislamu si chama cha siasa na haupambani na vyama vya siasa, bali unapambana na udhalimu na madhalimu iwe ni mtu, chama, serikali, NATO, 'Masheikh', Maaskofu n.k.
Kama ambavyo Mussa alipambana na Firauni na watu wake wakiongozwa na chama chao cha imani za kichawi ndivyo leo Waislamu wanavyopambana na vyama na serikali zisizomtambua Mungu katika maongozi yao, imani ambazo zinawawezesha kufanya dhulma dhidi ya wananchi bila ya khofu.
Askari polisi walimwaga damu ya Waislamu wasio na hatia pale Mwembechai; Mh. Rais amepokea madai ya Waislamu kuwa suala hilo halijesha. Hakusema zilikuwa 'balozi', siasa wala 'wakorofi wachache'. Maana yake ipo dhulma ambayo ilifanyika ambayo yahitaji ichunguzwe kwa kina na ipatiwe ufumbuzi.
Lakini pamoja na ukweli huo walitokea Masheikh wakakaa meza moja katika eneo la mauaji na walioamrisha mauaji yale huku mikono yao ingali imetapakaa damu na damu ya waliouliwa ingali mbichi; wakawaunga mkono na kuwakemea wafiwa wakiwa bado tangani.
Masheikh hao hawawezi kuitwa CHADEMA kwani siyo viongozi wa CHADEDMA waliosimamia mauaji yale.Tungependa tusisitize kwamba lengo si kupambana na chama chochote cha siasa. Uislamu ni uadilifu, haupendi dhulma. Mwisho wa dhulma ni maafa. Kila anayeitakia nchi yetu mema huyo ndiye mzalendo wa kweli. Na hatasita kuikimea dhulma hata kama imefanywa na serikali au chama tawala.
Sheikh asiyeguswa wala kuingiwa na huzuni Muislamu mwenzake akilengwa shabaha 'piga shaba', 'piga yule' hakuna jina litakalofaa zaidi ya lile la chama ambacho nacho hakikuona huzuni watu kuuliwa na wanawake kudhalilishwa. Hakikuona huzuni kiasi cha kufikia hatua ya kushabikia na kupongeza hatua zile za polisi zilizoacha wajane na mayatima huku zikitokomeza roho za vijana wabichi ambao hawajaacha mbegu za kuendeleza utajo wao.
Wanaitwa CCM si kwa maana ya kisiasa kwamba wao ni wanachama hai na wakereketwa wa CCM; lakini ni kwa maana ile ile ya kushutumiwa CCM kwamba imeipa haki mgongo na kufumbia macho dhulma inayofanywa dhidi ya Waislamu.
Masheikh wetu tungependa kuwanasihi waelewe kwamba uoni na fahamu za Waislamu si za kiwango cha chini kama wanavyodhania. Watakuwa wanaendelea kujidharaulisha na kujifedhehesha mbele za waumini endapo hawatakuwa na upeo wa kupima yepi ya kusema, wapi na kwa lengo gani.
--
|
|