Na Anaphy A. Saidi
KWANZA, nampongeza sana Bw. Maalim Bassaleh katika makala yake iliosomeka hivi; "Kwanini tusisali Iddi siku moja?" Akisisitiza umoja wa Waislamu katika toleo nambari 196 la gazeti hili tukufu la ANNUUR.
Pili, nachukua fursa hii kutoa ufafanuzi zaidi juu ya baadhi ya mambo aliyoyaeleza. Umoja wa Kiislamu ni jambo lililosisitizwa sana, na ndio sababu utakuta lugha ya swala kwa Waislamu wote ni Kiarabu, pia Waislamu wote huelekea upande mmoja wanaposali, pia Waislamu wenye kuhiji humiminika Makka kutoka sehemu mbalimbali duniani ili kutekeleza ibada ya hija katika wakati mmoja na sehemu moja. Hayo na mengi mengineyo huonyesha Uislamu unavyoashiria umoja.
Hata hivyo, ni kweli kwamba Mtume (s.a.w.) alisema; "Akijitahidi mwanachuoni akasibu basi atapata malipo mara mbili. Na akijitahidi akakosea basi atapata ujira mara moja". Lakini hukumu hii inamhusu mwenyewe mwanachuoni, sio wale wanaosikiliza au kufuata hukumu yake, kwa sababu wale wanaosikiliza au kufuata hukumu yake wakiona kuwa hukumu aliyoitoa si sahihi basi inawapasa wafuate iliyo sahihi na kuacha kuwa kama "bendera fuata upepo".
Na ikithibiti kuwa hukumu yake mwanachuoni haikusibu na analijua hilo, basi itampasa afuate yaliyo sahihi. Katika Qur'an (21:78-79) tunasimuliwa namna Nabii Daudi alivyotoa hukumu isiyosahihi, mwanawe anayeitwa Nabii Suleiman alimsahihisha babaye juu ya hukumu aliyoitoa, na Nabii Daudi akaikubali hukumu ile iliyotolewa na mwanawe. Sasa wengi wetu huwa tunaiga tu (taqlid) bila kujua usahihi au ubatili wa hukumu.
Pia ni kweli kwamba Mtume (s.a.w.) aliwahi kusali sala ya Iddi siku ya pili baada ya kushindwa kuisali katika siku ya kwanza kutokana na kuchelewa kupata habari za kuandama kwa mwezi. Mazingira ya hadithi yanaonyesha kuwa Mtume (s.a.w.) alipata habari ya kuandama kwa mwezi mwishoni mwa mchana (jioni) kutoka kwa msafara uliofika mjini Madina wakati huo, na kwa sababu wakati wa sala ya Iddi ulishapita, aliwaamuru masahaba wafungue saumu zao na kusali sala ya Iddi kesho yake.
Sasa, wale wanaofuata mwezi wa kimataifa hawana sababu yoyote ya msingi ya kuchelewesha kuisali Iddi kwa ajili ya kuwaongojea wale wanaofuata mwezi wa kitaifa kwa sababu hakuna ushahidi wowote ule wa kuchelewesha sala kwa ajili ya kuwasubiri wengine!
Na kama kwa kufuata uwingi basi wale wanaofuata mwezi wa kimataifa ndio walio wengi zaidi duniani. Kwa sababu wafuasi wa madhehebu ya Hanafi, Maliki na Hambali wote wanafuata mwezi wa kimataifa kutokana na rai za Maimamu wa madhehebu hayo wanayofuata, achilia mbali wale ambao hawajajiegemeza katika madhehebu.
Ama kama tukisema kwamba kwa sababu sala ya Iddi ni sunna tu hivyo tunaweza kuichelewesha kwa kutaka umoja, hili pia litakuwa tatizo. Kwani mara nyingi Waislamu tumekuwa tukipuuzia baadhi ya mambo kwa kusema kuwa, hii si suna tu? Tukumbuke kuwa Mtume (s.a.w.) alisema; "Nimekuachieni vizito viwili ambavyo mkishikamana navyo kikamilifu hamtapoea, kitabu cha Allah na sunna zangu". Sunna (mwenendo) wa Mtume (s.a.w.) ilikuwa ni kusali Iddi siku yenyewe ya Iddi na si vinginevyo.
Umuhimu wa kuisali Iddi katika siku yake kwa wale wanaofuata mwezi wa kimataifa ni kuweza kuwapa fursa Waislamu wengine juu ya tofauti ya suala hili ili waweze kulifanyia uchunguzi na kujua hakika yake japokuwa kuna baadhi ya Masheikh waliokalia ushindani tu katika suala hili.
Ili kuleta umoja wa kweli miongoni mwetu Waislamu ni wajibu turejee kwenye Qur'an na Sunna iwapo kuna mizozo baina yetu. Hakuna sababu yoyote ya kuhitilafiana hali ya kuwa Mungu wetu ni mmoja, Mtume wetu ni mmoja, Dini yetu ni moja, Kitabu chetu ni kimoja, Lailatul-Qadri ni moja, Arafa ni moja na kadhalika.
--
|
|