Makala
 
Hali ya jamii ilivyokuwa zamani na ilivyo sasa, nini la kufanya
 

Na Aboubakari S. Marwillo
 

MIONGONI mwa watu, haswa katika nchi zetu hizi masikini, wanasema kuwa Ukristo umeleta maendeleo. Wamekuwa na kauli hiyo kwa sababu hawana historia sahihi ya Ukristo ulivyofanya katika dunia yetu hii. Kufuatana na historia sahihi ilivyo, Ukristo haukuleta maendeleo na wala hautaleta maendeleo katika jamii yoyote ile. Upo ushahidi wa kutosha kuwa wasimamizi wa Ukristo wanachokifanya ni kubadili hatua kwa hatua fikra za watu ili hatimaye ziwafae hao wasimamizi na watu wenyewe wawe katika hasara hapa duniani na huko akhera.

Kabla ya kuja kwa Mtume (s.a.w.) enzi za Kikristo katika karne ya sita, iliwakilisha bayana awamu ya giza katika historia ya binadamu. Waliozusha itikadi ya Kikristo hawakuwa na nchi yoyote yenye nguvu kuuokoa ubinadamu.

Binadamu walimsahau kabisa Mwenyezi Mungu, na pia ikafika wakati binadamu huyo huyo akajisahau yeye mwenyewe. Kwa ujumla alipoteza kabisa mwelekeo wake na lengo la kuwepo kwake hapa duniani akalisahau. Hali hii ilipangwa ifanyike hivyo. Kwa sababu viongozi wa Kikristo walijifungia katika majumba yao makubwa na wakajitenga na mazingira ya dunia. La kushangaza sana waliungana na tabaka la watawala kusaidiana katika kuulinda na kuundeleza mpango wa uchumi na siasa - mpango uliokuwa umejaa dhulma na unyonyaji.

Mfumo huo wa uchumi na siasa uligeuza maisha ya watu kuwa mabaya kiasi kwamba wakajitumbukiza katika maovu na maporomoko ya maadili. Hawakuwa na la kufanya kwa maendeleo yao. Jamii zilikuwa na umasikini uliopindukia kawaida. Watu wa wakati na matajiri hawakufanya lolote wala chochote kuwasaidia watu, bali waliona ni bora kutumia utajiri wao au mali zao katika mambo ya kipuuzi na anasa. Mifano ya mambo ya kipuuzi na anasa ni kama haya yanayotajwa: Kucheza kamari, ulevi; kutumia fedha kufanya makaribisho; na kutumia fedha kwa mambo ya wanawake, miziki na laghai nyingine.

Makasisi wa Makanisa na Wakuu mbalimbali wa dini ya Kikristo, hawakujali kugeuza hali mbaya ya watu. Badala yake waliufanya Ukristo ni kitu cha kuhakikisha maovu yao. Waliyageuza maandiko mengi ya hiyo dini na kuweka maandiko yanayolenga kuyaenzi maslahi yao. Maandiko ya kale na asili yalipotea kupindukia utambuzi wa kawaida; na hata waasisi wa maandiko hayo wangelifufuka wasingeweza kuyatambua hata kidogo. Hivyo ndiyo kusema makasisi na wakuu hao hawakuwa na chochote cha kuwapa watu au kwa usemi mwingine hawakuwa na risala ya kuwapa watu kwa ajili ya kurekebisha mfumo wa maisha yao kwa faida yao hapa duniani na huko akhera.

Ukristo bado haujawa na utaratibu maalum ambao unaweza kutoa nguzo kamili ya ustaarabu wa dunia; au msingi madhubuti wa siasa na uongozi wa dunia. Ukristo una mafundisho machache sana yanayompwekesha Mwenyezi Mungu. Hivyo mafundisho hayo yalimweka binaadamu katika mchanganyiko maalum kujua uwezo wa Mwenyezi Mungu. Yule wanamsema kuwa ni Mtakatifu, yaani Paulo, pia alichangia mafundisho yake na kuyaweka rasmi katika vitabu vya Ukristo; hivyo kuwachanganya zaidi watu. Si vibaya nikisema mafundisho ya Paulo yanawakilisha mila za Kirumi. Paulo hakuwa peke yake. Wakati wa utawala wa Constantine, mizizi ya imani ya Ukristo ilijikita zaidi. Mafundisho halisi ya Yesu yalipotea, na mafundisho ya Ugiriki, Urumi na ya watu wengine yakashika nafasi yake na kuwa imani kamili ya watu wanaoitwa Wakristo.

Lingine la kushangaza ni desturi iliyoanzishwa ya kuabudu watakatifu na masanamu katika majumba ya ibada. Watu walipenda ibada hii ya kuabudu watakatifu na masanamu kuliko Warumi wenyewe.

Kufanya walivyofanya, baadaye palikuwepo na mgawanyiko na machafuko makubwa ndani ya madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Makazi ya watu, mashule mbalimbali na Makanisa yaligeuka kuwa makambi ya vita. Nchi ziliingia katika vita vya kiraia. Ni nini kilichosababisha hali mbaya ya namna hii? Ugomvi ulisababishwa kutokana na maumbile ya Yesu. Wengine waliamini Yesu ana sehemu ya Kiungu na sehemu nyingine ya kibinadamu. Au wengine walidai Yesu alikuwa na maumbile ya Kimungu katika sura ya kibinadamu hivyo ni Mungu. Watawala wa Kirumi walitumia mamlaka yao ya kiserikali kulazimisha imani hii kuwa ni imani moja kwa utawala wao wa Mashariki. Waliwauwa, bila hata kosa lolote wapinzani wa imani yao. Lakini hili halikufanikiwa hata kidogo.

Pamoja na hila, kadha wa kadha zilizofanyiwa watu, watu hawakuwa na uchumi mzuri. Kodi na kodi ndogondogo zilikuwa kubwa mno na hili liliwafanya watu wengi kulalamika na kuwa katika shida nyingi ambazo hazieleweki. Pia walinyang'anywa mali zao na kuhodhi mali ndiyo ilikuwa mtindo wa maisha.

Pia kulikuwepo maasi na upinzani dhidi ya hali hii duni. Watawala hawakuzingatia hata chembe upinzani huo, bali walichofanya ni kuwauwa baadhi ya watu, hususan wapinzani. Huku matajiri wakitumia utajiri wao ovyo-ovyo na katika anasa na mambo ya shahawati. Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hii ndiyo kusema kwamba matajiri hawakuwa na mazingira mazuri wala watawala hawakuwaongoza mwenendo mwema.

Nguzo ya jamii ilikuwa dhaifu kiasi kikubwa na misingi ya ustaarabu wa binadamu uliharibika na kuoza. Desturi ya kuowa ilichukiwa na badala yake watu walipendelea ukapera. Watu walikuwa huru kufanya wanavyotaka ili kuridhisha mioyo yao. Haki iliuzwa kama bidhaa katika soko au masoko. Rushwa na uvunjaji wa dhamana ni vitu vilivyokuwa vinashangiliwa na watawala, na waliviunga mkono. Wakati huo Warumi ndiyo waliokuwa watawala katika karne ya sita, na walianguka kiasi kikubwa na kuwa chini kuliko waliokuwa chini. Ndiyo kusema kuwa ilikuwa afadhali ya wanyama kuliko watawala hao.

Hali ya dunia iliporomoka vibaya sana kutokana na viwango vya kodi kuwa vikubwa, biashara kusinyaa, kilimo kudharauliwa na watu kupungua. Miji mikubwa iliharibiwa kabisa na haikupata tena neema zake.

Ni hivi karibuni ulimwengu utaingia katika karne ya ishirini na moja, ambayo inaelezwa na wanasiasa wetu kuwa ni karne ya sayansi na teknolojia. Lakini hebu tazama yanayotokea katika dunia ya leo ni sawa kabisa na yale yaliyotokea katika karne ya sita. Mauaji bila ya haki ni kitu cha kawaida leo. Kuabudu fikra za watu ni kitu cha kawaida hivi leo. Rushwa ni kitu cha kawaida hivi leo. Kuporomoka maadili katika jamii mbalimbali ni gumzo la kila siku mitaani na katika majukwaa mbalimbali ya vyombo vya utawala. Mfumo mbaya wa kodi, uchumi na kilimo duni ndiyo sea za watawala, nikitaja machache tu. Haya yote yanatokea kwa sababu watawala wetu hawataki kujifunza kutokana na makosa. Hawakubali kutakataa kuwa fikra na uongozi wa dunia zimegota. Hivi ni nani atakayewatoa kutoka katika upotovu na 'tope' hili la ujahili? Suala hili ni rahisi kujibu, lakini linahitaji mipango madhubuti; na watu madhubuti; na malengo madhubuti. Kinyume cha hivyo dunia itaendelea kupata taabu na mashaka makubwa.

Waislamu ndio waliopewa mwongozo sahihi wa kuiongoza dunia nzima. Hili linathibitishwa na Mwenyezi Mungu kuwa Qur'an ni mwongozo wa wacha Mungu; ni mwongozo kwa watu; na ni kitabu kisichokuwa na shaka ndani yake. Mtume (s.a.w.) pia wakati wa Hija yake ya mwisho ametukabidhi vitu viwili, yaani Qur'an na mwenendo wake.

Tukifuata vitu hivi viwili hatutapotea. Na ndiyo kusema kuwa tukiviacha tutapotea. Kuviacha vitu hivi ni sawa na kukanusha aya za Mwenyezi Mungu. Je; hii ni hasara au faida? Tunafahamishwa katika surat Al-Aaraf (7) aya ya 146 na 147 kuwa:

"Nitawaepusha na (kuzingatia) aya zangu wale wanaotakabari katika nchi pasipo haki; na ambao kila hoja wanayoiona hawaiamini; na kama wakiiona njia ya uwongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiiona njia ya upotefu (upotevu) wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu ya kuzikadhibisha aya zetu na kuzipuuza".

"Na wale waliozikadhibisha aya zetu na (wakakadhibisha) kukutana na akhera, amali zao zimeharibika. Kwani hawatalipwa mengine, ila yale yale waliyokuwa wakiyatenda. (Basi maadamu wanatenda mabaya, basi watalipwa ubaya wao".
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook