Uchambuzi/hoja binafsi
Je, Yehova na Allah ni miungu tofauti ? - 5
 

Na Muhibu Said

KATIKA matoleo yaliyopita, tulizidi kuona Qur'an tukufu na Biblia takatifu vikizidi kubainisha kwa uwazi zaidi sifa kuu ya Mungu wa kweli ambaye kwa sifa hizo alizidi kudhihirika kuwa ndiye Mungu yule yule mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbalimbali hadi kwa Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.) kwa majina tofauti. Kama nilivyoahidi katika toleo lililopita, endelea kufuatana nami sehemu ya tano ya mada hii, uzidi kuona kwa upana zaidi sifa kuu za Mungu huyo na uone kama kweli Mungu huyo amezaa mtoto na ndiye Mungu anayeabudiwa na Wakristo? Huku tukiendelea namada hii muhimu, ningependa kuwakumbusha hapa wasomaji wangu wapenzi kwamba wajihadhari na ubabaishaji wa neno la Mungu unaofanywa na mtaalamu mmoja wa magonjwa ya akinamama wa kupotosha makusudi aya za Qur'an tukufu kinyume na muradi wake na kunukuu bila kujua Hadithi dhaifu na za Kiyahudi (Israel Yyaat) akijifanya ati kanukuu maneno ya Mtume Muhammad (s.a.w.) kutoka katika 'Mavolume' mbalimbali ya vitabu vya watu vilivyokusanya Hadithi sahihi za Mtume (s.a.w.) na Hadithi dhaifu (zisizokuwa za Mtume) anavyoviita vya Kiislamu!

Kutokuzaa wala kuzaliwa

Kwa kuzingatia kuwa Yeye hafanani na kiumbe wake yeyote wala chochote katika kila hali, Mungu wa kweli ni lazima awe ametakasika kwa kuepukana mbali kabisa na sifa ya kuzaa na kuzaliwa hasa kwa kuzingatia udhaifu na upungufu mkubwa uliomo katika sifa hizo unaowakabili viumbe wake.

Kama Mungu angekuwa na sifa ya kuzaa au angekuwa amezaliwa, hapana shaka angekuwa amefanana na viumbe wake. Na hapo ile sifa yake tukufu ya kutokufanana na yeyote wala na chochote katika viumbe wake ingebatilika.

Aidha, udhaifu uliopo kwa kila chenye kuzaa na chenye kuzaliwa, kwa uchache, ni kwamba hakiwezi kufanikiwa mambo hayo isipokuwa kwa kutegemea ushirikiano na kingine au kwa kutegemea uwezo wa nje yake. Na huo ni upungufu mkubwa ulio mbali kabisa na sifa kamilifu za Mwenyezi Mungu mtukufu.

Kwa mantiki hiyo, ni wazi kuwa sifa hizi nazo ni vigezo vingine muhimu na vya msingi vinavyoweza kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo itabainika mmoja wao hana sifa hizo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu tunaona ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja wa kwenye vitabu hivyo ndiye peke yake mwenye sifa hizo ( ya kutozaa wala kuzaliwa). Maandiko yafuatayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu yanathibitisha ukweli huu:

BIBLIA:

"Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye, kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine". (Isaya 43:10)

"BWANA, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, BWANA wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu". (Isaya 44:6)

Mwenyezi Mungu anachokusudia kutufahamisha hapo juu ni kwamba hakuna Mungu yeyote wala chochote kilichomtangulia kuwepo na kwamba tufahamu kuwa yeye ndiye wa mwanzo kuwepo na kwa kuwa yeye ndiye wa mwanzo kuwepo, ni wazi kuwa hakuna aliyemuumba wala aliyemzaa.

Pamoja na kutufahamisha kuwa hakuna yeyote wala chochote kilichomtangulia kuwepo, Biblia pia imetufahamisha hivi:

"Wajue ya kuwa Wewe, uitwaye jina lako YEHOVA, Ndiwe peke yako Uliye juu, juu ya nchi yote". (Zaburi 83:18)

"Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma". (Yohana 17:3)

Tunachojifunza kutokana na shuhuda hizo za Biblia hapo juu ni kwamba, baada ya Yeye (Mungu) kutufahamisha kwamba hakuna kilichomtangulia kuwepo, Mungu pia yuko peke yake. Kwa maana kwamba hana Mungu wa kumwabudu, hana ukoo, hana baba, hana mama, hana mke, hana ndugu, hana familia wala hajazaa mtoto. Bali Yeye ni wa pekee. Kwa ufupi, hivi ndivyo tunayofundishwa na Biblia takatifu.

QUR'AN:

Ama kwa upande wa Qur'an tukufu, Allah (Mwenyezi Mungu s.w.) pia alijieleza bayana kuhusu sifa hizo (ya kutokuzaa wala kuzaliwa) kama ifuatavyo:

"Sema: Yeye Allah (Mwenyezi Mungu) ni Mmoja (tu). Allah (Mwenyezi Mungu) (tu) ndiye anayestahiki kukusudiwa (na viumbe vyake vyote kwa kumuabudu na kumuomba na kumtegemea). Hakuzaa wala Hakuzaliwa. Wala hana anayefanana Naye hata mmoja". (Qur. 112:1-4)

Maandiko hayo ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu hapo juu bado yanatudhihirishia wazi kwamba mwenye sifa ya kutozaa mtoto, kuumbwa na kutozaliwa ni Mwenyezi Mungu yule yule mmoja, peke yake, aliyejifunua kwa mara ya kwanza kwa Nabii Musa (a.s.) kwa jina la Yehova na ndiye ambaye amejifunua kwa jina lake kuu la Allah kwa Nabii wake wa mwisho, Mtume Muhammad (s.a.w.).

Upotofu wa Wakristo juu ya mahusiano kati ya Mungu, Bikira Mariamu na Yesu (a.s.)

Hapo juu, tumeona jinsi maandiko ya Qur'an tukufu na Biblia takatifu yanathibitisha Mungu akipinga vikali dhana nzima ya Yeye kuwa na sifa dhaifu na pungufu ya kuzaa na kuzaliwa. Pamoja na shuhuda hizo, lakutisha ni kwamba Wakristo bila ya hofu wala aibu wamefika kuwajengea watu picha inayoonyesha mahusiano ya mke na mume kati ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na Bikira Mariamu kupitia Nabii Isa ama Yesu (a.s.) kinyume na ukweli ulivyo!

Mahusiano hayo yanadhihirika pale Wakristo wanapojifariji wao wenyewe kwa kusema kuwa Nabii Yesu (a.s.) alikuwa na hali zote mbili - Mungu na Mwana aliyezaliwa kwa Mungu bila kuumbwa! Sehemu ya maelezo yao kama yalivyokaririwa na kitabu chao kiitwacho "Chuo kidogo cha sala na nyimbo" wanasema:

"Nasadiki kwa Mungu mmoja, Baba Mwenyezi Mwumba mbingu na nchi, na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Na kwa Bwana mmoja, Yesu Kristo Mwana wa pekee wa Mungu. Aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote. Mungu aliyetoka kwa Mungu, Mwanga kwa Mwanga, Mungu kweli kwa Mungu kweli. Aliyezaliwa bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba, ambaye vitu vyote vimeumbwa naye. Ameshuka toka mbinguni kwa ajili yetu sisi wanadamu na kwa ajili ya wokovu wetu". (Taz. Uk. 64-65)

"Mwana wa Mungu, Yesu Kristu, Mwana mzaliwa wa mbinguni". (Taz. Uk. 59)

Kulingana na maelezo hayo, wanachotaka Wakristo kukionyesha hapo ni kwamba Yesu hakuumbwa bali ni mtoto aliyezaliwa na Mungu huko mbinguni kisha akashuka duniani kuchanganyika na wanadamu lakini akiwa na Umungu sawa na Baba yake Mungu kwa kuwa ni mtoto aliyezaliwa naye!

Aidha, kwa njia hiyo wakathubutu kumwita Bikira Mariamu (mama wa Yesu) kuwa ni "mama mtakatifu wa Mungu". Wanasema:

"Salamu, Maria, umejaa neema Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote, na Yesu mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Maria mtakatifu, Mama wa Mungu, utuombee sisi wakosefu, sasa na saa ya kufa kwetu. Amina". (Taz. Uk. 14)

"Salamu Maria... Utuombee, mzazi mtakatifu wa Mungu. Tujaliwe ahadi za Kristu". (Taz. Uk. 8)

Ukizingatia maelezo yao ya awali kwamba Umungu wa Yesu ni sawa na Baba yake Mungu aliyemzaa huko mbinguni, Wakristo hapa vile vile wanajaribu kuonyesha Mungu wao (Yesu) pia anaye mzazi mwingine aliyemzaa ambaye ndiye Bikira Mariamu. Ni wazi kuwa mantiki hiyo ya Wakristo hapo haitoi picha nyingine zaidi ya kuonyesha mahusiano ya mke na mume kati ya Mwenyezi Mungu na Bikira Mariamu!

Wakitilia mkazo mahusiano hayo ya Mungu na Bikira Mariamu, Wakristo pia wamediriki kumwita Bikira Mariamu kuwa ni "Malkia wa Malaika, wa Mababu, Manabii, Mitume, Mashahidi, Waungana, Mabikira, Watakatifu wote na kubwa zaidi wamemwita "Malkia wa Mbunguni!" (Taz. Uk. 33,35).

Mara nyingi Malkia huwa ni binti ya mfalme aliyerithi kiti cha baba yake au huwa ni mke wa mfalme (rejea kamusi ya Kiswahili Sanifu Dar es Salaam Oxford University Press, Nairobi 1981, Uk. 151). Mbinguni kama maandiko yanavyofundisha ndiko aliko Mwenyezi Mungu (Taz. Mathayo 6:9), ambaye peke yake ndiye mfalme wa Malaika, Mitume, Manabii na kila kitu. Aidha, huko mbinguni hayupo baba yake Mariamu aliyefariki ambaye tunayeweza kusema labda Wakristo kwa kumwita kwao Mariamu "Malkia wa mbinguni", alimrithi baba yake huyo kiti cha ufalme. Sasa wanapomwita hivyo (Malkia wa mbinguni) wanazidi kutoa picha gani ya kimahusiano kati yake na Mungu ambaye ndiye mfalme wa mbinguni?

Ni dhahiri kuwa kama ambavyo wanashindwa kutamka wazi kwamba Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu ni Miungu watatu, vivyo hivyo, hawawezi kutamka wazi kwamba Bikira Mariamu aliyezaa Yesu ni mke wa Mungu, kwa kufahamu kuwa tamko lao hilo halitokubaliana na akili hata ya kawaida. Lakini kama tulivyoona maelezo yao, ni wazi kuwa mantiki yao inalenga katika kumfanya Bikira Mariamu kuwa na mahusiano ya mke na mume na Mwenyezi Mungu Mtukufu iil wamfanye Nabii Isa ama Yesu kuwa ni mtoto aliyezaliwa na Mungu!

Kwa msingi huo, ndio Allah (Mwenyezi Mungu s.w.) akawatolea Wakristo makemeo makali kuhusiana na mantiki nzima ya mafundisho yao hayo kama ifuatavyo:

"Na Mayahudi wanasema: Uzeri ni Mwana wa Allah (Mwenyezi Mungu), na Wakristo wanasema: Masihi ni Mwana wa Allah (Mwenyezi Mungu); haya ndiyo wasemayo kwa vinywa vyao (pasi na kuyapima). Wanayaiga maneno ya wale waliokufuru kabla yao, Allah (Mwenyezi Mungu) awaagamize. Wanageuzwa namna gani hawa!"

"Wamewafanya wanavyuoni wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Allah (Mwenyezi Mungu), na (wamemfanya) Masihi Mwana wa Mariamu (pia mungu), hali hawakuamrishwa isipokuwa kumuabudu Mungu mmoja, hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Yeye. Ametakasika na yale wanayomshirikisha nayo". (Qur. 9:30-31)

"Na (makafiri) husema: (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema amejifanyia mtoto. Bila shaka mumeleta jambo lichukizalo kabisa (kwa kusema hivyo). Zinakaribia mbingu kutatuka kwa (tamko) hilo na ardhi (ikakatika) vipande vipande. Kwa kule kudai kuwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema ana mtoto. Wala haiwi kwa (Mwenyezi Mungu) Mwingi wa rehema kuwa na mtoto". (19:88-92)

Pamoja na makemeo yake hayo dhidi ya Wakristo ambao wanajaribu kumuonyesha Yesu kwamba ni mtoto aliyezaliwa na Mungu kwa kule kumvika kwao mama yake "umalkia wa mbinguni" na "umama wa Mungu", Allah (s.w.) pia aliendelea kukanusha dhana nzima ya kuzaa mtoto kwa kuhoji mantiki hiyo ya Wakristo, kama ifuatavyo:

"Yeye ndiye Mwumba wa mbingu na ardhi. Inamkinikaje awe na mwana, hali hana mke. Naye ndiye aliyeumba kila kitu (sio baadhi yake kavizaa). Naye ni Mjuzi wa kila kitu". (Qur. 6:101)

Pamoja na msisitizo huo wa Allah, jambo la kuzingatia hapa ni kwamba wanaopingwa hapo ni Wakristo wanaojaribu kupotosha ukweli wa mambo kati ya Mwenyezi Mungu na Bikira Mariamu (a.s.) na wala hapo haipingwi Torati, Zaburi, Injili wala mafundisho ya Manabii.

Kutokufa (Yu Daima)

Kwa kuzingatia kuwa yeye hafanani na kiumbe wake yeyote wala chochote katika kila hali, ni dhahiri kuwa sifa kuu nyingine ya msingi ya Mungu wa kweli ni lazima iwe kutokufa, hasa kwa kuzingatia kuwa yeye pekee yake ndiye anayetegemewa na viumbe wake wote kwa kila haja, kwa vile yeye peke yake ndiye Mwendeshaji wa mambo yote katika kila sekunde.

Hakuna yeyote wala chochote kinachoweza kuendesha ulimwengu na kukidhi haja zote za viumbe wote katika muda wote ambao Mungu angekufa. Kwa mantiki hiyo basi, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia ni kigezo muhimu na cha msingi kimachoweza, kuwa hoja ya msingi ya kutofautisha Allah na Yehova iwapo tu itabainika 'mmoja wao' hana sifa hiyo. Hata hivyo, tusomapo maandiko ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu tunaona vyote vinafundisha kwamba mwenye sifa hiyo (ya kutokufa) ni Mwenyezi Mungu peke yake aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti. Maandiko yafuatayo ya Qur'ani Tukufu na Biblia Takatifu yanathibitisha ukweli huu:

Biblia:

"Nitasema, Ee Mungu wangu, usiniondoe katikati ya siku zangu; Miaka yako nitangu kizazi hata kizazi. hapo mwanzo uliutia msingi wa nchi, Na mbingu ni kazi ya mikono yako. Hizi zitaharibika, bali Wewe utadumu; Naam, hizi zitachakaa kama nguo; Na kama mavazi utazibadilisha, Nazo zitabadilika. Lakini Wewe U yeye yule; Na miaka yako haitakoma". (Zaburi 102:24-27).

"Mungu akamwambia Musa, MIMI NIKO AMBAYE NIKO; akasema ndivyo utakavyowaambia wana wa Isreili; MIMI NIKO amenituma kwenu" (Kutoka 3:14).

"Ambaye yeye peke yake hapatikani na mauti, amekaa katika nuru isiyoweza kukaribiwa; wala hakuna mwanadamu aliyemwona, wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye hata milele. Amina". (1 Timotheo 6:16).

Qur'an:

"Wala usimuombe - pamoja na Allah (Mwenyezi Mungu) - Mungu mwingine; hakuna aabudiwaye kwa haki ila Yeye; kila kitu kitakufa isipokuwa yeye (Mwenyezi Mungu basi). Hukumu (Yahova mambo yote) iko kwake, na kwake mtarejezwa (nyote)". (Qur'ani 28:88).

Aidha, kwa sifa yake ya kutokuonekana ni wazi kuwa hakuna yeyote wala chochote (na chenye uwezo wa) kumwua.

"Allah (Mwenyezi Mungu) hakuna Mola ila yeye, (na) ndiye mwenye uhai wa maisha, Msimamia kila jambo..." (Qur'an, 2:255).

Kulingana na shuhdua hizo juu, tunaona wazi kuwa Qur'an Tukufu na Biblia Takatifu vyote kwa pamoja vinafundisha kwamba Mwenyezi Mungu yule yule mmoja aliyejifunua au kujitambulisha kwa Manabii wake mbali mbali kwa majina tofauti ndiye peke yake mwenye uhai wa milele (yu daima) - hafi-na kwa ujumla yeye peke yake ndiye mwenye sifa ya kutokufa. Kwa shuhuda hizo, ni wazi kuwa sifa hii nayo pia inadhihirisha wazi kuwa Allah anayefundishwa na Qur'ani Tukufu ndiye Yehova anayefundishwa na Biblia Takatifu kwa majina tofauti.

Ukweli huu tunaupata katika Qur'an, Torati, Zaburi, Injili na sio kwenye Hadithi dhaifu zinazopingana na vitabu hvyo anazosingiziwa ati kasema Mtume Muhammad (s.a.w.)

Itaendelea toleo lijalo.
 --

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook