Na Abu Zubeir, Dodoma
SHEIKH Ahmed Zubeir amewaambia Waislamu wasikubali propaganda kuwa eti Waislamu hawakutaka kusoma toka wali; bali walikuwa wa mwanzo kusoma lakini wakazikataa shule za Wakristo waloweka taratibu zilizokuwa zikitumika za kuwabatiza Waislamu ili wakubalike kuingia katika shule zao.
Aliwafahamisha vijana kuwa sasa uwanja wa kutafuta elimu ni mpana; hivyo vijana wanapaswa kuitafuta elimu popote pale na kwa gharama zote.
Aidha, Sheikh Zubeir amesema kuwa dhulma iliyojaa dhidi ya Waislamu haitaondoka hadi pale Waislamu watakapolivalia njuga suala zima la kuitafuta elimu na wakaacha mtindo wa kuigawa elimu katika matapo mawili (elimu ya dini na dunia).
Sheikh Ahmed Zubeir wa Masjid Nunge mjini Dodoma ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akiwakilisha mada yake katika semina ya Umoja wa Vijana wa Kiislamu (U.V.K) iliyofanyika katika shule ya Seminari Al-Hijra. Katika kusisitiza suala zima la elimu, Sheikh Zubeir aliwaeleza vijana wa Kiislamu wapatao 150 kuwa Uislamu ndiyo dini pekee iliyotoa amri ya watu watafute elimu (wasome), aidha alisema mifumo mingine ya masiha iliyobuniwa na watu imeiga kutoka kwa Waislamu.
Naye Sheikh Muslim Yusuph akiwakilisha mada yake aliwataka vijana (Waislamu) juu ya kulingania Uislamu kwa wale ambao hawajabahatika kuukubali.
Sheikh Muslim alisema kazi ya kuwatia watu katika Uislamu ni amri ya Allah (s.w.) na hivyo kila Muislamu anapaswa kufanya kazi hiyo.
Wakati huo huo, katika maazimio yao, vijana wa Kiislamu wameahidi kuutumia muda wao vizuri kwa kusoma na kuzingatia kwa makini ili baadaye wawe wakombozi wa nchi hii kwa kuweka sera ya haki na usawa kwa wananchi wote.
Na Mwandishi Wetu
MASJID-NUUR Kiwalani Jumapili iliyopita iligeuka kuwa sehemu ya majonzi na vilio kufuatia onesho la mkanda wa video wa mauaji ya Mwembechai.
Mamia ya wanawake wa Kiislamu waliohudhuria mhadhara wa Kiislamu uliofanyika mahali hapo walijikuta wakiangua vilio baada ya kushuhudia matukio kadhaa ya kinyama yaliyofanywa na polisi ambayo yamenaswa na mkanda huo.
Baadhi ya kinamama hao walishangazwa na jinsi polisi walivyokuwa wakiua watu wasio na hatia huku wakishangilia.
Akizungumza baada ya onesho hilo, Mwenyekiti wa Kitengo cha uhamasishaji cha kamati ya wanawake Ukhti Arafa alihoji kuwa ni mpaka lini Waislamu wa Tanzania wataendelea kupuuzwa na kunyanyaswa.
Alisema serikali ya CCM chini ya Rais Benjamin Mkapa itakuwa imeweka kumbukumbu mbaya iwapo itaamua kutokuchukua hatua yoyote dhidi ya wauaji na wale walioamuru kufanyika mauaji ya Mwembechai.
Akionyesha upogo wa kimaamuzi uliopo serikali kuhusiana na masuala yanayohusu Waislamu, Bi Arafa alilinganisha tukio la Mwembechai na matukio yaliyotokea hivi karibuni kule Zanzibar na Dodoma vijijini.
Alisema wanajeshi waliopiga raia kule Zanzibar wamechukuliwa hatua kali mara moja, wanajeshi waliofanya fujo kijiji cha Veyula huko Dodoma wameshakamatwa tayari kuchukuliwa hatua lakini polisi walioua Waislamu Mwembechai wako huru na wengine wamepandishwa vyeo kufuatia kashfa ya Mwembechai.
Ukht Arafa alionyesha masikitiko yake kuwa pamoja na Waislamu kuomba tume iundwe, serikali ya Rais Mkapa imeendelea kukaa kimya kwa muda mrefu sasa huku ikikiri hadharani kupokea malalamiko ya Waislamu.
Alioanisha unyama wa Mwembechai na kadhia ya mabucha ya nguruwe ya mwaka 93 ambapo alisema Waislamu walifungwa kwa sababu ya kukemea uuzaji holela wa nyama ya nguruwe.
"Waislamu tuna kila sababu ya kuhisi kwamba serikali ya CCM haitupendi", alisema kwa masikitiko Bi Arafa.
Aidha aliwataka wanawake wa Kiislamu kutokubali kurubuniwa na baadhi ya taasisi au mashirika ya kigeni ambayo hivi karibuni yametangaza kuwapa mikopo na vyerahani.
Alisema, mashirika hayo yana 'agenda' ya kuwatumia wanawake kisiasa kwa maslahi yao.
Hadhari ya Bi Arafa imekuja muda mfupi tu baada ya Muslim World Congress kuandaa semina iliyohudhuriwa na wanawake wa Kiislamu jijini na mikoa ya jirani.
Semina hiyo ilifanyika katika ukumbi wa Starlight ambapo pamoja na mambo mengine washiriki walitakiwa wajiunge kivikundi sehemu wanazotoka ili iwe rahisi kwa jumuiya hiyo kutoa mikopo na misaada kwa wanawake kupitia vikundi hivyo.
Semina hiyo ilifunguliwa
na Makamu wa Rais Dkt. Omar Juma.
Na Muhibu Said
WAKRISTO 11 wameripotiwa kurejea katika Uislamu hivi karibuni kufuatia mihadhara miwili mikubwa iliyofanywa katika maeneo tofauti wilayani Kinondoni, Jijini na kikundi cha Khidmat Da'awah cha mjini Dar es Salaam.
Mihadhara hiyo iliyoongozwa na Mwenyekiti wa kikundi hicho, Ustadh Magezi Shaaban, ilifanyika wilayani hapo katika Msikiti wa Kwa Kidile, Mwananyamala 'A' kuanzia Aprili 18 hadi 28 na kwenye uwanja wa jengo la "Baytul Yatiyma", jirani na Msikiti wa Mkwajuni uliopo eneo la Kinondoni Mkwajuni, Jijini kuanzia Aprili 27 hadi Mei 5, mwaka huu.
Kati ya waumini hao wapya, saba wanatoka dhehebu la Roman Catholic, Kanisa la Lutheran mmoja, Anglicana mmoja, asiyekuwa na Kanisa mmoja na Mlokole mmoja.
Waumini wanne miongoni mwao walisilimu katika muhadhara uliofanyika katika Msikiti wa Kwa Kidile, Mwananyamala 'A' na wengine saba walisilimu katika muhadhara uliofanyika katika uwanja wa "Baytul Yatima", Kinondoni Mkwajuni, Jijini.
Kwa mujibu wa Ustadh Magezi, kikosi hicho hivi sasa kimehamia katika uwanja wa Temeke Mwisho, Jijini Dar es Salaam kikiendelea na muhadhara wake uwanjani hapo.
Aidha, Ustadh Magezi aliongeza
kuwa Taasisi yake ya Khidmat inakusudia kupanua Da'awah yake kwa kuwatawanya
zaidi wahadhiri wake katika kila kona ya nchi chini ya vikosi visivyopungua
vitano.
Katika hafla hiyo iliyoandaliwa na Jumuiya ya wanafunzi wa Kiislamu chuoni hapo, pamoja na mambo mengine, walimu hao pia waliahidi kuijenga upya historia halisi ya Tanzania na ya Uislamu na Waislamu nchini kisha kuwatanabaisha wanafunzi wao na jamii kiujumla ili wajue watokako, walipo na kule waendako.
Katika risala yao wanachuo hao waliziomba taasisi za Kiislamu kuwasaidia kujenga Msikiti, Maktaba na kuwapatia ajira pamoja na kuwaendeleza kitaaluma ili waifaidishe jamii ya Kiislamu kwa "kuwekeza" katika akili za watu (wanafunzi).
Naye mgeni rasmi alijibu risala hiyo, aliahidi kuyafanyia kazi maombi yao na kuwataka wahitimu hao kuwalea wana shule watakaokuwa nao huko waendako hususan wanafunzi wa Kiislamu, kwa misingi ya "kiutu". Mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Elimu wa Mnadhama Burhan Mtengwa.
Mapema katika hafla hiyo, mwalimu mlezi wa wanafunzi wa Kiislamu chuoni hapo aliwafahamisha Waislamu kuwa, chuo hicho kina wanafunzi 620 kati yao 74 wanachukua cheti na waliobaki stashahada.
Mwalimu huyo Bw. Muhammed Maje alisema kwamba wanafunzi wa Kiislamu chuoni hapo hawazidi asilimia 15 ya wanachuo wote, jambo ambalo si tu linatoa picha ya mbinyo wa wana shule wa Kiislamu katika sekondari na vyuo, bali pia unatoa changamoto kwa umma wa Kiislamu kukaza mkwiji katika suala zila la elimu.
Naye Ustadh Mbarara Abdallah katika mada yake; "Familia ya Kiislamu na malezi" iliyowalenga walimu hao kwenye hafla hiyo aliwataka wahitimu hususan wanawake waepuke mtego wa wale aliowaita kuwa ni madalali wa haki za wanawake, ambao huwarubuni mabanati wa Kiislamu kwa kisingizio cha ukombozi wa mwanamke.
Aliwaeleza wazi walimu hao kuwa kinachodaiwa sasa na "madalali" hao si usawa bali kufanana. Hivyo akawataka walimu hao wa kike wakawafunze mabanati wa Kiislamu huko waendako msimamo wa Uislamu kwamba haki za mwanamke ni haki za binadamu na sio vinginevyo. Na kuwa Uislamu ulikwishamkomboa mwanamke miaka 1420 iliyopita, kinyume na propaganda chafu za makafiri kwamba dini hiyo inamkandamiza mwanamke.
Wengine waliotoa nasaha zao ni pamoja na Ustadh Juma wa Masjid Kiblatain (Manzese), Jumuiya ya wanafunzi wa Jabal Hira, Mzumbe sekondari, IDM-Mzumbe, Kigurunyembe sekondari, At-Taawn Girls Islamic High School na Umoja wa Kikristo wa wanafunzi Tanzania (UKWATA) tawi la chuo hicho.
Wakati kwa upande wa Chuo (Wahadhiri) uliwasilishwa na Mwalimu Mrimbo ambaye alionyesha mshangao wake wa wazi kwa wanachuo hao wa Kiislamu kuagana Kiislamu wakati walikaribishwa kwa disko la kukata na shoka.
"...Kama mnavyoagana Kiislamu
basi pia mkaribishane Kiislamu. Na hii si kwa wanavyuo tu, bali hata wanashule
wa sekondari. Muwakaribishe wenzenu wa kidato cha kwanza na cha tano Kiislamu",
alisisitiza Mkufunzi huyo ambaye ni Mkristo (Mkatoliki).
--
|
|