Baada ya kauli ya Dk. Omar Ali Juma:
Kamata kamata yaanza tena Dar
 

Na Mwandishi Wetu

SIKU moja tu baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa Makamu wa Rais ameonya juu ya shughuli za Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu nchini kwa madai kwamba haijasajiliwa, baadhi ya waumini wamekamatwa na kupekuliwa majumbani mwao.

Aidha, kituo kimoja cha televisheni Jijini kimeripoti katika taarifa yake ya habari jana usiku kwamba Mh. Omar Ali Juma amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Alfred Gewe kushughulikia agizo lake la kuipiga marufuku Kamati ya Ponda.

Juhudi za gazeti hili hazikuweza kubaini idadi ya waumini waliokwisha kukamatwa kufuatia agizo hilo, hata hivyo limethitibitisha kukamatwa kwa muumini mmoja ajulikanaye kwa jina la Omar.

Muumini huyo alikamatwa jana mchana katika maeneo ya Msikiti wa Qiblatain ambapo huwa anauza kanda mbalimbali zikiwemo zile za mihadhara inayofanyika Mtambani pamoja na kanda.

Kufuatia kukamatwa kwa muumini huyo na taarifa zilizozagaa juu ya kupekuliwa kwa baadhi ya watu pakitafutwa vitu vinavyohusiana na Msikiti wa Mtambani au Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu, baadhi ya waumini katika Misikiti kadhaa walisikika wakisema kwamba itabidi kuanzia leo (jana) wayahame majumba yao kama ilivyokuwa wakati wa kamata kamata ya mabucha ya nguruwe na kadhia ya Mwembechai.

Wengi waliokuwa wakitoa kauli hiyo ni ama waathirika wa kadhia zilizotangulia.

Hayo yanafanyika wakati Rais Benjamin Mkapa akiendelea kutafuta ushauri na ushahidi wa kisayansi juu ya madai ya Waislamu kwamba wananyanyaswa hapa nchini. Madai ambayo Makamu wa Rais Dk. Omar Juma aliyakanusha katika mkutano wa hadhara ulioanyika maeneo ya Manzese wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za wananchi iliyomalizika Jumatano (juzi) wiki hii.

Swali kwa nini serikali inawanyanyasa Waislamu lililoulizwa na kijana mdogo wa Kimachinga, lilionekana kuamsha hasira kwa wana CCM waliohudhuria mkutano huo iliyopelekea baadhi yao kutaka kumvamia kijana huyo huku wakimzomea jambo ambalo lingeweza kusababisha mtafaruku kama ingekosekana busara ya baadhi ya wazalendo waliosimama kudhibiti hali hiyo.

Hata hivyo, kijana aliyeuliza swali hakuweza kuendelea kutokana na ghasia zilizokuwa zikifanywa na wakereketwa wa CCM ambao walisikika wakisema kuwa kijana huyo alitumwa na baadhi ya watu kuuliza swali hilo.

Akijibu madai ya kunyanyaswa Waislamu, Makamu wa Rais Dk. Omar Juma aliwauliza watu waliokuwa wakimsikiliza kama kulikuwa na yeyote ambaye angeweza kueleza ni katika maeneo yepi Waislamu wananyanyaswa, hata hivyo vitisho vya wakereketwa na hali nzima iliyokuwepo mahali hapo hakuna aliyethubutu kujitokeza.

Dk. Omar alionekana kutumia fursa hiyo kuwashutumu Waislamu hasa Kamati ya Sheikh Ponda na Msikiti wa Mtambani kwamba ni taasisi zinazotumiwa kuleta vurugu nchini.

Alisema serikali haijawaingilia Waislamu katika haki zao zinazohusu uhuru wa kuabudu ambazo alisema zimo katika kitabu chao kitukufu Qur'an.

Alizitaja haki hizo kuwa ni uhuru wa kuabudu, kufunga Ramadhani na kwenda kuhiji Makka.
 

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook