Mzee Issa Ponda azungumza Kigoma
 

Na Mwandishi Wetu

MZEE Issa Ponda baba wa Katibu wa Kamati ya Kutetea Haki za Waislamu Bwana Ponda Issa Ponda amewataka Waislamu kuungana katika yale yanayowaunganisha ili waweze kukabiliana na nguvu ya adui iliyowaelemea.

Mzee Issa alitoa wito huo wakati akizungumza na mwandishi wa habari hizi nyumbani kwake siku chache baada ya maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu yaliyofanyika kitaifa mkoani Kigoma.

Mzee huyo maarufu Kigoma aliwakumbusha Waislamu kuwa silaha yao ni ucha Mungu kwa mujibu wa kitabu cha Allah na mafunzo sahihi ya Mtume (s.a.w.).

Akizungumzia madai ya kusakwa kwa mwanawe na polisi mkoa wa Dar es Salaam, Mzee huyo wa Kibwari tapo maarufu la Kimanyema alisema watendaji wengi wa vyombo vya dola hawafahamu historia ya nchi hii matokeo yake wamekuwa wakifanya mambo kiupofu.

Alisema wangelifahamu vyema Tanzania ya kabla ya uhuru (Tanganyika) wasingeshiriki kufanya haya wanayoyafanya.

Aidha alisema anamuunga mkono mwanawe Ponda Issa Ponda kwa kuwa anatekeleza kile alichomfundisha.

"Kama ningesikia amefanya ujambazi mahali ningekuwa wa kwanza kuisaidia polisi, lakini anasakwa kwa kuwa anahimiza haki na uadilifu, mimi niko pamoja naye 'Hattaa ataanal yaqiin' (mpaka idhihirike yakini)", aliongea kwa msisitizo Mzee Issa.

Aliwaomba Waislamu wote nchini wapokee kama zawadi aya ya Qur'an isemayo:

"Je, watu wanadhani wataachwa kwa kuwa wanasema "Tumeamini?" Basi ndio wasijaribiwe. Hapana, bila shaka tuliwatia katika taabu wale waliokuwa kabla yao, na kwa yakini Mwenyezi Mungu atawatambulisha wale walio wakweli na atawatambulisha (wale walio) waongo. Je, wanadhani wale wafanyao maovu kwamba watatushinda (tusiwapate kuwapatia adhabu?) Hukumu mbaya hiyo wanayohukumu". (29:2-4)

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook