Maoni yetu
Ahadi ya Rais Mkapa Diamond kiini macho?
 

KAULI ya Makamu wa Rais Mh. Dk. Omar Ali Juma juzi imewaacha Waislamu wakiwa wametatizika. Kwamba je; aliyofanya Mh. Rais Benjamin William Mkapa pale Diamond Jubilee Hall wakati wa Baraza la Idd ni kiini macho? Au je uamuzi aliouchukua Mh. Rais kukubali mwaliko wa Baraza la Idd el Fitri pamoja na kuipokea risala ya Waislamu haukubaliki kwa viongozi wenzake na watendaji wa serikali?

Kauli tunayoizungumzia hapa ni ile aliyoitoa katika mkutano wake wa hadhara pale Manzese juzi. Mkutano ambao uliwavuta watu wengi hasa wa mbali ambao walikuwa wakija kwa magari ambayo haikueleweka kwamba waliyakodi wenyewe au walikodishiwa.

Wananchi walipewa fursa ya kuelezea kero zao baada ya hotuba ya Mheshimiwa Makamu wa Rais ambapo fursa hiyo waliitumia vyema. Hata hivyo, aliposimama kijana Muislamu kuelezea kero za Waislamu alizomewa sana na walioonekana kuwa wakereketwa wa CCM.

Kijana huyo aliogopa na akashindwa kuendelea kujieleza. Je, waliofanya kitendo kile waliandaliwa kuja kuwazomea Waislamu! Je, kero za Waislamu stahiki yake kuzomewa! Salamu gani wanapelekewa Waislamu katika kipindi hiki! Je, ingekuwa ni kero za Wakristo zinaelezwa zogo la kuzomea lingekuwepo!

Kama lengo lilikuwa kuzisikia kero za wananchi basi kero ya awali ilikuwa hii ya raia na mwananchi kuzomewa jambo ambalo linampora haki yake ya kujieleza na kutoa maoni yake. Tulitaraji Mh. Makamu aione kero hiyo iliyofanywa mbele yake, lakini kinyume chake kijana akazidi kuandamwa kwa madai kwamba katumwa na fursa hiyo ikatumiwa kuzuia shughuli za Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu kwa kujenga hoja kwamba haijasajiliwa.

Katika ziara zake na shughuli zake, Mh. Makamu wa Rais amekuwa akipambana na kuyashughulikia masuala mbalimbali ya Waislamu.

Huko nyuma aliwahi kulazimika kuingilia 'mgogoro' wa Msikiti wa Sinza. Katika kulazimika huko waliwahi kutumwa F.F.U. halikadhalika Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bibi Ritha Mlaki ambapo walivuruga staha, nidhamu ya Msikiti na Ibada zilizokuwa zikifanyika.

Lakini bado Waislamu wanajiuliza kipi kilimfanya alazimike kuingilia wakati yeye si mswaliji wa Msikiti huo, si mkazi wa Sinza, na ikiwa serikali haina dini!

Rais Mstaafu wa Zanzibar Mh. Aboud Jumbe aliwahi kushughulikia mgogoro wa kundi la Ijumaa na Dhuhr kule Bukoba, lakini kushughulikia kwake hakukuishia kwa DC na polisi kutumwa Misikitini kulidhibiti kundi moja.

Si muda mrefu uliopita alilazimika pia kuingilia suala la ikhtilafu za mwezi. Akaamrisha watu wafuate kauli ya Mufti na kuchukua azma ya kuwazuia wanaoswali kabla ya 'kibali' cha Mufti.

Katika mauaji yaliyofanyika Mwembechai mwaka jana ambapo Polisi waliua Waislamu kadhaa; Makamu wa Rais Mh. Dkt. Omar Ali Juma alikuwa miongoni mwa viongozi wa serikali waliotoa kauli hadharani kuunga mkono hatua zilizochukuliwa na polisi.

Kabla ya kauli ya Mh. Dkt. Omar Waislamu walikuwa wameshatoa madai yao kwamba wamedhulumiwa, wameuliwa na kudhalilishwa pasipo haki, Katiba na sheria za nchi hazikufuatwa. Na kwa ajili hiyo wakataka Tume ya uchunguzi iundwe na walioua wafikishwe mahakamani.

Pengine katika kuwatetea polisi Mh. Makamu wa Rais alidai kwamba hapana haja ya kuundwa Tume maana ukweli unajulikana. Na akaongeza kusema kwamba polisi sio mbwa; kwamba waweza kupopolewa mawe tu wasijihami.

Lakini je, ni kweli polisi walidiziwa na mawe! Na je, sheria za nchi ndivyo zinavyoagiza kwamba polisi akipigwa jiwe naye ajibishe kwa kumlenga mtu risasi ya kichwa au kifuani! Na awali ya yote kipi kiliwapeleka askari Msikitini hata wakapigwa mawe! Hayo ni baadhi ya maswali ambayo majibu yake yangetolewa na Tume ya uchunguzi na mahakamani. Lakini hayo Mh. Makamu wa Rais hakuzingatia.

Katika tamko la Manzese Mh. Makamu wa Rais amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa havikusajiliwa rasmi.

Maelezo hayo yalilenga kupiga marufuku shughuli za Kamati ya Kupigania Haki za Waislamu nchini. Na hiyo ilikuwa baada ya kumtuhumu kijana aliyehoji kunyanyaswa Waislamu kwamba katumwa.

Waliomtangulia kijana huyo hayupo aliyeshutumiwa kwamba katumwa na mtu, chama au 'maadui wa nje; japo walitoa kero nzito nzito. Inapokuja kwa Waisalmu yeye katumwa! Tuseme Muislamu yeye hana haki ya kulalamika hata akihisi kwamba anaonewa au kudhulumiwa! Au tuseme kauli hizi ni katika jumla ya vikwazo vya kuzuia haki kutendeka!

Kamati ya Waislamu iliwasilisha madai ya Waislamu kwa Mh. Rais Mkapa naye akayapokea kwa moyo mkunjufu pamoja na kuahidi kuyashughulikia. Kwa kauli ya Makamu wa Rais; kukanganyikiwa kumewasibu Waislamu. Je, ndio iwe yameyeyuka mategemeo yao kwa Mh. Rais kwamba yeye na Baraza lake la Mawaziri watatoa ufumbuzi wa yaliyokuwa kwenye risala ile!

Je, alichofanya Mh. Rais pale Diamond Jubilee ni kiini macho! Au alichofanya hakikubaliki kwa viongozi wenzake? Maana hata hiyo Kamati ambayo hivi sasa hujulikana kama Halmashauri Kuu ya Waislamu haikusajiliwa. Ilikuwa haikusajiliwa siku ilipo kabidhi risala ya Waislamu kwa Mh. Rais Mkapa na mpaka leo haijasajiliwa.
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook