SIKU moja nilitaka kufanya Experiment (jaribio) ya kupima ulimbukeni wa watu. Wazo la kufanya experiment (jaribio) lilikuja baada ya kugundua kwamba nilikuwa nimesahau ugali kwenye hot pot kutokana na kuwa bize kupita kiasi. Nilivyoutoa kwenye hot pot, ugali ule ulitoa harufu mbaya ya kuoza, kwani ulikuwa humo kwa siku nne au tano hivi. Ila ulikuwa na umbo zuri la duara.
Niliuchukua usiga wangu, (usiga kikwetu ni kiporo cha ugali), nikautafutia vitu vizuri vya kuupamba, ukawa kama keki. Niliwaalika watu ambao nilijua wanapenda visherehe sherehe, hasa vya kizungu, wenyewe wanaita minuso. Wakahudhuria, nikawapa vibiskuti na vijuisi kupoteza lengo, halafu nikatoa ile keki.
Kwanza kabisa nilitoa maelezo mafupi kuhusu keki yangu kwa kusema:
"Waheshimiwa waalikwa, sasa umefika ule wakati wa kula keki. Keki hii imeshuka jana jioni na ndege ya saa moja. Kwa hiyo bado iko fresh kabisa. Kwa wale wenzangu na mimi waliozoea minuso ya kimataifa wataifurahia keki hii, na ninadhani itawakumbusha mbali. Wale wengine ambao hawana uzoefu, keki hii inaweza ikawa na harufu na ladha ya ajabu, isije ikawatia kichefuchefu, wakatapika na kuchafua suti zao. Nawashauri waonje kidogo tu kupata uzoefu, au waache kabisa. Naomba wenye uzoefu wapite hapa mmoja mmoja niwalishe vipande vya keki spesho. Karibuni".
Baada ya kumaliza maelezo, mabibi na mabwana wote waliohudhuria walipanga foleni, kila mmoja akijidai ana uzoefu. Moyoni nikasema experiment yangu kweli imepata watu niliowataka. Watu walibugia vipande vya Usiga, na kila mmoja alijidai kuona ladha. Wengine wakajifanya kurudia ili waonekane babu kubwa, wana uzoefu wa minuso ya kimataifa, wakawa wanaukata usiga kifua mbele. Wengine niliwasikia wakisifiana kwa kusema "Ya, ya! Hii ni fresh from London!" Nilikuwa nachekea tumboni, ila moyoni niliwasikitikia.
Jabirio langu lilinipa uhakika kwamba ulimbukeni ni tatizo la kisaikolojia.
Nilikuja kupata uhakika siku nyingine. Nilienda kusalimia ndugu zangu fulani. Alikuwepo kisura mmoja niliyetambulishwa. Halafu wenyeji wangu wakaniambia kwamba kisura yule alihitaji kupelekwa nyumbani kwa jamaa yetu mwingine ambaye hakuna anayepafahamu anapokaa ila mimi. Nikapewa kazi ya kumpeleka. Nikasema hewala.
Tulipokuwa tunatoka nje, nilisikia sauti ya mtu mmoja akisema: "Sa Changwa leo kapatikana". Nilijua ana maana gani. Ni kwa sababu hakutegemea kama ningekubali kuongozana na kisura yule mitaani, maana nikianza chini kuja juu, alikuwa kavaa viatu vyenye kisigino kirefu, halafu kimechongoka kama msumari, akipita karibu yako weka mguu mbali. Miguu yote nakaribu nusu ya mapaja vilikuwa wazi, kwani alikuwa amevaa kijisketi kifupi mno. Juu kidogo zaidi alivaa kiguo kisichochomekeka. Kichwani alikuwa anamzigo wa makamba meusi yaliyosokotwa, wenyewe wanaita "rasta".
Tulipokuwa tunaelekea kituo cha basi, niligundua alikuwa anapata tabu kutembea. Mimi najua tabu ya kutembea muda mrefu ukiwa unakanyagia vidole. Kisigino kiko juu. Nilifanya zoezi hili wakati ule nilipokuwa napenda kucheza mpira. Ndivyo huyu dada alivyokuwa akitembea na viatu vyake.
Tulipofika kituoni tulipata daladala. Dada yule alivyokaa kwenye siti alipata tabu nyingine. Alijitahidi saana kuitafuta sketi yake ili aivute imfunike, lakini mkono ukawa hauifikii ile sketi. Moyoni nilijisema: "Utaipata wapi, babu we! Haipo!" Hiyo ndiyo tabia ya sketi fupi. Inapotea mtu akikaa, usiombe akienda sokoni kununua nyanya zilizopangwa chini.
Tabu ya tatu aliyoipata ni kwamba, wakati mkono mmoja unajaribu kuifikia sketi ili aivute imsitiri, mkono mwingine ulikuwa una kazi ya kupekenyua mzigo wa kamba alizofunga kichwani ili ajikune. Inaelekea kichwa kilikuwa kinawasha. Hiyo ni tabia ya kichwa kikikosa maji na sabuni kwa siku kadhaa.
Kwa vile nilishafanya jaribio la keki ya Birth day, sikupata tabu kuuliza kwa nini yule kisura alikuwa akiteseka vile. Ni yale yale ya kula Usiga iil usionekane mshamba. Na huyu kisura alikubali mateso yote kwa gharama ya kuonekana mwanamke wa kisasa. Mateso yote yale ni kwa ajili ya kuwapendeza wenye macho. Na sio mateso tu, bali na gharama nyingine. Zile kamba za kichwani kanunua dukani, na bado akaenda saluni kulipa fedha ili afungwe zile kamba kichwani. Yote nini? Aonekane mzuri, wa kileo, sio wa kuja, japo anateseka. "Kuburudika" kwa watu wanapomuangalia ndio thawabu yake. Mwenyezi Mungu anasema:
"...Na anayetaka thawabu ya dunia tutampa...".
Muislamu hawezi kupata kichaa hiki cha ulimbukeni wa kula usiga na kujiaminisha kuwa ni keki, tena ya birthday, wala kuteseka kwa ajili ya kufurahisha watu, au kujikweza. Muislamu yuko radhi kuteseka kwa ajili ya Mola wake tu.
Mambo yote ya kikafiri yako hivyo. Ni usiga uliofanywa keki. Juu juu unaonekana fresh from London, lakini ndani ni uozo. Ndio maana dunia leo haina raha wala amani, ila watu tu wanavumilia ladha na harufu ya usiga ili wasionekane washamba. Lakini wanajua na wanaona kwamba wameharibu kila kitu, na bado wanavurunda, na watavurunda hadi ulimbukeni ututoke!
Kuna wale wanaojiita Waislamu lakini wanaiga ulimbukeni huu wa kula usiga na kujifanya wanakula keki. Utakuta nao wanaiga haya, kuvaa kwao, sherehe zao, na wao pia eti wameingia kwenye ulimbueni wa kuiga mambo ya Kizungu, Muislamu naye leo anasherehekea Birthday, na kupata magharama yasiyo ya lazima. Unachosherehekea ni nini hapa, kwa lipi ulilolifanya lenye manufaa, au basi tu na wewe upate hasara kwa faida ya kuitwa wa kisasa. Mtume (s.a.w.) aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa kufunga, sio kwa ulimbukeni.
--
|
|