Mafundisho ya Qur'an
 
Harakati za Mitume zililenga kusimamisha haki katika jamii
 
 

Kwa mujibu wa Qur-an ujumbe wa mitume hasa mitume mursaliin(Prophet-revolutionaries), watumishi wa Allah na viongozi wa wanyonge (wafuasi wa mwanzo kupokea ujumbe wa wa Allah), kiujumla ulikuwa na madhumuni matatu: Mosi, kuusimamisha ukweli unaotoka kwa Allah; pili, kuendesha mapambano dhidi ya Baatil, ukandamizaji na dhulma na tatu, kuunda jamii au udugu wa kijamii unaotokana na usawa, wema, uadilifu na upendo.

Musa dhidi ya Firauni ni mfano wa ulinganisho wa nguvu mbili pinzani kati ya mema na maovu, haki na baatil, ukweli na uongo. Qur-an imeeleza hili katika aya kadhaa kuwakilisha mahasimu(adui) wawili. Nguvu ya matajiri na Makuhani (Masheikh) walioshirikiana na tabaka tawala lililojenga kiburi dhidi ya wanyonge, mafukara, watumwa, madhaifu, makabwela, wajane, mayatima na wale wote walioonekana si chochote machoni mwa watawala. Hatimaye mitume wakiongoza wanyonge waliokubali kushikamana na haki(ukweli) waliibuka washindi dhidi ya madhalimu:

"Tunakusomea habari za Musa na Firauni kwa (njia ya ) haki kwa ajili ya watu wanaoamini.

Hakika Firauni alitakabari katika ardhi, akawafanya watu wa huko makundi mbali mbali. Akalidhoofisha kundi moja miongoni mwao, akiwachinja watoto wao wanaume na kuwaacha hai watoto wao wanawake. hakika yeye alikuwa miongoni mwa waharibifu(kabisa).

Na tukawafanyia ihsani wale waliodhoofishwa katika ardhi hiyo na kuwafanya viongozi, na kuwafanya warithi(wa neema hizo).

Na kuwapa nguvu ardhini; na kumwonyesha Firauni na Hamana na majeshi yao, yale waliyokuwa wakiyaogopa". (28:3-6).

Harakati za mtume Musa kwa kaumu yake kimsingi zilikuwa dhidi ya nguvu ya wachawi na wakandamizaji. Aliasi serikali ya Firauni na kukwaruzana na makundi au matabaka yaliyonufaika na mfumo mbovu wa kijamii uliokuwepo . Hatimaye aliangusha utawala huo kufuatia tukio la kihistoria la Firauni na jamaa zake kuzamishwa baharini. Hivi ndivyo Allah alivyowaahidi waja wake wema wa zama zote wenye kupigania haki kwamba mwisho wa mapambano ya haki ni ushindi kwa waumini licha ya hila na madhila kutoka kambi ya adui:

"Na tutakukalisheni(nyinyi) katika nchi hizi(hizi) baada yao." Watapata haya wale walioogopa kusimamishwa mbele yangu na wakaogopa maonyo yangu."

Na walitafutatafuta(walipeleleza na kupanga njama), na akashindwa kila jabari mkaidi(14:14-15).

Sifa kuu ya Mitume ni ucha Mungu ambao uliowaongoza wao na wale waliowafuata kuuelekea ukweli na usawa wa kijamii. Walikuwa watu madhubuti, wema, wenye huruma wanaojali shida za watu na wanyenyekevu. Walijitolea kila walichokuwa nacho kwa ajili ya kuisimamisha haki ulimwenguni. Waliteswa, walikataliwa, walibughudhiwa, kukejeliwa na wengine kuuawa:

Je! Hazikukujieni habari za wale waliokuwa kabla yenu? Watu wa Nuhu na Adi na Thamudi na wale wa baada yao ambao hakuna awajuaye ila Mwenyezi Mungu? Waliwajia Mitume wao kwa hoja zilizo wazi wazi. Wakarudisha mikono yao juu ya vinywa vyao, na wakasema(kuwaambia Mitume hao) "Hakika sisi tunayakataa mliyotumwa nayo. Na hakika sisi tunayo shaka ituhangaishayo kwa hayo mnayotuitia(ya kumuabudu Mwenyezi Mungu mmoja).

Mitume wao wakasema: Je! Mnamfanyia shaka Mwenyezi Mungu. Muumba wa mbingu na ardhi? Yeye anakuiteni akusameheni dhambi zenu na akupeni muhula mpaka muda uliowekwa." Wakasema"Hamkuwa nyinyi ila ni watu kama sisi. Mnataka tu kutuzuilia na yale waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu. Basi tuleteeni hoja zilizo wazi.

Mitume wao wakawaambia: Sisi hatukuwa ila ni watu kama nyinyi(kama mnavyosema). Lakini Mwenyezi Mungu huwafanyia ihsani awatakao katika waja wake. Wala sisi hatuwezi kukuleteeni hoja hizo isipokuwa kwa ruhusa ya Mwenyezi Mungu. Na kwa Mwenyezi Mungu wategemee Waislamu(wote)."

"Na tuna nini tusimtegem

ee Mwenyezi Mungu, na hali ametuonyesha njia zetu. Na tutayavumilia mnayootuudhi. Basi kwa Mwenyezi Mungu tu wategemee wategemeao."(14:12).

Na wale waliokufuru wakawaambia Mitume yao: "Tutakutoeni katika nchi yetu au lazima murudi katika mila yetu." Basi Mola wao akawaletea wahyi kuwa "Tutawaangamiza madhalimu(14:9-13).

Hawa ndio mitume wa Allah, wanaadamu walioongoza harakati za kusimamisha haki katika ardhi. Wanaadamu walioanzisha harakati za ukombozi wa wanyonge na madhaifu. Waliolazimika kuhamia ugenini pale ilipobidi ili kupata fursa ya kuendesha harakati dhidi ya mifumo dhalimu. Katika vita hii mitume walihimili magumu kijasiri, walikuwa wavumilivu wasiokata tamaa wala kujitweza kwa madhalimu:

Mwenyezi Mungu amenunua kwa Waislamu nafsi zao na mali zao ili na yeye awape Pepo. Wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu; wanaua na wanauawa. Hii ndiyo ahadi aliyojilazimisha (Mwenyezi Mungu) katika Taurati na Injili na Qur-ani. Na ni nani atekelezaye zaidi ahadi yake kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye. Na huko ndiko kufuzu kukubwa.(9:111).

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook