Kukamatwa kwa wahubiri wa Kiislamu Nzega:
Anayedaiwa kuwa mlalamikaji akana kuwashitaki watuhumiwa

SHEIKH wa Wilaya ya Nzega mkoani Tabora, amekanusha madai kwamba amehusika kuwasilisha polisi tuhuma dhidi ya Waislamu 15 waliokamatwa kufuatia mhadhara wa kidini uliofanyika wilayani humo hivi karibuni.

Sheikh Muhammed Ibrahim amekanusha madai hayo baada ya makundi ya Waislamu mjini hapa kumlaumu kwa kuwashitaki waumini hao badala ya tofauti zilizosemekana kujitokeza kujadiliwa katika vikao vya Waislamu wenyewe.

Miezi miwili iliyopita polisi mkoani Tabora iliendesha operesheni maalum kuwasaka watu waliodaiwa kutoa kashfa katika mahubiri yao dhidi ya kiongozi mmoja wa dini wilayani Nzega.

Kamanda wa polisi mkoani Tabora Bwana Ignas Mtana katika mazungumzo ya simu na gazeti hili alikiri baadaye kukamatwa kwa watu 15 kwa madai ya uvunjaji wa sheria na kutoa mahubiri ya matusi dhidi ya baadhi ya watu wilayani humo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Nzega mtu aliyedaiwa kupeleka taarifa hizo polisi ni Sheikh wa wilaya hiyo.

Akiongea na mpasha habari wa gazeti hili mjini Tabora hivi karibuni Sheikh Mohammed Ibrahim alionyesha mshangao wa jinsi yeye alivyohusishwa katika kesi hiyo kama ndiye mlalamikaji wakati hajawahi kufikisha polisi tuhuma za kukashifiwa.

Alisema yeye anaunga mkono mahubiri ya wahadhiri hao kwamba yanatokana na vitabu vya dini na kusema kama polisi mkoani Tabora ilikerwa na mahubiri hayo basi ingetafuta sababu nyingine ya kuhalalisha ukamataji huo dhidi ya wahubiri.

Watuhumiwa hao wako rumande na dhamana yao kuzuiliwa miezi miwili sasa.

Kwa mara ya mwisho walipofikishwa mahakamani dhamana ilizuiliwa kwa hoja kwamba familia ya anayedaiwa kuwa mlalamikaji ambaye ni Sheikh Mohammed Ibrahim ingekuwa hatarini.

Hata hivyo alipohojiwa Sheikh mwenyewe kuhusiana na swala hilo alisema mbali ya yeye kuhusishwa na lalamiko ambalo halifahamu pia hana mahusiano mabaya na watuhumiwa na vile vile familia yake haijawahi kuripoti polisi kutishiwa maisha na baadhi ya watu.

Japo katiba ya nchi inaeleza kuwa serikali ya Tanzania ni ya kisekula hata hivyo, katika masiku ya hivi karibuni vyombo vya dola hususan polisi imekuwa ikiingilia shughuli za Waislamu na kuwakamata wahadhiri wake kwa tuhuma ambazo baadaye hushindwa kuzithibitisha hali inayopelekea hisia mbaya miongoni mwa wananchi kuwa watendaji wa chombo cha dola ambao hujikuta wengi ni wa dini moja hutenda kwa hisia za dini yao badala ya kuzingatia sheria na kanuni za nchi.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook