Na Abu Burhanuddiin
WATUKUFU Waislamu madai ya msingi ya Waislamu ni yapi? Vyeo na madaraka? Elimu sawa? Ukadhi!, OIC? Mizengwe kwenye kuwekeza? Mihadhara! Au ruhusa ya haraka haraka ya kuandikisha Jumuiya na taasisi za Kiislamu? Makala hii itaonyesha kwa kina madai yetu ya msingi hasa ni yapi.
Maoni yetu, ndiyo-siyo
Tunaposema Waislamu tunadai haki zetu serikalini tuna maana gani? Au tunaposema tumedhulumiwa na serikali tuna maana gani! Yaelekea kuna fikra tofauti zinazotembea miongoni mwa tunaolalamika.
Inayojiita Halmashauri Kuu ya Waislamu Tanzania imetaja mambo kadhaa kuwa ndio kero au haki au tuseme maeneo ambayo Waislamu wamedhulumiwa au kulalamikiwa. Waliosoma Waraka wa Kamati ya Kusimamia haki za Waislamu iliyosainiwa na Bwana Ponda ambayo ndio sababu halisi iliyopelekea vyombo vya Dola kutangaza kumtafuta ina lugha hiyo hiyo. Warsha ilipokuwa hai, nayo ilitumia lugha hiyohiyo. Ni hivyo hivyo kwa wahadhiri katika mihadhara na hata Tahariri za ANNUUR na makala zake muelekeo ni huo huo pia.
Hivyo ni dhahiri kuwa wengi wetu tunapozungumzia haki za Waislamu tunafikiria kuwa na Makadhi, kupewa pengine kwa upendeleo vyeo serikalini na kupewa nafasi sawa kwenye elimu na kama haya.
Madai yetu ya msingi
Halmashauri Kuu imeongeza suala la Mwembechai, OIC na mizengwe Waislamu wanapotaka kuwekeza na kucheleweshwa kwenye tasjila za Taasisi za Kiislamu.
Maeneo haya ni muhimu na hayadharauliki, lakini watukufu Waislamu hisia ambazo wengine tunakuwa nazo tunapotamka haki za Waislamu maana ya msingi kabisa ni kulinda na kuhifadhi Uislamu wetu nchini kwetu. Kulinda na kuuhifadhi Uislamu wetu nchini kunahitaji makubaliano ya msingi kabisa ya namna ya kuendesha nchi baina ya sisi Waislamu na Wakristo ambao wanatufuatia kwa wingi kwamba tutaendesha nchi hii kwa misingi ya dini zetu bila kudhulumiana na kulinda mazingira ambayo huenda yatakuja kuparaganya nchi.
Hapa ndipo penye tatizo: Dhulma kwa Muislamu ipo pale Uislamu wenyewe unapopigwa vita na kudhoofishwa; kupewa madaraka bila kulinda Uislamu kazi bure. Muislamu kupewa Uwaziri lakini akaendeleza sera za kuua Uislamu sio kuwafanyia haki Waislamu ni kuwadhulumu. Kumpa Urais Muislamu lakini aongoze kwa misingi ya kuukana Uislamu ni kuudhulumu Uislamu na Waislamu. Ndio maana watukufu Waislamu enzi ya Rais wa kwanza ambaye ni Mkatoliki aliwaweka ndani Masheikh. Lakini wakati wa Rais aliyemfuatia pia ingawa ni Muislamu aliwaweka ndani Masheikh na kuwafunga kwa kusingiziwa kuvunja mabucha ya nguruwe.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa sasa Muislamu kawaweka rumande Waislamu kwa miezi kadhaa kwa hoja ya mihadhara, wakati anafahamu kuwa kazi waliyokuwa wanafanya wahadhairi ni ibada na wanapata thawabu. Kama si mbunge wa Kigamboni na wazee wengine kwenda kwa Rais wangeozea ndani achilia mbali waliofia gerezani.
Usishtuke hii ni pamoja na ukweli kuwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai wa Mkoa, Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai Taifa, Mkuu wa Jeshi la Polisi Polisi Taifa, wote hao ni Waislamu. Wote hawa wanajua walichokuwa wanafanya wahadhiri wale kuwa ni Uislamu kwa Mwenyezi Mungu wanathawabu, lakini mbele ya Dola ya Tanzania ni wahalifu, wana hatia ya kufungwa.
Aliyeunda Maparole mara ya kwanza ni nani? Ni Waziri wa Mambo ya Ndani ambaye ni Muislamu. Kwanini aliweka Wakristo watupu? Alikuwa anafuata system (muelekeo) wa nchi katika kufanya mambo yake.
Waziri wa Elimu ni Muislamu, alipanga mitihani siku za Idil Fitr mpaka Rais alipotengua. Kwanini? Sababu ni ile ile kuwa mtiifu kwenye System ya Kikristo.
Mkondo wa fikra hii ni huu, hata utakapotaka upewe Kadhi. Kwani Mufti na Kadhi katika Uislamu wanatofauti? Mufti tunae kwa miaka zaidi ya ishirini (20) sasa anausaidiaje Uislamu? Kadhi atasimamia sheria gani katika serikali isiyokuwa na dini na isiyotambua dini za raia wake ila inasema tu watu wana uhuru wa kuabudu ili mradi hawavunji sheria!
Hapa nchini hivi sasa kuna Mabaraza ya usuluhishi ya BAKWATA yaliyotokana na sheria ya ndoa ya mwaka 1971. Ni kweli yanasimamia sheria za Kiislamu au ni wakala tu wa serikali na hukumu ziko mahakamani?
Hivi sasa Kadhi wa Unguja, pamoja na nchi kuwa na Waislamu asilimia 99.9 sheria zote zinazotumika ni za Kiislamu? Kadhi wa Uganda na Kadhi wa Kenya ni nyadhifa za kisiasa au Makadhi wa Uislamu?
Nifupishe kwa kusema kuwa naamini hoja yangu imeeleweka nayo ni kwamba madaraka, nafasi za elimu, kuwa na makadhi na kadhalika, kweli ni mambo muhimu lakini haya ni matokeo (off shoot) ya utaratibu wa uendeshaji nchi, hivyo madai haya sio ya msingi kwetu abadan. Msingi wa nchi ni Katiba. Katiba ya Dini ya kikafiri lakini inalazimisha iendeshe wananchi ambao dini zao sio (ukafiri) secularism; ni Uislamu na Ukristo ndio tatizo la msingi, ambalo likifumbiwa macho kwa mategemeo dini ya Secularism kwa vile ndiyo Dini ya Dola itawalazimisha Waislamu na wengineo kuwa chini yao ni ndoto isiyoitakia mema nchi hii?
Katiba ya Kisekula kisha ikaandika mambo ya dini ndiyo iliyotufikisha hapa tulipo. Eti nchi haina dini lakini watu wake wana dini. Watu wana uhuru wa kuabudu ila wasivunje sheria!
Hii ndio pumbao la siasa lililotufikisha hapa tulipo. Kwa Katiba za namna hii inawezekana kuimarisha Ukristo nchini na kudumaza Uislamu. Rais wa Pili ingawa alikuwa Muislamu hakuweza kuusaidia Uislamu kwa sababu muundo wa uendeshaji nchi unapinga Uislamu.
Kwa hiyo haki zetu ni pamoja na kudai kwa nguvu zote Katiba itakayotambua kuwepo kwa Uislamu na Waislamu nchini. Katiba itambue Uislamu kuwa ndio njia ya maisha ya Waislamu, hivyo ki-nchi kisifanyike chochote cha kufuta Uislamu moja kwa moja au kwa kuzungaka. Hali iwe hii hii kwa Ukristo na dini nyingine zenye wafuasi wengi na mfumo kamili wa maisha.
Hii ndio agenda yetu, hii
ndio haki yetu ya msingi, kwa namna hii tutalinda na kuhifadhi Uislamu
wetu, namna nyingine yoyote ile haitatusaidia. Tutabakia tu Waislamu wa
majina na kutumikia ukafiri na hatimaye Uislamu utatoweka kabisa (Mungu
apishie mbali) kwa kutumia sera za kikafiri.
--
|
|