Ndugu Mhariri,
Naomba nafasi kabika gazeti letu ili nipate kutoa kueleza mtazamo mbaya walionao baadhi ya Waislamu juu ya Ufadhili.
Baadhi ya Waislamu kwa kuona kuwa Uislamu ni Dini ya Allah (s.w.) yaani umefaradhishwa na Mwenyezi Mungu (s.w.) basi wanaitarajia isimame na kufanya kazi kimiujiza ujiza bila ya wao kutoa na kufanya jitihada zozote.
Ni kwa mtazamo huu mbaya, Waislamu walio wengi hawaoni kuwa ni jukumu la kila Muislamu kujitolea mali, Elimu (ujuzi) na muda wao katika kuwasimamisha na kuupeleka mbele Uislamu.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba siku hizi kumezuka na kujengeka dhana ya ufadhili kwa upande wa matajiri (Walio jaaliwa) na ufadhiliwa kwa upande wa Wasionacho (maskini). Kwa mana nyingine Waislamu ambao ni matajiri wanaona kwamba haiwalazimu yaani si jukumu lao kuupigania Uislamu kwa kutoa mali, nafsi na muda wao bali wao wanafadhili tu (wanasaidia tu), na kwa upande mwingine Waislamu wenye kipato kidogo nao wanaathiriwa sana na fikira za kufadhiliwa kiasi ambacho hata kama wanaweza kufanya jambo kwa awamu kwa kuchangishana wao wenyewe husubiri ufadhili.
Ni lazima tufahamu kwamba katika harakati za kuusimamisha Uislamu, maswahaba wa Mtume (s.a.w.) walitoa mali zao, nafsi na muda wao ili tu Uislamu usimame. Hawakutoa yote haya kwa mtazamo wa "ufadhili" (Kusaidia tu) bali walifanya haya kukufahamu kuwa huo ulikuwa Wajibu wa jukumu lao kama Waislamu. Na ni kutokana na jitihada hizo zilizofanywa na Mtume na Maswahaba zake ndipo Mwenyezi Mungu akawazesha Uislamu kutawala Dunia.
Aya ifuatazo zinatoa msisitizo wa kutoa mali na Nafsi kwa ajili ya Uislamu sio "Kuufadhili" yaani kusaidia tu kwa matashi yako:
"Enyi mlioamini! Je, nikujulisheni biashara itakayo kuokoeni na adhabu iumizayo? Muamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Piganieni dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu, nayo ni bora kwenu ikiwa mnajua." (61:10-11).
Saidi Ally Mubarakh
Ubungo Islamic College
of Education.
Ndugu Mhariri
NAPENDA kutoa shukrani zangu za dhati kwa gazeti lako kwa kunipatia fursa hii ya kuungana na vijana wenzangu wa Kiislamu.
Litakuwa ni jambo la kushangaza sana kwa kijana wa kiume kuonekana akivaa heleni, "cheni ya gold", kusuka nywele na kadhalika halafu aseme anaenda na wakati. Huku kutakuwa ni kujidhalilisha kijinsia, kupitwa na wakati.
Pia nao dada zetu acheni mambo ya kujifanya mnakwenda na wakati kumbe mmepitwa na wakati. Ni jambo la kushangaza sana pale mwanamke anapojichubua kwa kutumia vidonge au njia mbalimbali ya kumfanya abadilike rangi na kusahau au kumletea kibri yule aliyemuumba katika umbo lililo bora zaidi kuliko hilo analolitafuta na kulihitaji.
Pia sio kujichubua tu bali mpaka kufuga kucha kama chui, kuvaa nguo zinazobana, zenye kuonyesha ramani ya miili yao, zingine zilizopasuliwa mpaka kwenye shemu za mapajani, kutembea vichwa wazi na kadhalika huku nako sio kwenda na wakati bali ni kujidhalilisha kijinsia.
Kwenda na wakati ni kumudu kupambana na mazingira mapya na ukaweza kuibuka mshindi ukiwa mwanadamu bora zaidi; mume bora zadi na mke bora zaidi.
Abdulhamiid Y. Asaly,
Ubungo Islamic High School,
P.O. Box 55105,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri,
Hatuna budi kumshukuru Allah (s.w.) kwa kutujaalia kupata fursa katika gazeti hili yakutoa dukuduku letu la kutaka kujua ni namna gani walelewe vijana wa Kiislamu ambao wana umri kati ya miaka 15-25, wanaolelewa mbali na nyumbani kwao, mfano katika shule za bweni, vyuo na vituo mbalimbali, na hawakulelewa katika misingi ya Kiislamu katika utoto wao hali ya kuwa wazee wao ni Waislamu.
Kwa mfano, katika shule nyingi za Kiislamu hivi sasa, tabia za vijana zinaenda kinyume kabisa na matakwa ya Allah (s.w.). Vijana wengi wa kike na wa kiume huamua kuvaa mavazi yasioendana na misingi ya Kiislamu, wawapo katika mazingira ya shule na nje ya shule. Pia heshima hakuna kabisa kati ya ujana huo na walezi wao, lugha za (matusi) zisizokuwa na maana zimekuwa ni kama maji ya kunywa.
Aidha miziki shuleni imekuwa kama Ibada. Kwa mfano kijana hawezi kulala wala kusoma mpaka asikilize muziki. Pia mambo muhimu atakiwayo Muislamu afanyi hayafanywi ipasavyo kama vile Swala na mengineyo.
Je, vijana hawa walelewe kwa misingi ya Tawhiid pekee kwa kuhofia kuwa nguvu itakapotumika watamshirikisha Allah (s.w.). Kama hivyo ndivyo mbona wakati wa Mtume (s.a.w.) alikuwa akiwalazimisha wale wote waliofikia kiwango cha kulipa kodi walipe. Vipi kuhusiana na suala hili katika kumshirikisha Allah (s.w.).
Je, Sheria zimewekwa na Allah (s.w.) ili zivunjwe? Na kama hivyo sivyo kwa nini wanaozivunja wasishughulikiwe? Tunaambiwa kwamba wakati wa Mtume (s.w.) kulikuwa na mahakama ilikuwa inawahukumu wale wote waliokuwa wakivunja sheria za Allah (s.w.).
Aidha walezi wa vijana hawa wanapowaacha vijana wao wafanye wapendavyo ati kwa kuwa hao wanajua baya na zuri. Wanaliangaliaje suala hili?
Je, vijana hawa watakapowaathiri wale ambao walikuwa wakifuata sheria za Allah (s.w.) kwa ukamilifu, hilo halitakuwa ni tatizo tena kwa jamii nzima? Kutokana na uzembe wa walio wachache?
Tunamalizia kwa kumuomba Allah (s.w.) awawezeshe Waislamu wasomaji wa gazeti hili waweze kulipatia suala hili jawabu muafaka kwa kufuata mwongozo wake Allah (s.w.).
Mwanafunzi Muislamu,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
MUUNGANO wa mwaka 1964 ambao unatimu miaka 35, ulitokana na kuunganishwa nchi mbili huru Zanzibar na Tanganyika. Katiba ya Muungano inatamka wazi kutakuwa na serikali ya Muungano ambayo itakuwa na mamlaka juu ya mambo yote ya Muungano katika Jamhuri ya Muungano pia juu ya mambo yote yahusuyo Tanzania Bara (Tanganyika).
Kwa vile Rais wa Zanzibar ameondolewa ndani ya serikali ya Muungano ni wazi kuwa Wazanzibari hawawakilishwi ndani ya Muungano. Kutuwakilisha huku kwa Wazanzibari kumeathiri sana maendeleo ya Zanzibar katika maeneo mengi, miongoni mwayo Mambo ya Nje.
Kupitia wizara hii Wanzanzibari wananyimwa kushiriki kimataifa katika mambo ya Muungano mfano Afya, Elimu, Michezo na jamii. Vile vile licha ya kuwa misaada na mikopo kutoka nje inaendeshwa kimuungano lakini serikali ya Muungano imelikana jambo hili kama si la kimuungano, matokeo yake ni Wazanzibari pekee ndio waliozuiliwa misaada, ilhali serikali ya Muungano (Watanganyika) wanaendelea kupata misaada kutoka nchi wahisani. Hapo nyuma wakati Zanzibar ilipojiunga na OIC serikali ya Muungano iliilazimisha Zanzibar kujitoa OIC bila ya kuzingatia kama mambo ya kidini hayaendeshwi kimuungano.
Mahakama Kuu ya Rufaa: Ibara ya 117 (3) ya katiba ya Muungano inaipa mahakama hii uwezo wa mwisho wa kuamua kesi zote zilizoanzia mahakama kuu za Zanzibar na Tanzania (Tanganyika). Zaidi ya 90% ya Wazanzibari ni Waislamu na Zanzibar ipo Mahakama ya Kiislamu ya Kadhi na mambo yote ya kidini Tanzania hayaendeshwi kimuungano. Sasa iweje mahakama hii isiyo na Sheikh hata mmoja iwe na mamlaka ya kuamua mambo yote ya Kiislamu ya Zanzibar?
Maliasili ya mafuta: Zanzibar mpaka sasa haina maliasili yoyote, Tanganyika kuna madini ya thamani kama dhahabu, almasi, Tanzanite n.k. Kuna uwezekano mkubwa kutokana na ushahidi wa mashirika ya NORAD, PETRO CANADA, AGIP, BP na SHELL kwamba Zanzibar mafuta (Petroleum) yapo, visima viwili viliwahi kuchimbwa Pemba na AGIP, BP na SHELL kinachoshangaza hapa madini ya Tanganyika hayaendeshwi kimuungano na Zanzibar haifaidiki na chochote nayo, lakini mafuta (Petroleum) yameainishwa pekee kuwa yanaendeshwa kimuungano.
Mambo ya sarafu: Chombo husika na jambo hili ni Benki Kuu ya Tanzania chini ya sheria ya Benki Kuu (Act. No. 12 of 1966). Ikumbukwe kuwa kabla ya kuvunjika kwa jumuiya ya Afrika Mashariki 1977, kulikuwepo na East African Currency Board (EACB), Zanzibar ilikuwa mwanachama wa Bodi na ikiwakilishwa hivyo ikipata faida na mikopo moja kwa moja kutokana na shughuli zote za bodi hii. Lakini mara tu baada ya jumuiya hii kuvunjwa, Benki Kuu ya Tanzania ikajitwalia haki zote za Zanzibar toka EACB. Isitoshe Zanzibar haiwakilishwi katika Bodi ya Benki Kuu ya Tanzania wala haifaidiki na shughuli za kibiashara za Benki hii isipokuwa kununua noti kwa ajili ya matumizi yake ya kawaida tu.
Mbali ya Zanzibar kumezwa katika mambo hayo serikali ya Muungano haizungumzii chochote kisheria kuhusu uwakilishi wa Zanzibar kwenye Bodi za: Baraza la Mitihani (NECTA), Shirika la Ndege (ATC), Shirika la Simu (TTCL).
Zanzibar haifaidiki kutokana na biashara ya mashirika haya. Matatizo ambayo yamepelekea Zanzibar kukabidhi mamlaka (Sovereignity) yake kwa Watanganyika kupitia Muungano na Watanganyika kubaki na sovereignity yao ndani ya Muungano yanatokana na muundo usioridhisha wa serikali mbili uliopo sasa na ambao viongozi wa CCM wanaushikilia bila ya kujali athari wazipatazo Wazanzibari kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni.
Kutokuwakilishwa huku kwa Wazanzibari (SMZ) ndani ya serikali ya Muungano kumeufanya Muungano kuwa kama dongo tepetepe ndani ya mikono ya wafinyazi (Watanganyika), kuutumia penye manufaa nao na kukaana penye hasara nao, haya ndio matunda ya Muungano kwa Zanzibar.
Shoka Shamte,
Pemba,
Zanziar.
Ndugu Mhariri
NAMSHUKURU Mwenyezi Mungu Allah (s.w.) alieumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake. Kwa kunijaalia kuishika kalamu hii, kwa uweza wake, na kuweza kuyaandika haya machache, sifa njema zinamstahiki Mwenyezi Mungu Allah (s.w.).
Jibu la Ustadh Ally Sadiki katika barua yake iliyotoka katika siku hiyo, alipenda afafanuliwe kuhusiana na alivyosikia kwamba kuna Hadith moja ya Bwana Mtume (s.a.w.) inasema kwamba kila kilichopo ardhini kimelaaniwa isipokuwa vitu viwili tu, Qur'an na msomaji wa Qur'an.
Baraka, ni kuifuata Qur'an, utapata baraka na kuepukana na laana. Na usipoifuata Qur'an ambayo inakumbusha vitabu vilivyotangulia na kuonya na mengineo, utapata tabu hapa duniani bila ya kujitambua na itakupelekea kumkufuru Muumba wako. Hata katika hali ya kumshirikisha na hadi umauti umekukuta, na hiyo laana ndio itakufika.
Uasi ulimpelekea Ibilisi kukosa Rehema au kutokurehemewa; akalaaniwa.
Mtu hujilaani mwenyewe kwa kumuasi Allah (s.w.).
Nampongeza Ustadh Idd S. Kikong'ona wa Morogoro kwa shairi lake zuri. "Hawa ndio waja wema". Pia anijulishe anuani yake kamili.
Salim Kingale Muhammed,
S.L.P. 2354,
Tanga.
--
|
|