Uhuru Jumanne, Aprili 4, 1967
MABEBERU pamoja na makabaila wasiopenda ustawi wa nchi zetu za Afrika ya Mashariki wamejitokeza tena na kutamka kwamba, lile Azimio la Arusha ni adui mkubwa wa ushirikiano uliopo kati ya nchi zetu tatu. Katika ripoti ya mwaka wa Shirika liitwalo Association of East African Industries iliyotolewa hivi karibuni ilidaiwa kwamba Azimio la Arusha limekuwa ni pigo kubwa na la mwisho litakalovunja kabisa ushirikiano wa wa nchi tatu za Afrika Mashariki. Eti ssa hakuna matumaini tena ya nchi hizi tatu kuweza kuungana.
Matamshi haya yalishambuliwa vikali sana na baadhi ya viongozi wetu. Mara tu baada ya makabaila hawa kutoa taarifa yao, Bwana Mwai Kibaki, Waziri wa Kenya wa Biashara na Viwanda alilaani vikali sana ripoti hiyo na kusema kwamba watu wa Afrika ya Mashariki wao ndio wenye mamlaka ya kuamua wenyewe katika mambo yetu yanayohusu na wala siyo watu wengine.
Waziri wa Fedha wa Tanzania, Bwana Jamal, mwishoni mwa wiki hii, saa chache kabla ya kuruka kwenda Cairo kama mmoja wa wajumbe wanaoongozana na Mwalimu katika kutembelea Cairo, aliishambulia vikali sana ripoti hiyo. Alisema kwamba shirika hilo zaidi linawatumikia mabwana zake walioko nje ya Afrika ya Mashariki na kwamba ripoti yake kuhusu Azimio la Arusha haikuwa lolote isipokuwa kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi za Afrika ya Mashariki.
Sisi tunashangaa kuona makabaila katika Afrika ya Mashariki wakiingilia mambo yasiyowahusu hata kidogo. Tunashangaa kuona watu ambao siyo viongozi wa nchi zetu tatu na wala hatukuwachagua ili watutetee, wanajitokeza na kujifanya kwamba wao ndio manabii wa kuagua Afrika ya Mashariki ama hapana. Ni watu gani hawa hata waingiile mambo ya ndani ya Afrika ya Mashariki? Hawa, walitoka ng'ambo kuja kuchuma. Walileta mirija katika Afrika ya Mashariki na sasa kwa kuwa wameona Tanzania imeikata mirija, wanatafuta vijisababu ili wavuruge vichwa vyetu. WALIPYOTO WABAYA SANA HAWA.
Tanzania ilipotwaa mabenki na makampuni makubwa makubwa ya wafanyabiashara na kuyafanya mali ya taifa, viongozi wetu hawakutamka kwamba Tanzania imekuwa mfano wa kisiwa katika Afrika ya Mashariki. Hata kidogo! Viongozi wetu hawakusema kwamba Azimio la Arusha ni kitisho cha Umoja wa nchi za Afrika ya Mashariki.
Maadui wa Afrika ya Mashariki lazima waelewe kwamba Tanzania iliikata mirija ili kuinua uchumi wa umma. Ilitaka njia zote za uchumi ziwe mikononi mwa umma. Makabaila wa shirika la Association of East African Industries waelewe kwamba kabla hawajaleta mitaji yao katika Afrika ya Mashariki, nchi zetu tatu zilikuwa zikishirikiana katika kila jambo. Ushirikiano huu, hata kama makabaila hawa wakitia maneno yao chumvi yapataje, utaendelea kudumu. Watake wasitake, lakini sisi tunalojua ni kwamba siasa inayoifaa Afrika ya Mashariki pamoja na bara zima la Afrika ni siasa ya Ujamaa.
Matatizo ya Afrika ya Mashariki
yatamalizwa na wananchi wa Afrika ya Mashariki wenyewe na wala siyo makabaila
ambao wako hapa kama wanyonyaji wa kutunyonya sisi wanyonge. Uchungu wa
mwana anayeujua zaidi ni mzazi. Malipyoto na wanyonyaji katika Afrika ya
Mashariki hawana nafasi.
Uhuru Alhamisi, Agosti
14, 1969
RAIS Nyerere alisema jana kwamba mafanikio ya Benki ya Taifa ya Biashara yameshinda dua mbaya za maadui wa Tanzania na yameimarisha mioyo ya wananchi katika juhudi za kupata uhuru wa uchumi.
Akiongea kwenye sherehe ya kufungua tawi la TANU katika Benki ya Taifa ya Biashara katika barabara ya City Drive, Rais alisema kwamba Benki ingeshindwa kufanya kazi yake Azimio lote la Arusha lingevurugika na kuwafurahisha makabaila wanyonyaji.
Aliwasifu wafanya kazi wote wa Benki kwa ushirikiano walioonyesha hasa wakati mabenki ya kigeni yalipotaifishwa mnamo mwezi Februari, 1967. Alisema kwamba kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa ushirikiano Benki imeweza kusimama imara na kuendelea.
Mwalimu alisema kwamba madhumini ya TANU katika kufungua matawi yake katika mashirika mbalimbali na viwanda ni kutilia mkazo jinsi chama kinavyoshughulika sana na uchumi wa nchi na kuwaelimisha wafanyakazi ili wawe wakifanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya taifa wala sio kwa faida zao wenyewe tu.
Alisema kwamba kizingiti kilichopo hasa kinachozuia maendeleo ya haraka sio fedha bali ni ukosefu wa wafanyakazi wenye ujuzi wa kuwemo katika mashirika mbalimbali ya Taifa. "Fedha kila siku zinaweza kupatikana wakati ikiwepo kazi", alisema.
Mwalimu aliwahimiza viongozi wa tawi hilo la TANU kujifunza siasa za chama kwa kusoma vitabu mbalimbali na kuhudhuria semina zinazotayarishwa na Makao Makuu ya Chama. Alisema kwamba ni muhimu kwao kuzijua siasa ili wawe tayari kuzitekeleza. Pia aliwataka wanachama wote kukielewa chama vilivyo kwa kuisoma Katiba yake.
Mapema, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Biashara Bwana Amon Nsekela alisema kwamba vitendo vilivyofanyika katika Benki katika mwaka uliopita vimeonyesha kwamba Benki inatambua mapinduzi yanayofanyika. Alisema kwamba Tanzania imo katika hali ambayo inahitaji kufikiri na kuchukua hatua kwa ajili ya ustawi wa uchumi wa taifa zima.
"Mapinduzi yaliyodhihirishwa na hatua zilizochukuliwa Februari 1967 yalikuwa ni ya lazima na ya maana ambayo tulikuwa hatuna budi kuyaanza ili kupambana na hali ya baada ya mapinduzi", alisema.
Bwana Nsekela mwishowe alimkabidhi
Rais shilingi 1,888/25 kuwa mchango wa wafanyakazi wa Benki wa Dar es Salaam
kusaidia chama cha watoto yatima, na vitabu vitatu.
AKIWA amevaa vazi jekundu la Sheria, Mheshimiwa Julius Nyerere, Rais wa TANU alishangiliwa na umati wa watu alipopokea shahada ya digrii ya Doctor of Laws katika Chuo Kikuu cha Edinburgh Scotland, tarehe 5 Julai. Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho ndiye aliyemvika Mheshimiwa kofia ya heshima ya cheo hicho.
Mkuu wa Chuo hicho alimsifu Mheshimiwa katika hotuba akisema kuwa Bwana Nyerere alipokuwa mwanafunzi katika chuo hicho miaka 10 iliyopita, alikuwa na akili pekee, na alianza kujishughulisha na siasa akingali katika Chuo hicho. Bwana C.K. Tumbo, Balozi wa Tanganyika katika Uingereza, na Bwana Mwambenja walihudhuria sherehe hiyo.
Mheshimiwa alikuwa ameruka kwa ndege tokaTanganyika tarehe 1 Julai kwenda Scotland,akarudi Tanganyika tarehe 7 Julai kusherehekea siku ya Saba Saba.
Ingawa aliendea shughuli
ya kupewa digrii lakini alipofika Scotland waandishi wa habari walimzunguka
kumwuliza kama atagombea uchaguzi kuwa Rais wa Tanganyika itakapokuwa Jamhuri.
Akawajibu akisema mtu wa kugombea uchaguzi lazima ateuliwe na chama cha
TANU.
--
|
|