CHAKULA NA LISHE
 
 
Mkapa kawasahau waliokufa kwa njaa
 

Na Mjahid Mwinyimvua
 

JUMAMOSI ya Mei 1, mwaka huu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, alilihutubia taifa kwa njia ya redio. Hutuba hiyo aliitoa akiwa katika uwanja wa Jamhuri, Mjini Morogoro katika sherehe za sikukuu ya Wafanyakazi (May Day).

Katika hutuba hiyo, Mheshimiwa Rais alikuwa anamalizia kila hoja aliyoiona ina nguvu zaidi kwa kibwagizo cha "ukweli na uwazi".

Kumbukumbu zangu hazionyeshi kama Mheshimiwa Rais Mkapa alishawahi kulihutubia taifa na kutumia neno hilo (ukweli na uwazi) mara nyingi zaidi kama vile alivyofanya kwenye sherehe hizo za Mei Mosi wiki iliyopita.

Rais Mkapa akiwa kama mtaalamu wa mawasiliano kwa umma (Mass Communication), alipoyatumia maneno hayo (ukweli na uwazi) mara kwa mara alilenga kujenga fikra katika bongo za Watanzania kuwa serikali yake ni ya ukweli na uwazi mtupu. Yaani haiwafichi kitu raia wake.

Hata hivyo, kwa kila aliyeisikiliza (au atakayeisikiliza) kwa makini na mawazo huru, aligundua (atagundua) kasoro kadhaa zinazoonyesha pengo lililopo baina ya maneno ya Mh. Rais na hali halisi. Kwa mnasaba wa makala hii ya chakula la lishe, nitazungumzia kitendo cha Mheshimiwa Rais kuwasahau Watanzania wanyonge waliokufa kwa njaa 1998/99.

Katika sherehe hizo za Mei Mosi, Rais Mkapa pia aligusia baa la njaa lililoikumba nchi na namna serikali yake ya 'ukweli na uwazi' ilivyojitahidi kulishughulikia. Ni kweli serikali imejitahidi kadiri inavyoweza kulitatua tatizo hilo la upungufu wa chakula. Tunaipongeza kwa hilo.

Lakini, ni ukweli pia kuwa roho kadhaa za wananchi wa Tanzania wapiga kura zimepotea kutokana na baa hilo la njaa. Hapa napo tulimtegemea Mheshimiwa Rais kulizungumzia hili tena kisayansi. Yaani atutajie sehemu gani ya nchi na watu wangapi waliokufa na ilikuwaje kuwaje serikali ya wachapakazi na watu makini ikawa haikuchukua hatua muafaka hadi watu wakafa.

Huu nao ni ukweli na uwazi ambao hatujui kwa nini Rais Mkapa hakutujulisha. Au tuseme ameliweka hilo mpaka kwenye sherehe ya wakulima, nanenane?

Lakini mawazo yaliyo huru hayakubali, kwa sababu Rais alizungumzia baa la njaa, na ili mazungumzo yake yawe kamili, tena ya kisayansi (kwa vile Rais anapenda mambo ya kisayansi) na yawe ya ukweli na uwazi, alilazimika kutaja madhara ya baa la njaa. Moja ya madhara hayo ni kupotea kwa roho za Watanzania ambao ni viumbe wa Mwenyezi Mungu, nguvu kazi ya taifa na pia wapiga kura wenzetu.

Takwimu za waliokufa kwa njaa ni muhimu sana kutolewa hadharani tena siku ile na kiongozi wa ngazi ya juu kabisa katika nchi kiongozi aliyewekwa madarakani kwa kura za wananchi ambao baadhi yao ndio hao waliokufa kwa njaa. Hii ni kwa sababu, vyombo vya habari vimejitahidi sana kuweka mambo wazi.

Kwa mfano, wapi kuna upungufu wa chakula na wangapi wameshaathirika kwa kufa n.k. Lakini taarifa hizo ambazo nyingine zilikuwa na majina ya vijiji, waliokufa na wale waliohudhuria mazishi, zilikanushwa vikali na watendaji a serikali hasa katika ngazi za mikoa na wilaya.

Kuna viongozi kule Dodoma waliosema kuwa wananchi hawakufa kwa njaa bali utapiamlo (malnutrition!) Viongozi kama hawa hivi kweli wanajua maana ya utampiamlo?

Kwa faida ya wasomaji na viongozi wa sampuli ya hapo juu nitaeleza kwa kifupi neno utampiamlo.

Utampiamlo ni hali katika mwili inayotokana na ima wingi au upungufu wa virutubisho kwa maneno mepesi, kama mtu anakula chakula kingi (over feeding) anaweza kupata utapiamlo, na pia yule anayekula chakula kidogo (underfeeding) anaweza kupata utapiamlo. Mlo usiokuwa na virutubisho muhimu pia unaweza kuleta utapiamlo.

Unapozitazama nchi maskini kama vile Tanzania, utapiamlo uliokithiri ni ule wa upungufu wa chakula. Upungufu wa chakula ndiyo hii inayoitwa njaa. Sasa viongozi wetu wanaposema watu hawakufa kwa njaa bali utapiamlo, hivi wanajielewa? Taifa litaingiaje karne ya sayansi na teknolojia na viongozi kama hawa!

Rais Mkapa siyo hakuwa muwazi (hakutoa takwimu) kwa wale waliokufa kwa njaa bali pia hakutoa japo salamu za pole (rambi rambi) kwa wafiwa na Watanzania wengine kwa ujumla.

Hapa ndipo ninaposema, "Rais Mkapa kawasahau waliokufa kwa njaa".

Kwa kumalizia makala hii napenda wananchi wakumbuke kuwa, baa la njaa la mwaka jana na mwaka huu katika nchi yetu limeleta madhara makubwa ambayo siyo tu yamepoteza roho za ndugu na wapendwa wetu, bali pia yameleta mambo ya aibu na fedheha kwa nchi huru kama Tanzania.

Kwa mfano, hivi karibuni gazeti la Alasiri limeripoti hali ya kutisha inayowakabili wananchi katika tarafa mbili zilizoko katika wilaya ya Kilosa, mkoa wa Morogoro. Kwa kifupi, gazeti hilo la Aprili 30, mwaka huu limeripoti kuwa, wananchi wanakabiliwa na njaa, na kutokana na umasikini wanalazimika kwenda kwa matajiri kukopa kiasi fulani cha pesa ili wakanunue chakula.

Bila kipingamizi tajiri hutoa pesa kwa masharti ya kuandikiana mkataba, ambao masharti yake ni pamoja na kumweka kama poni mwanae ili baadaye utakapopata pesa unalipa lile deni na kumchukua bintio (mwanao) na kurudi naye nyumbani.

"Unapewa pesa kuondoka, huku nyuma yule tajiri hulazimisha kufanya mapenzi na bintiyo akidai kuwa hilo ndilo lilikuwa sharti kuu katika mkataba mliongia naye".

Alasiri linaendelea kusema kuwa: Watoto wa kike hugeuzwa chombo cha kujifurahishia na wale wa kiume wanatumikishwa mashambani kama watumwa. Kadhalika ndoa nyingi zimevunjika ama kwa akina baba kukimbia nyumbani na kwenda kutafuta chakula mjini au akina mama kukimbia tabu.

Hii ndiyo Tanzania ambayo serikali yake ya awamu ya tatu inajigamba kukusanya kodi kikamilifu.
 --

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook