MASHAIRI
 
 
Tukio la Mwembechai
 
Tukio la Mwembechai, hivi mwalifikirije?
Kuanzisha vurumai, polisi huwa ikoje?
Watu kuporwa uhai, hilo mwalitazamaje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Mkapa jibu madai, utawala wako vije?
Waleta kizaizai, kuuwa watu iweje?
Twasema hatunyamai, ovu tutanyamazaje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Na Dokta Omari, Makamu unawazaje?
Na Fredrick Sumai, na Makamba mwasemaje?
Na Ali Ameir ai, mwaajabisha mkoje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Mahita haushangai, na Gewe mhadhanije?
Makiwa na Jitimai, umma mtaupozaje?
Haki hatengemai, hivi mnadhulumuje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Muislamu hakai, kwa raha mnatakaje?
Auawa bila rai, na muuaji yuwaje?
Hafunguliwi jinai, hivi kukosa kukoje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Wauaji walaghai, hivi mnawaachaje?
Asie stihizai, "PONDA" mwamtafutaje?
Watu hamtuhadai, sisi tuwachaguweje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Utawala haufai, leo tutaupendaje?
Vipi hatuukatai, kura zetu tuwapeje?
Nyinyi mmetukinai, sisi tuwachaguweje?
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
Tama hatuwatumai, hata vipi msemeje,
Mwakani hatuzubai, kura zetu msingoje,
CCM baibai, humpati mtu aje,
Hivi mwalifikirije, tukio la Mwembechai?
 
"Ni Mkonikoni wa Washairi"
Abdallah Ahmed Seif (Ngome Imara),
S.L.P. 1786 - Mtaa wa Airport,
Dodoma - Kanda ya Kati.

Mashairi yaso vina
 
1. Shairi lahitajika, kwa vina hata mizani,
Ndipo litkamilika, likawa lenye thamani,
Msomaji huridhika, hurudia mara ten,
Mashairi yaso vina, hupungua ladha yake.
 
2. Mashairi yaso vina, hayatamu mdomoni,
Pindi utapoliona, moyo haulitamani,
Shauku hua hauna, nisemavyo si utani,
Mashairi yaso vina, hupungua raha yake.
 
3. ubeti usio vina, huu sasa usomeni,
Ili mpate hakika, vina viko mbali mbali,
Havikupangika sawa, jaribuni kukariri,
Mashairi yaso vina, hupungua ladha yake.
 
4. Imekua tofauti, katikati na mwishoni,
Tizameni madhubiti, kasoro iliyondani,
Mtaona halifiti, zimekuwa tunguo duni,
Mashairi yaso vina, hupungua ladha yake.
 
5. Msitari wa awali, utakapoishia (Ni)
Ufatie na wa pili, kama ule wa Mwanzoni,
Wa tatu pia dalili, umalizie mwishoni,
Mashairi yaso vina, hupungua raha yake.
 
6. Usifate -U-AU-A, fata na herufi zake,
Ndipo zuri litakua, huzidia raha yake,
Mizani muhimu pia, hilo nalo ukumbuke,
Mashairi yaso vina, hupungua ladha yake.
 
Suleiman Khamis,
P.O. Box 571,
Arusha.

Baraka nawatakia kidato cha sita
 
Bismillah Rabuka, kalamu nashikilia,
Kuondoa na kuweka, ni kazi yake Jalia,
Mola ulie tutuka, katika hi dunia.
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Ndugu zangu Islamu, heri hii pokeeni,
Haya naomba fahamu, enyi mlo masomoni,
Kweli hili jambo tamu, heri kuwatakieni,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Dua ninawaombea, awaongoze Manani,
Na njia zenye udhia, Rabi akuepusheni,
Mpate kukaza nia, mmalize mitihani,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Mfanye kwa ufanisi, muupate ufumbuzi,
Ugumu msiuhisi, awaongoze Mwenyezi,
Ondoeni wasiwasi, Mola awe tegemezi,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Islamu Usagara, na wote walo Jangwani,
Najua mpo vinara, Tambaza na Kinondoni,
Tumeziona ishara, Zanaki nimebaini,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Wa Ubungo pokeeni, na Jitegemee pia,
Heri kuu wote nchini, Islamu nazitoa,
Hidaya hii tunzeni, tupate kujikwamua,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Bali ndugu nawasihi, jihadi mpiganie,
Elimu mmeiwahi, heshima msichezee,
Maisha mkayaishi, dini mkashikilia,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Vijana twategemewa, maadili simamia,
Motoni tutendwa tuwa, uovu kutokemea,
Bali tutafanikiwa, tukizitii sharia,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Ndugu mkatawanyike, mijini na vijijini,
Maadili myashike, dini kaitangazeni,
Maovu mkaepuke, Ibilisi mtengeni,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Nimefika ukingoni, kalamu naweka chini,
Nasaha zangu shikeni, enyi mlio makini,
Tufuate Qur'an, ili tufike peponi,
Baraka nawatakia, kwenye yenu mitihani.
 
Fatma Mkombozi,
Arusha.

Kurudia kosa ni kosa kubwa
 
Ndugu zangu kumbukeni, tisini na tano mwaka,
Mlijitia makosani, sitosahau haraka,
Mkapa mchagueni, kwa sauti mlimaka,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Kufanya kosa si kosa, kosa ni kulirudia,
Ulitufika mkasa, wajibu kujikosoa,
Marekebisho yapasa, uchaguzi kufikia,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Yale ya tisini na tano, yasipatupate mwakani,
Tujenge mshikamano, tuwashinde mafatani,
Matamu yao maneno, tuyatoe maanani,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Injiani elfu mbili, mjihadhari jamani,
Mapesa na kandamili, wenyewe waachieni,
Si kwa matusi na kejeli, ila tu vikataeni,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Isilamu watukufu, Mola ametutukuza,
Kuongozwa maradufu, Rabbi ametukataza,
Rahmani ni Raufu, iwapo tukiteleza,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Ni nzuri zao sera, wafanyapo kampeni,
Ni mbaya zao dhamira, walizonazo nyoyoni,
Mkiwapa zenu kura, msijejuta mbeleni,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Dhulma unyanyasaji, wakiwa madarakani,
Watokee wasemaji, huambiwa ni udini,
yatafanywa mauaji, au watawekwa ndani,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Ukapa umeingia, ni nyimbo kwa kila kona,
Yafaa kuuondoa, tufanye kila namna,
Uongozi kuchukua, hiyo ni yetu dhamana,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Yarabbi tunakuomba, utuondolee kiza,
Mabaya yakitukumba, ni vema kutuongoza,
Isitupate kasumba, diniyo kuiburuza,
Tukuogope Muumba, sheria kutekeleza,
Kufanya kosa si kosa, kosa kurudia kosa.
 
Zuhura Uwesu Mashaka,
Dar es Salaam.
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook