Katika somo letu lililopita tuliona maana ya dola, tukaangalia vyombo vyake na tukagusia utendaji wa kitengo au idara iliyokuwepo kabla ya mfumo wa demokrasia na uwazi. Kwa kuhitimisha tuliona kuwa kitengo hicho kilijishughulisha na maeneo makuu matano ambayo tuliyataja kuwa ni:
(1) Kupeleleza na kupeleka habari zilizo dhidi ya "system" iliyopo sambamba na kupendekeza au kuishauri serikali hatua za kuchukua.
(2) Kukusanya habari na taarifa muhimu kwa ajili ya Serikali.
3). Kuingilia kati shughuli za idara au mashirika mengine ya upelelezi na ujasusi.
4). Kueneza na kushinikiza sera na matakwa ya watawala kwa njia mbalimbali za siri zikiwemo vitisho (intimidation), upotoshaji wa habari (misinformation), udhibiti wa habari, urubunifu, kufitinisha na kufarakanisha wapinzani, kuendesha propaganda na kuwaua kisiasa wapinzani(character assassination), kupenyeza au kuwatumia watendaji (double agents) ndani ya makundi ya watu, taasisi, jumuiya n. k. (kwa urefu tusome kitabu kiitwacho The Faber book of Espionage by Nigel West).
(5). Kuchambua na kutathmini habari na matukio yaliyokusanywa.
Chombo chengine cha dola ya kisekula ni Bunge. Kazi za bunge ni kutunga sheria na kudhibiti mwenendo wa serikali. Hata hivyo katika mfumo wa serikali iliyo chini ya Rais (Presidential form of government) Sheria zinazopitishwa na Bunge haziwi sheria bila ya kupata idhini ya kukubali ya Rais.
Chombo cha mwisho ni Mahakama. Jukumu la Mahakama katika mfumo wa kisekula linaelezwa kuwa ni kufafanua utekelezaji wa Sheria na kuonyesha namna ya uwajibikaji na kuadhibu pale inapobidi. Kwa hiyo mahakama huelekzwa kuwa ndiyo yenye kutoa au kusimamia utoaji wa haki.
Vyombo vya kijasusi
Mataifa makubwa ya kisekula, mbali ya vitengo vya ndani vya upelelezi huwa na mashirika ya kijasusi yanayofanya ujasusi nchi nyingine kwa manufaa ya mataifa hayo (Taz.British Intelligence and Covert Action Africa, Middle East and Europe since 1945 by Jonathan Bloch & Patrick Fitzegerald na Intelligence, Espionage, Counter espionage and Covert Operations: A Guide to Information sources Gale Research Company, Detroit, 1978, by Blackstock, P. Schaf R.L.)
Hata hivyo karibu Mataifa yote yamekuwa na vitengo vya usalama (security) na ujasusi (A Dictionary of Modern Politics: A Guide to the complex ideology and terminology which surrounds the world of politics, by David Robertson, 1993 uk.239).
Nchi za Marekani na Israil ni maarufu katika shughuli hii ya ujasusi. Taifa la marekani, kwa mfano, mbali ya shirika lake la ndani la upelelezi FBI (Federal Bureau Investigation) pia ina mashirika mengine kama CIA (Central Intelligence Agency), NSA (National Security Agency) na DIA (Defence Intelligence Agency).
Taifa la Israel lina mashirika mawili makubwa, shirika la Shin-Bet likijushughulisha na upelelezi wa ndani ya Israel na shirika la Mossad nje ya Israel.
Uingereza ina vitengo vikuu viwili. Kitengo cha uslama (M15) ambacho hushirikiana na idara maalum ya polisi chini ya ofisi ya Waziri Mkuu vikiwajibika na usalama wa ndani. Pia kuna shirika la kijasusi la Secret Intelligence Service (SIS) au M16, hili liko chini ya Wizara ya mambo ya nje. Secret Intelligence Service (SIS) hufanya ujasusi nje ya Uingereza kwa maslahi ya Nchi hiyo.
Ufaransa nayo ina shirika liitwalo Service Documentation Exterieure Contre Espionage (SDECE). Na Ujerumani ina kitengo kama hicho kiitwacho Bundes Nachristen Dienst (BND).
Ili kupata picha ya jumla ya namna mashirika ya kijasusi yanavyofanya kazi zake, tungeangalia kwa ufupi mashirika ya kijasusi ya Taifa la Marekani.
Shirika la FBI lilianzishwa mwaka 1909. Mwaka 1934 lilipewa mamlaka ya kuendesha ghughuli zake kitaifa. Kuanzia mwaka 1939 FBI hujishughulisha na utafutaji wa habari ndani ya Amerika na inapotokea dharura nje ya Amerika na pia kujihami. FBI huwasaka majasusi wote wa kigeni wanaoendesha shughuli zao ndani ya Amerika. Na ili kupanua shughuli za ujasusi kuweza kulinda maslahi ya Marekani sambamba na kuendesha vita ya hivi sasa dhidi ya unaosemekana kuwa ni ugaidi (terrorism) wa kimataifa, FBI inaendesha shughuli zake katika nchi kadhaa Duniani. (suala la ugaidi tutaliangalia kwa ufupi baada ya kumaliza kujadili mfumo wa dola ya kiislamu na uendeshaji wake).
Shirika la CIA lilianzishwa mwaka 1947. Muswada wa kuanzishwa shirika hilo ulitolewa mwaka 1944 na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Harry Truman. muswada huo umeigawa CIA katika kurugenzi kadhaa(Taz.The Shadow warriors OSS and the origins of the C.I.A. by Bradley F. Smith). Kurugenzi ya uendeshaji (Operation) inayojihusisha na ukusanyaji wa habari kutoka nchi za nje, na pia kuyalinda maslahi ya Marekani (Counter Intelligence). Kurugenzi ya ujasusi, hujihusisha na uchambuzi wa habari toka sehemu mbali mbali na huzitoa katika taarifa zake. Kurugenzi ya uendeshaji inayojishughulisha na usalama pamoja na ajira. Kurugenzi ya sayansi na teknolojia hujihusisha na mawasiliano, yakiwemo ya simu (Signals) ya ufuatiliaji wa mazungumzo na habari zote zinazopita kwenye mitandao ya simu na kompyuta. Pia inajihusisha kuchambua na kutafsiri picha (National Photographic Interpretation center). Pia ipo ofisi ya kusikiliza matangazo ya redio za nje (Foreign Broadcast Information Service). n.k.
Shirika la NSA (National Security Agency), lilianzishwa mwaka 1952 na linajihusisha na kuhami habari zinazokusanywa na taasisi mbali mbali za kijasusi, kukusanya mawasiliano ya simu za nje na kubuni mafunzo na maneno ambayo hutumiwa na mashirika na idara za kijasusi na usalama kwa kutuma taarifa za siri. Sambamba na kazi hiyo NSA hujaribu kuvuruga maneno ya mashirika mengine ya kijasusi.
--
|
|