JIFUNZE SHERIA
 
Uendeshaji wa Mashitaka - 3
 
 
Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 
Hati ya Mashitaka

UTARATIBU wa kuorodhesha makosa mbalimbali kwenye Hati ya Mashitaka moja unaonekana mpana kiasi cha kutoa uhuru mkubwa kwa mtayarishaji Hati ya Mashitaka kuliko vile (kama tutakavyoona baadaye kidogo) anavyoweza kufanya kwa makosa yale tu yanayofanana au aina moja. Mfano iwapo mtuhumiwa amevunja nyumba kwa nia ya kuiba, akafanya hivyo, kisha akambaka mwanamke mwenye nyumba, anaweza kushitakiwa kwa makosa hayo mawili katika Hati ya Mashitaka moja. Huko India hupendelea makosa kama hayo kushitakiwa mbalimbali. (F.220, kanuni ya Mwenendo wa Jinai ya India, 1973).

Tukirejea kwenye sharti la pili tukuchue mfano mwepesi: mtuhumiwa, karani wa mahesabu katika Wizara ya Fedha Tanzania, bila idhini anaandika hundi ya shilingi 100,000/= akiiga saini za wenye mamlaka ya kutia saini hundi hiyo, halafu anaiwasilisha benki na kujichukulia fedha hizo baada ya juma moja tangu aiandike hundi yenyewe. Ilivyo ni kuwa ile tarehe ambapo mtuhumiwa aliigiza saini za wahusika alikuwa ameghushi maandishi. Hata kama asingeweza kuiwasilisha hundi hiyo benki kosa hilo lingekuwa kamili. Na tarehe ambayo aliipeleka hundi hiyo benki, hata kabla ya kupokea fedha zenyewe, atakuwa ametenda kosa la kueneza au kuitumia hati ambayo imeghushiwa. (F.322, Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16. Sheria za Tanzania).

Anapofanikiwa kulipwa fedha zenyewe atakuwa amekamilisha makosa ya kujipatia mali kwa njia ya udanganyifu (F.302, Kanuni ya Adhabu. i.h.j) pamoja na kukamilisha wizi wa fedha za serikali ya Tanzania. (F. 265, Kanuni ya Adhabu, i.h.j).

Hivyo kwa kutumia hundi hiyo hiyo moja, ingawa kwa tarehe mbalimbali, mtuhumiwa anastahili kushitakiwa kwa makosa yote hayo katika Hati ya Mashitaka moja. Makosa hayo yote sio ya aina moja lakini yanafanana na vile vile ni sehemu ya mfululizo wa makosa yenyewe. Lazima kuwe na mfululizo wa makosa yanayodaiwa kuwa yametendwa na mshitakiwa. Ikiwa kuna vitendo mbalimbali kama ilivyo katika mfano tulioujadili hapo juu, ili vitendo hivyo viweze kuorodheshwa kama mashitaka yaani makosa mbalimbali katika Hati ya Mashitaka hiyo, lazima iwe wazi kwamba wakati kitendo cha kwanza kilichofanyika vitendo vilivyofuatia vilikuwa vinatazamiwa au ni budi vingetokea. Suala hili lilijadiliwa vizuri na Jaji Newbold katika Akber Rashid Nathani v. R., (1965 E.A. 777) aliposema haikuwa sahihi kumshitaki mrufani kwa makosa ya wizi na kutoa rushwa katika Hati ya Mashtaka moja kwa vile vitendo vya makosa hayo havikuwa kwenye mfululizo mmoja.

Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki yamesisitiza kuwa ingawa sio kinyume cha sheria kumshitaki kwa makosa makubwa mawili kwenye Hati ya Mashitaka moja, ni vizuri mashitaka hayo yatenganishwe ili kumpa nafasi nzuri mshitakiwa kujitetea katika mashauri yatakayosikilizwa tarehe mbalimbali. (Yowana Sebukiza 1965 E.A. 684).

Katika kesi ya R. v. Agnes Doris Liundi (1980 L.R.T. n.107) mshitakiwa alishtakiwa kwa makosa matatu ya mauaji ya kukusudia ya watoto watatu kwenye Taarifa ya Mashitaka moja na kupatikana na hatia dhidi ya makosa yote hayo. Mauaji yenyewe yalifanyika katika mfululizo mmoja.

Ikiwa Hati ya Taarifa ya Mashitaka inahusu zaidi ya kosa moja basi kila kosa hilo litawekwa kwenye shitaka la pekee. Mashitaka ya makosa hayo yataorodheshwa ili kurahisisha marejeo ya lazima wakati wa kuendesha mashitaka na kuandika hukumu. Alimuradi masharti yaliyozungumziwa hayakiukwi. Kuyatenganisha makosa hayo kwa kufungua Hati au Taarifa za Mashitaka nyingi kunaweza kusaidia uendeshaji mashitaka uwe rahisi zaidi kuhusiana na vielelezo na hata pengine idadi ya mashahidi. Tatizo ni kuwa baadaye upande wa mashitaka unaweza usiruhusiwe kufungua mashitaka kukamilisha makosa yaliyobakia kutokana na vitendo na ushahidi ule ule. Kufanya hivyo huwa sawa na kumsumbua mshitakiwa au kumsababisha kupewa adhabu za makosa yanayotokana na vitendo vile vile. Itaonekana baadaye kuwa adhabu za makosa yanayotokana na kitendo au vitendo vya aina moja hutolewa kufuatana na kila kosa au uzito wake lakini hutumikiwa kwa pamoja isipokuwa tu kama mazingira ya shauri lenyewe yanahitaji adhabu hizo zitumikiwe moja baada ya nyingine. ( R. v. Sawedi Mukasa 13 E.A.C.A. 97. Pia angalia Kamuhanda v. R. (1971) H.C.E. n.45)

Kama sheria inaonyesha kuwa kosa litatendeka kwa kutenda au kutotenda moja au zaidi ya moja ya vitendo vinavyotajwa itakuwa sio sahihi kumshitaki mshitakiwa kwa vitendo hivyo chini ya kosa moja. Kila kitendo kinachofanya kosa moja budi kiwekwe chini ya shitaka la pekee. Katika Cherere Gukuli v. R., (1955 E.A.C.A. 478. Pia angalia 1955 E.A. 478) mrufani alishitakiwa na kutiwa hatiani wakati wa MAU MAU kwa kula au kuwepo wakati wa kula kiapo cha MAU MAU, akahukumiwa kifo. Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki yalibatilisha hukumu ya Mahakama Kuu ya Kenya kwa sababu Taarifa ya Mashitaka dhidi ya mrufani ilichanganya makosa mawili tofauti katika shitaka moja. Mahakama yalisema kwamba athari hiyo ilimfanya mrufani asiweze kuelewa hasa anashitakiwa kwa kosa gani kati ya yale mawili na kutojua hasa ametiwa hatiani kwa kosa lipi kati ya hayo mawili.

Kuna mifano mingi ya makosa ambayo huweza kufanyika chini ya fungu moja la sheria. Kwa mfano kupokea au kuhifadhi mali ya wizi. (F.311, Kanuni ya Adhabu, i.h.j. Pia angalia R.v. Nassa Ginneries (1955) 22 E.A.C.A 434. Pia (1960) E.A. 338 na Wachira Nyera v. R. (1954 21 E.A.C.A. 398). Njia sahihi ni kuonyesha kuwa kosa la pili, katika shitaka la pili, ni badili ya lile la kwanza. Wakati wa kuendeshwa shauri, kama kawaida, ushahidi wote uliopo kuthibitisha makosa hayo mawili hutolewa. Lakini iwapo mahakama yataona kuwa kosa la kwanza limethibitishwa basi yatamtia hatiani mashitaka kwa kosa hilo tu na kuliacha lile la pili. (R. v. Nassa Ginneries (1955) 22 E.A.C.A. 434. Pia angalia Seffu Bakari v. R., (1960) E.A. 338 na Wachira Nyera v. R (1954)).

Mbali na kuunganisha makosa katika Hati ya Taarifa ya Mashitaka moja washitakiwa wafuatao wanaweza kuunganishwa katika Hati au Taarifa ya Mashitaka moja. Kwanza ni wale washitakiwa ambao wameshitakiwa kwa kosa moja lililotendwa katika kitendo kimoja. (F.134(a),(a), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Aghalabu sharti hili hutumika kuwaunganisha washitakiwa waliotenda kosa kwa nia moja yaani kwa kushirikiana. Hata hivyo sio lazima washitakiwa hao wawe na nia moja ya kutenda kosa lenyewe madhali tu liwe katika mfululizo wa tukio linalohusiana na kosa lenyewe. Mfano: duka linavunjwa usiku wa tarehe 8 Mei, 1994. Thomas anaiba redio kutoka ndani ya duka hilo halafu Bakari anaiba saa kutoka duka hilo hilo. Thomas atashitakiwa kwa wizi wa redio na Bakari kwa wizi wa saa. Kutokana na mfululizo wa utendaji wa makosa usiku huo ushahidi utakaotolewa utaweza kuyagusia makosa mawili ya wizi dhidi ya Thomas na Bakari. Lakini ikiwa kuna ushahidi wa njama ya wizi baina ya washitakiwa hao basi wote watashitakiwa pamoja kwa kosa la wizi wa redio na saa yenyewe. Kwa hiyo kama kila mmoja atashitakiwa pekee kwa wizi wa kitu alichokiiba basi kutakuwa na mashitaka mawili katika Hati ya Mashitaka. Iwapo wote watashitakiwa pamoja kwa wizi wa saa na redio basi kutakuwa na shitaka moja tu.

Aidha, watu ambao wanamsaidia mshitakiwa kutenda kosa wanaweza kushitakiwa naye pamoja kwa kosa lililotendwa. (F.134(1) (b), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Pia watu waliotenda makosa mbalimbali kutokana na kitendo kimoja au mfululizo wake wanaweza kushitakiwa katika Hati ya Mashitaka moja. Katika Nazir Ahmed Ali na Mwenzake v. R., (1962 E.A. 345) warufani walitiwa hatiani kwa makosa matatu ya wizi wa magari tofauti na tarehe mbalimbali. Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki yalikiri kuwa ilikuwa makosa kuwashitaki warufani katika Hati ya Mashitaka moja kwa makosa yaliyotendwa siku mbalimbali. Hata hivyo yalikataa rufani hiyo kwa vile athari yenyewe haikuwanyima haki.

Na katika R. V. Hassan Salehe na Mwenzake (1906-8 E.A.C.A. 105) mahakama yaliiruhusu rufani ya washitakiwa ambao awali walitiwa hatiani kwa makosa mawili ya kubaka ambayo yalifanywa dhidi ya wanawake wawili tofauti wakati mmoja na sehemu moja. Ingawa makosa hayo yalitendwa wakati mmoja yalikuwa hayaungwi na kitendo kimoja. Kila mfufani alimbaka mwanamke wake. Amri ya kusikilizwa upya mashauri hayo ilitolewa.

Hati au Taarifa ya Mashitaka inaweza kubadilishwa au kurekebishwa katika hatua yoyote ile ya usikilizaji wa shauri iwapo mahakama yanaona kuna athari ya mantiki ya kiuandishi. (234(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Kwa mfano mahakama yanaweza yakautaka upande wa mashitaka kuongeza maneno ya lazima kumfanya mshitakiwa aelewe vizuri kosa analoshitakiwa nalo. Au yanaweza kurekebisha fungu la sheria lilingane na shitaka lenyewe. Aidha yanaweza kuamuru kubadilisha shitaka kwa kuweka shitaka ambalo si sahihi kutokana na muhtasari wa shitaka au ushahidi ambao umetolewa hadi wakati huo.

Lakini shitaka haliwezi kubadilishwa au kurekebishwa wakati ambapo pande zote zimekamilisha kutoa ushahidi au wakati wa kuandika hukumu yenyewe. (Jaston Masengula v. R., 1977 L.R.T. n.32). Na kwa vyovyote vile ikiwa shitaka linarekebishwa lazima mshitakiwa apewe fursa ya kusomewa na kujibu shitaka hilo. Aidha apewe nafasi ya kuwaita tena mashahidi wake au wa upande wa mashitaka na kuwahoji tena kadiri anavyopenda kulingana na marekebisho ya shitaka lenyewe. Nafasi hiyo humwezesha kutoa ushahidi ambao utaweza kutoa utetezi, kama upo, dhidi ya kosa lile ambalo limebadilishwa. Katika Jaston Masengula v. R., (K.h.j). Hakimu alibadilisha shitaka wakati wa kuandika hukumu jambo ambalo lilimfanya asiweze kumpa nafasi mshitakiwa kujibu na kutoa utetezi dhidi ya shitaka jipya. Mshitakiwa huyo alitiwa hatiani na kukata rufani ambayo iliruhusiwa na Mahakama Kuu.

Athari nyingi katika Hati au Taarifa za Mashitaka, hasa za kiuandishi, huweza kugunduliwa kwa urahisi mara ya kwanza ambapo mshitakiwa anaitwa kujibu shitaka lake. Kwa mfano shitaka la kuvunja nyumba na kuiba usiku linaweza kuwa na athari mbili. Kwanza maelezo yake yanaweza kuonyesha kosa hilo limetendeka kinyume cha fungu la 265 linalohusiana na wizi wa kawaida. Pili muhtasari wa shitaka hilo unaweza usionyeshe au ukaonyesha kuwa kosa hilo limetendeka mchana badala ya usiku. Athari za aina hiyo zinaweza kurekebishwa mapema ipasavyo kabla mashahidi hawajaanza kutoa ushahidi wao.

Bali wakati mwingine athari hudhihirika wakati ushahidi umekwishaanza kutolewa. Kwa mfano mshitakiwa anakabiliwa na shitaka moja la wizi. Lakini wakati wa ushahidi unapoendelea kutolewa inabainika kuwa mali iliyoibwa ilipatikana baada ya kuvunjwa kwa nyumba. Itabidi mahakama yabadilishe shtaka hilo kulingana na kosa sahihi la kuvunja na kuiba.

Njia nzuri basi kwa mahakama ni kuwa macho na kuzichunguza vyema Hati na Taarifa za Mashitaka kabla shauri kuanza na kuona kuwa ushahidi unaotolewa unahusiana na kosa au makosa yenyewe ili kufanya marekebisho haraka inapobidi.

Waendesha mashitaka nao wanaweza kutoa maombi ya kubadilisha mashitaka wakati wowote ule shauri linaposikilizwa lakini sio kawaida kufanya hivyo baada ya pande zote kumaliza kutoa ushahidi.

Jambo moja linafaa kuongezewa hapa. Kabla ya upande wa mashitaka haujaandika Hati au Taarifa ya Mashitaka na kuiwasilisha rasmi mahakamani ni vizuri wawe na hakika kuwa shitaka lenyewe linalingana na ushahidi uliopo. Kwa mfano karibuni taarifa zote za mauaji huwa ni za mauaji ya kukusudia ambapo aghalabu ushahidi wenyewe unadhihirisha wazi kuwa ni mauaji ya kutokukusudia. Matokeo mshitakiwa hupewa wasiwasi mkubwa mno wa shitaka na kosa zito kama hilo. Pili, kama ilivyoelezwa huko nyuma, hawezi kupewa dhamana kutokana na uzito wa kosa linalodaiwa.

Aidha sio busara na haki kufungua mashitaka mahakamani wakati ambapo ushahidi wenyewe haujapatikana. Kesi nyingi nchini, kwa bahati mbaya, husikilizwa baada ya muda mrefu wa kuahirishwa kutokana na kutokamilika kwa upelelezi. Inafika wakati ambapo uendeshaji mashitaka huonekana kama mchezo. Kwa mfano mwendesha mashitaka huweza kuyaeleza mahakama kuwa upelelezi umekamilika au kuomba tarehe ya shauri inapowadia, kwa mastaajabu makubwa, upande wa mashitaka hudai shauri liahirishwe tena kwa vile upelelezi bado haujakamilika. (R. v. Selemani Jamani and Another, Shauri la Jinai Na. 32, 1982, Mbeya District Court). Hoja kama hii haiingii akilini mwa mtu timamu. Kwa bahati mbaya mahakama hukubali hoja kama hizo japo kwa masikitiko na kuahirisha mashauri. (R. v. Rashid Ahmed, Shauri la Jinai Na. 260, 1989,Ilala District Court). Matokeo kesi moja huweza kuahirishwa zaidi ya miaka miwili kutokana na maombi ya upande wa mashitaka. (R. v. Emmanuel Mwaposya and Another, Shauri la Jinai Na. 687, 1989, Ilala District Court). Jambo hili huleta usumbufu wa kila aina inayoweza kufikiriwa.
 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook