SAYANSI NA TEKNOLOJIA
 
 
MUONGOZO WA KUNUNUA KOMPYUTA (5)
 

Hii ni sehemu ya tano na ya mwisho ya makala hii inayotoa muongozo wa kununua kompyuta. Katika sehemu nne za mwanzo, tumevielezea viungo vyote muhimu zaidi vinavyokuwemo kwenye kompyuta. Katika sehemu hii, tutavielezea viungo vilivyobakia ambavyo ni muhimu kuwemo kwenye kompyuta lakini haviathiri sana ubora wa kompyuta.

CD-ROM Drive

CD-ROM ni ufupisho wa Compact Disc, Read-Only Memory, ambayo ni diski inayotumiwa kutunza data za aina mbali mbali. CD-ROM mara nyingi hukatwa jina na kuitwa CD. CD-ROM drive ni kifaa ambacho kinasaidia kusoma data kutoka kwenye CD (Compact Disc). CD-ROM drive ni muhimu kuwemo kwenye kompyuta hasa kwa siku hizi ambapo programu nyingi zinazouzwa huwekwa kwenye CD. Ukiwa na CD-ROM drive unaweza pia kuchezesha CD za kawaida zenye sauti, kama zile CD za nyimbo ambazo hujuilikana kama audio CD au CD-Audio.

CD-ROM drive, kama jina linavyojieleza, ina uwezo wa kusoma tu (Read-Only), yaani haina uwezo wa kuandika data kwenye CD. Vifaa vinavyoweza kuandika data kwenye CD maalum ni pamoja na CD-R (CD-Recordable) drive na CD-RW (CD-Read and Write) drive.

CD za sauti, zimetengenezwa kupeleka data kwa kasi ya 150 kilobytes per second. Kasi hiyo inatosheleza kabisa kuchezesha nyimbo na muziki wa aina mbali mbali. Lakini kasi hiyo ni ndogo sana kusafirishia data zilizo kwenye CD kwa matumizi ya kompyuta. Na ndio maana CD-ROM drives zinazotumika kwenye kompyuta hufanywa kuwa na uwezo wa kusafirisha data kwa kasi kubwa zaidi ya kasi ya audio CD.

CD-ROM drive inayoambiwa kuwa ina double speed (yaani 2X) inasafirisha data kwa kasi ya 300 kilobytes/s ambayo ni mara mbili ya kasi ya audio CD. Lakini hata hiyo nayo bado ni ndogo, na ndio maana katika miaka ya karibuni zimetengenezwa CD-ROM drives zenye kasi ya 40X (yaani 40 x 150 = 6000 kilobytes/s = 5.86 megabytes/s), au zaidi. Kasi ya 5.86 MB/s nayo pia si kubwa kwani haifikii hata kasi ya basi la data la aina ya ISA (Industry Standard Architecture) ambayo ni 15.9 MB/s. Kasi hiyo ya CD-ROM drive pia ni ndogo sana ukiilinganisha na kasi ya hard disk drives za miaka ya karibuni kama vile za aina ya Ultra DMA-33 ambazo zina kasi ya 33.3 MB/s.

Hata hivyo, kwa matumizi mengi, hakuwi na haja ya kusomwa data mara kwa mara kutoka kwenye CD-ROM drive kwa hivyo kasi yake ndogo haileti athari kubwa. Watu wengi hutumia CD-ROM drive wakati wa kuingiza programu mpya kwenye kompyuta tu na pengine mara chache kwa kuchezeshea CD za muziki. Kwa matumizi hayo, CD-ROM drive yenye kasi inayozidi 24X inatosheleza kabisa. Lakini kama tulivyotangulia kusema hapo juu, siku hizi zipo CD-ROM drives za kasi ya 40X na kuzidi hapo na bei yake si kubwa hata kidogo. Kwa hivyo hakuna hasara yoyote ki-gharama, kompyuta yako kuwa na CD-ROM drive ya kasi kubwa.

CD-ROM drives zipo za aina mbili muhimu kulingana na aina ya kiungo kilichopo baina ya CD-ROM drive na sehemu nyengine za kompyuta. Kuna CD-ROM drives za aina ya IDE/ATAPI (Integrated Drive Electronics / AT Attachment Packet Interface) zinazounganishwa kwenye waya ule ule unaotumiwa kuunganishia hard disk drives, na pia zipo za aina ya SCSI (Small Computer System Interface) zinazotumia kiungo maalum cha kasi kubwa. CD-ROM drives za aina ya IDE/ATAPI ndio maarufu zaidi kwa vile ni rahisi kuunganishwa kwenye kompyuta ingawa hazina kasi kubwa kushinda za aina ya "skazi" (SCSI). CD-ROM drives za aina ya "skazi" ni ghali zaidi.

Watengenezaji maarufu wa CD-ROM drives zilizo imara ni pamoja na Mitsumi, Sony, Panasonic, Creative Labs, na Pioneer. Siku hizi pia vinauzwa vifaa vinavyoitwa DVD (Digital Video Disc) drives ambavyo vinaweza kusoma CD za kawaida na hata CD maalum zenye michezo ya sinema. Mpaka nikiandika makala hii, teknolojia ya DVD bado haijapata umaarufu sana na wala haijakomaa, kwa hivyo ni vyema mtu kuongojea kidogo kama hana haraka.

Kadi ya Sauti

Kadi ya sauti, yaani sound card hushirikiana pamoja na CD-ROM drive kuifanya kompyuta yako kuwa na sifa ya kuitwa "kompyuta ya multimedia" kwa vile inaiwezesha kompyuta kutoa sauti nzuri unapochezesha mafaili yenye data za sauti na picha.

Kwa watumiaji wengi wa kawaida, kadi ya sauti haina lazima kuwa yenye sifa za juu sana. Cha muhimu kujua ni kuwa kadi za sauti hutumia idadi mbali mbali ya bits katika kuwakilisha viwango mbali mbali vya sauti. Kuna kadi za sauti za 16-bit, 32-bit, 64-bit, na hata 128-bit. Kila bits zikiwa nyingi ndivyo kadi ya sauti inavyowezesha kutoa viwango vingi zaidi vya sauti na kuifanya sauti iwe safi zaidi. Kwa matumizi ya kawaida, kadi ya sauti ya 16-bit inatosheleza kabisa, labda uwe unaitumia sana kompyuta yako kuchezeshea data zenye sauti na ukahitaji kuwa na sauti safi zaidi. Ni vyema pia kununua kadi ya sauti ya kuchomekwa kwenye basi la data la aina ya PCI.

Kwa kadi za sauti, Creative Labs ndiyo kampuni maarufu zaidi. Kampuni nyengine maarufu ni pamoja na Yamaha, na Ensonic.

Kadi ya sauti inahitaji spika (speaker). Spika ziko za aina nyingi sana na kwa bahati nzuri bei yake si kubwa hata kidogo. Unaweza kununua spika ya kompyuta ya nguvu ya 100 watts kwa US$10 tu. Cha muhimu ni kuwa na spika inayotosheleza mahitaji yako. Kama mara kwa mara unaitumia kompyuta yako kwa programu zinazotoa sauti basi ni vyema kununua spika nzuri. Pengine utapendelea spika zenye sub-woofer ambazo huwa ni mkusanyiko wa spika kadhaa na ambazo huuzwa kwa bei kubwa kidogo, kama US$40 hivi au kuzidi.

Floppy Disk Drive, Mouse, FaxModem, na Keyboard

Floppy disk drive ni kifaa kinachokusaidia kusoma na kuandika data kwenye disketi. Hiki ni kifaa muhimu kimatumizi lakini namna kinavyotengenezwa ni mara chache kuleta purukushani. Hata hivyo wapo baadhi ya watengenezaji kama Fujitsu ambao nimewahi kusikia watu wakilalamika kuwa floppy disk drives zao si madhubuti. Kampuni ya Panasonic ndio maarufu zaidi kwa kutengeneza floppy disk drives imara.

Floppy disk drives za kawaida zina uwezo wa kusoma disketi zenye uwezo wa kuhifadhi data mpaka za ukubwa wa 1.44 MB, lakini zipo floppy disk drives ambazo zinaweza kusoma na kuandika data kwenye disketi maalum zenye uwezo wa kuhifadhi data mpaka za ukubwa wa 2.88 MB. Sidhani kama kuna umuhimu wowote wa kuwa na floppy disk drives za namna hiyo kwa matumizi ya kawaida.

Mouse ni kifaa muhimu sana kwa watumiaji wa kompyuta na kwa bahati mbaya hakipewi umuhimu unaostahiki. Ni muhimu sana kununua mouse iliyo madhubuti inayoweza kudumu kwa muda mrefu. Mouse zipo za aina nyingi sana lakini kwa ujumla, nunua mouse iliyotengenezwa na Logitech au Microsoft kwani hao ndio wanaotambulika kwa kutengeneza mouse zilizo madhubuti zaidi ingawa ghali kidogo. Si muhimu, lakini inapendelewa kuwa na mouse yenye vifungo vitatu (3-button mouse) ili kuweza kuzifaidi programu (ambazo si nyingi sana) zinazohitaji kuwa na mouse ya vifungo vitatu.

Ukinunua kompyuta mpya sasa hivi hakikisha kuwa ina modem ya kasi ya 56 kilobits/sec (yaani 56K) na inayotumia standard ya V.90. Modem ni kifaa ambacho kinaiunganisha kompyuta moja na kompyuta nyengine hasa wakati wa kuiunganisha kompyuta na Internet. Ni vyema kununua modem ya ndani (internal modem) ya kuchomekwa kwenye basi la data la PCI, kama huihitaji modem hiyo kwa ajili ya kuitumia kwenye kompyuta nyengine. Modem za ndani huuzwa kwa bei ndogo zaidi ya modem za nje (external) ingawa zote zinafanyakazi sawa sawa. Modem ya ndani huondoa udhia wa kuhitajika power adapter inayohitajika kuipatia umeme modem ya nje, na pia waya wa modem (modem cable). Modem ya ndani hupata umeme wake kutoka kwenye kompyuta yenyewe.

Epuka kabisa kununua modems zinazoitwa WinModems ambazo zinauzwa kwa bei rahisi sana lakini si madhubuti hata kidogo hasa kwa vile ufanyaji kazi wake unategemea zaidi programu-mama (operating system) iliyo ndani ya kompyuta. Watengenezaji maarufu wa modems ni US Robotics (ambao karibuni wamenunuliwa na kampuni ya 3COM), Supra, na Motorola. Takriban modems zote zinazotengenezwa siku hizi zina uwezo wa kutuma na kupokea fax na ndio maana zikaitwa FaxModems.

Keyboard nacho ni kifaa muhimu kwa vile kinatumiwa wakati wote. Kwa bahati nzuri, keyboard ni kifaa ambacho hakiharibiki mara kwa mara hata hivyo ni muhimu kunua keyboard iliyo rahisi kuitumia bila ya kuumiza vidole. Watengenezaji maarufu wa keyboards ni Keytronic, na Mitsumi. Kuna keyboard zinazojuilikana kama Win95 keyboards, hizi huwa na vifungo (keys) 104. Vifungo viwili kati ya hivyo vina picha ya Windows, na kimoja kina picha ya menu. Vifungo hivyo ni maalum kwa ajili ya kutumiwa pamoja na Windows 95/98. Kubonyeza vifungo vyenye picha ya Windows, ni sawa na kubonyeza Start, na kubonyeza kifungo chenye picha ya menu ni sawa na kubonyeza kifungo cha kulia cha mouse (right mouse button). Kuna na matumizi mengine kadhaa ya vifungo hivyo kwenye Windows 95/98. Kama kompyuta yako inatumia Windows 95 au Windows 98 basi ni vyema kununua keyboard ya aina ya Win 95.

Case

Case ni sanduku linalofunika kompyuta yako. Kuna mitindo (styles) mitano maarufu ya masanduku hayo. Mitindo hiyo, kwa mpangilio wa kuanzia na kubwa kwendea dogo, ni kama ifuatayo: Full Tower, Mid Tower, Mini Tower, Desktop, na Slimline. Siku hizi pia utasikia kuna kitu wanaita Corporate Tower ambalo ni sanduku la ukubwa wa kati ya Full Tower na Mid Tower.

Masanduku yenye neno "tower" huifanya kompyuta isimame kwa urefu wakati desktop na slimline hifanya kompyuta ilale kwa upana. Kama una nafasi ndogo kwenye meza ya kompyuta, pengine ni bora kununua sanduku la mtindo wa desktop ili monita ikae juu ya hilo sanduku. Lakini pia unaweza kununua sanduku la mtindo wa "tower" na sanduku hilo ukaliweka kwenye mvungu wa meza.

Kila sanduku likiwa kubwa ndiyo vizuri zaidi kwa vile kompyuta inapata upepo kwa wingi zaidi na kuvifanya vifaa visipate joto sana, na pia inakuwa rahisi kuingiza vifaa vipya kwenye kompyuta. Kwenye hali ya hewa ya joto ni muhimu kuwa na angalau sanduku la mtindo wa Mid Tower na ikiwezekana unaweza pia kuweka feni maalum ndani ya sanduku hilo.

Ni muhimu kuhakikisha kuwa sanduku la kompyuta lina nafasi ya kutosha kuweka ndani yake floppy disk drive, CD-ROM drive ya ndani, na hard disk drives nne.

Kitu chengine muhimu kinachokuja kwenye case ya kompyuta ni power supply inayosambaza umeme kwenye vifaa mbali mbali vilivyo ndani ya kompyuta. Power supply ni vyema iwe na nguvu ya 250 watts au zaidi ili iweze kutumika pamoja na vifaa vingi zaidi. Unaponunua kompyuta, hakikisha kuwa power supply ina plagi za kutosha za kupeleka umeme kwenye floppy disk drive, CD-ROM drive ya ndani, na hard disk drives nne.

Programu

Ukinunua kompyuta mpya hivi sasa inapendekezwa iwe na operating system ya Windows 98. Programu nyengine itategemea mahitaji yao lakini programu maarufu ni Microsoft Office 97 ambayo inakupa Word 97 kwa ajili ya kuandikia barua na maandishi mbali mbali, Excel kwa kufanya kazi kwenye mahesabu ya spreadsheet na Access ambayo ni programu ya database.

Utahitaji pia kuwa na programu ya kuilinda kompyuta yako ili isiingie virusi vya kompyuta (computer viruses). Programu ya Norton Anti-Virus ni maarufu kwa kazi hiyo. Pia ni vyema kuwa na programu ya WinZip ili ikusaidie kubana (compress) na kubanua (uncompress) mafaili yanayopatikana kutoka sehemu mbali mbali.

Hitimisho

Kwenye makala hii tumeelezea kwa kina vifaa kadhaa muhimu vinavyokuwemo kwenye kompyuta. Umadhubuti wa kompyuta yako utategemea aina ya vifaa vitakavyokuwemo kwenye kompyuta hiyo. Kwa bahati mbaya, vifaa madhubuti vinauzwa kwa bei kubwa zaidi. Ni muhimu kutafuta kompyuta inayokidhi mahitaji yako bila ya kutoboa mfuko wako. Ni muhimu kujenga tabia ya kudadisi unapokwenda kununua kompyuta kwani kuna baadhi ya wanaouza kompyuta hupenda kubambika vifaa vilivyo dhaifu kwenye kompyuta wanazowauzia wateja wao. Wajinga ndio waliwao. Tunatumai kuwa baada ya kuisoma makala hii, hutakuwa mmoja kati ya wajinga hao.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook