MAANA halisi ya neno Maulid ni uzawa na kwa desturi iliyozoeleka Maulid ni uzawa wa Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.). Je, Waislamu wanapofanya sherehe za Maulid huwa nini azma yao? Mwandishi wetu Haura Shamte anachambua zaidi.
IMEKUWA ni kawaida kwa Waislamu hususan wa pande za Afrika Mashariki kufanya sherehe za Maulid kila wanapojisikia kufanya hivyo.
Husoma Maulid wanapoingia kwenye nyumba mpya, wanapotoka arobaini ya uzazi, wanaporudi kuhiji Makka, wanapotoa watoto jandoni, wanapoowa au kuolewa, wanatopoka eda na kadhalika.
Kwa mantiki hiyo Maulid yanaeleweka kwa Waswahili ni furaha au kujipongeza baada ya kuvuka salama kutokana na jambo fulani la kijamii.
Mtume Muhammad (s.a.w.) alizaliwa tarehe 12 mfungo sita siku ya Jumatatu na katika uhadi wake kila siku ya Jumatatu alikuwa akifunga kwa minajili ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwake nakwa kuwa jambo alilokuwa akilifanya Mtume ni Sunnah inakuwa Sunnah kwa Waislamu kufunga kila siku ya Jumatatu.
Fundisho tunalopata hapo ni kuwa hakuna amali bora atakayokuwa ameifanya mja katika maadhimisho ya uzawa kama funga. Bwana Mtume Muhammad (s.a.w.) hakusoma Maulid kuadhimisha kuzaliwa kwake wala watoto wake wala jambo hilo halijafanywa na yeyote katika masahaba zake. Je, Waislamu hilo tumelipata wapi?
Wakristo hufanya sherehe zao zinazodaiwa za kuzaliwa Yesu (a.s.) mara moja kwa mwaka Desemba 25, lakini ajabu ni kuwa kwa Waislamu hakuna siku maalum yaweza ikawa Jumamosi, Jumapili, Alhamisi, Ijumaa na kadhalika.
Je, Waislamu walishawahi kujiuliza nini maana ya kusoma Maulid? Kama Maulid ni furaha je, kuna umuhimu gani wa kumsimamisha Mtume (s.a.w.) katika furaha hiyo? Si vibaya kwa Muislamu kumtaja Mtume (s.a.w.) kwa wakati wowote ule aupendao, lakini je, kumtaja Mtukufu wa Daraja katika Maulid yenye mtindo wa disko na mchanganyiko holela wa wanaume na wanawake ni ibada? Ni Sunnah au ni jambo gani?
Kama Maulid ni mashairi ya kumsifia Mtume (s.a.w.), Mtume (s.a.w.) mwenyewe hakukataza kusifiwa kusiko pindukia mipaka, lakini je, Maulid ndio mtindo sahihi wa kumsifu Mtume (s.a.w.)? Ni vizuri kama tutabuni mtindo maalum wa kuwafundisha watoto wetu Sira ya Mtume Muhammad (s.a.w.) watakayoielewa na kuitumia, lakini mtindo wa kusoma mashairi ya Maulid kikasuku hauwasaidii kuinua ufahamu wao juu ya mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w.).
Bibi Aishat (r.a.) alipoulizwa juu ya mwenendo wa Mtume (s.a.w.) alisema ni kama Qur’an inayotembea, lakini je kwa kusoma Maulid kikasuku jamii inapata fundisho gani?
Kama maulidi inakusudiwa kukusanya Waislamu na kubadilishana mawazo na kuimarisha umoja wao, basi awla mjumuiko huo ungepangiwa utaratibu mzuri zaidi kungekuwa na mawaidha, majadiliano, mashairi na kadhalika. Na pia mkusanyiko huo ungeitwa jina jingine kwani kusoma Maulid katika kila hafla kunaishushia maana na hadhi maana nzima ya Maulid.
Kutokana na mwenendo huo wa kusoma Maulid kwa wakati wowote, saa yoyote na katika tukio lolote, hivi karibuni Mwalimu Julius Nyerere alikabidhiwa jumba lake la fahari huko Butiama yasemekana kuwa alisoma Maulid kulifungua rasmi.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Rais Mstaafu wa awamu wa pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Rais Mkapa, mawaziri kadhaa na mkuu wa majeshi, Maulid hiyo ndiyo iliyokuwa kivutio kikubwa kutokana na sauti za watoto waliokuwa wakisoma.
Wachunguzi wa mambo walieleza kuwa Mwalmu Nyerere aliyekuwa wakati fulani akivaa kofia ya Kiislamu aliamua kuyasoma Maulid hayo kutokana na itikadi za watu wa Pwani ambao husoma Maulid katika shughuli zao nyingine ikiwemo kufungua nyumba mpya.
Mmoja wa waliohudhuria hafla hiyo alisema kuwa kwa kuwa Mwalimu Nyerere amekaa sana Pwani, marafiki zake wengi walikuwa watu wa Pwani na Masheikh wengi wa Bagamoyo, hivyo utamaduni huo wa kipwani pwani ambao ni wa Kiislamu naye ameukumbatia sana.
Hiyo ni habari iliyotolewa na gazeti moja la wiki No. 32. Hebu tuchunguze maneno itikadi za watu wa Pwani, utamaduni wa Kipwani pwani, je, vifungu hivyo vina uhusiano wowote na Uislamu?
Kutokana na vifungu hivyo vya maneno tunabaini kuwa Maulid ni itikadi ya watu wa pwani na ni utamaduni wa kipwani pwani ambao hauna mnasaba wowote na Uislamu. Hivyo Maulid si Sunnah wala fardhi. Na habari hiyo haikukusudiwa kuusifu Uislamu bali kukashifu, imehusu nini Nyerere na Maulid?
Historia ya Maulid katika Pwani ya Bahari ya Hindi
Waarabu walipoingia katika pwani ya bahari ya hindi waliwakuta wenyeji wake wakiwa wapagani, ingawa wao walikuja kwa ajili ya kufanya biashara pia waliitumia fursa hiyo kueneza dini ya Uislamu.
Mbinu mojawapo waliyoitumia ni kusoma Maulid ambayo ndiyo yaliyokuwa kivutio kikubwa cha watu kuingia katika dini, walisoma mashairi ya kuvutia na kupiga dufu hivyo watu wengi wa pwani ya hindi waliingia katika Uislamu kwa kufuata mvuto wa mashairi yaliyojulikana kama kaswida.
Na jambo hilo si ajabu kutumiwa na Waarabu kwani mashairi ndiyo utamaduni wao wa asili. Walisoma mashairi katika kumsifu mfalme, kumsifu shujaa wa vita na hata katika malumbano baina ya wao kwa wao.
Hakukuwa na ubaya wowote kwa watu kutumia Maulid kama njia ya kueneza dini lakini je katika zama hizi bado Maulid ni nyenzo ya kueneza dini?
Watu hivi sasa wamefunuka mawazo wanataka hoja zilizo wazi kuwashawishi waumini unachokiamini na wafuate unachotaka wakifuate, mashairi na midundo kwao imebaki ni starehe tu, hivyo si busara tena kusambaza hoja nzito za dini kwa kutumia madufu na sauti nyororo za wasichana na vijana wadogo wa kiume na hata zile nzito za mabarobaro ni mbinu ambayo imepitwa na wakati.
Waislamu hivi sasa wanapaswa kuweka Strategia mpya katika kuufikisha ujumbe na kujenga mshikamano.
"Maulidi" yaweza kubadilishwa
badala ya kupiga dufu na sauti nyororo tukayageuza kuwa majukwaa (forum)
ya kisiasa kutangaza sera za Uislamu kwa kupiga vita mifumo ya kidhalimu
na ukandamizaji inayotawala jamii zetu.
|
|