HALI ya Waislamu walio wengi kiuchumi ni ngumu sana. Akinamama hawana ajira wala biashara zenye kuaminika. Mabinti hawana kisomo na wanaotaka kusoma hawana karo wala wa kuwadhamini (sponsors).
Wengi wa watoto wa Kiislamu wameishia kuwa vibaka na changudoa kwa kuporwa haki yao ya elimu na ajira. Hawa wanahitaji kusaidiwa na kukombolewa.
Wajane na watoto yatima ambao waume zao, wazazi na walezi wao wameuliwa pale Mwembechai au kufia gerezani, wanateseka. Hawana chakula wala karo ya shule.
Mtoto Chuki Athumani hata kutambaa hawezi, anahitaji japo kigari cha moto. Tungependa kuona hawa wakiendewa na kupewa misaada. Kuwakusanya akina mama wa wilaya nzima wakiwakilishwa na wenzao wapatao 100 na kuwapa viroba vitano vya unga au mchele tukiwaacha waathirika wa Mwembechai ni kejeli kwa Waislamu.
Kejeli hii haipo mbali sana na ile ya kuwakusanya mabinti wa Kiislamu wakishindana kughani (msabaka) Qur'an huku hakuna mipango yoyote madhubuti ya kuwafanya waijue Qur'an na maisha yao yaongozwe na Qur'an na wajikomboe ili waepukane na uchangudoa, U-Miss Tanzania, U-Maimuna na kuwa wapika chai maofisini kwa mabosi Rita na Marry.
Waislamu na hasa jumuiya za Kiislamu; ni lazima zijue nini shida, agenda na matarajio ya Waislamu. Kwenda kinyume na haya ni kuwasaliti Waislamu.
Wamiliki wa mashule mbalimbali ya sekondari pamoja na waalimu baada ya kuwanoa wanafunzi huwapambanisha katika mtihani wa pamoja iwe kiwilaya au hata mkoa (Mock) ili kupima mafanikio ya kazi zao.
Vipi leo sisi tufurahie kuandaa msabaka wa wanafunzi ambao hatujui wanasoma katika mazingira gani. Hatujui waalimu wao wana mshahara au la, hatujui wana madeski au whukaa chini. Wala hatujui madrasa zao zinavuja au kusoma chini ya miti.
Kwanini tusije na programu za kuanzisha madrasa (shule) au kuziboresha zilizopo kwa kuyakarabati majengo kutoa vifaa na kuwalipa waalimu mishahara.
Tusitegemee kuona watu wanaanzisha jumuiya ili wakaandae msabaka, waanzishe shule na vyuo vyao kisha wawapambanishe wanafunzi wao.
Inakuwa kiroja zaidi Jumuiya au taasisi inapokuwa na hadhi ya kimataifa halafu ikaona shida ya Waislamu wa Tanzania ni kukosa uwezo wa kuendesha msabaka na hivyo ikajitwisha jukumu hilo.
--
|
|