Waliokamatwa Nzega wapewa dhamana
 
 

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya kusota rumande hatimaye waumini 15 waliokamatwa wilayani Nzega miezi miwili iliyopita wamepewa dhamana na mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Tabora.

Waumini hao walikamatwa mjini humo kwa tuhuma za kutoa mahubiri ya kashfa dhidi ya dini nyingine.

Kwa miezi miwili mfululizo waumini hao waliwekwa rumande na dhamana yao kuzuiliwa kwa madai ya kuwa kuwepo kwao nje kungehatarisha hali ya usalama wilayani humo na kutishia maisha ya baadhi ya watu.

Kabla ya kutoa dhamana kwa watuhumiwa hao, Mahakama iliweka sharti kwa kila mmoja kudhaminiwa na watu sita.

Wakizungumza baada ya kuachiwa huru, waumini hao wamesema wafungwa na mahabusu gerezani wanahitaji ujumbe wa Mwenyezi Mungu kuweza kubadili mienendo yao.

Hivyo waliwaomba Waislamu nchini kote wawe na utaratibu wa kutembelea magerezani kufikisha maadili ya Uislamu kwa wafungwa.

Walisema kwa kipindi kifupi walichokaa gerezani walifanikiwa kuwasilimisha wafungwa na mahabusu 26.

"Tumeanzisha mijadala ya neno la Mungu gerezani", amesema mmoja wa waumini hao.

Kesi yao imeahirishwa hadi Juni 9, mwaka huu itakapotajwa tena.


Vijana watakiwa kuuupa haki ujana wao
 

Na Jihadi Sabala, Shinyanga

KATIKA ujumbe uliotolewa hivi karibuni na Amir Mohamed Issa kwenye Mahafali ya TAMSA ya kuwaaga vijana wa Kiislamu wanaomaliza kidato cha sita mkoani hapa mwaka huu umo wito unaowataka vijana wa Kiislamu kuupa ujana haki yake kwa kusukuma mbele kalimah ya La Ilaaha Illa Llaah.

Alisema ujana ndiyo rasilimali ya umma na kwamba umma wowote, hata ule wa makafiri huwategemea vijana katika ulinzi, utetezi na ustawi wa umma wao.

Amir Mohamed alisema kuwa ikiwa Waislamu hawajui umuhimu wa vijana wa ummah wao wawaangalie wasio Waislamu ambao wanalitambua vyema hilo.

Aliyataja baadhi ya makundi hayo ya vijana kama vile iliyokuwa TYL na sasa UV-CCM, SCAUT, YCS, UKWATA, VIWAWA na jumuiya nyingine mbalimbali.

Kutokana na ukweli huo, Amir Mohamed aliwataka vijana wanaomaliza kidato cha sita kuuona umuhimu wa wao kama vijana kushiriki kikamilifu katika harakati za kusimamisha Uislamu popote pale watakapokuwa na kuungana na wenzao katika harakati hizo.

Hata hivyo, alisema kuwa wajibu huu hauwezi kutekelezwa vyema bila ya kuusoma na kuuelewa vyema Uislamu na pia kuyafahamu vyema mazingira wanayokwenda kuishi nayo.

Aliyataja mazingira hayo kuwa ni uadui na chuki ya maadui wa Uislamu kwa Uislamu na Waislamu wenyewe, ujahili (ukafiri) wa asili na ujahili mamboleo (Modernity) pamoja na matatizo ya ndani ya ummah ambamo kuna migawanyiko mbalimbali kama ile ya kundi la wajuzi wa elimu inayoitwa ya "dini" na lile la wajuzi wanaoitwa wa elimu ya "dunia", farka za kiitikadi na kimadhehebu pamoja na tofauti ya taasisi chungu nzima walizonazo.

Akawataka vijana hao kuto kutumika kama chachu ya mgawanyiko huo uliopo bali wawe ni daraja la kuwaunga pamoja pande tofauti kwa maslahi ya ummah wa Kiislamu.

Wakati huo huo, Mwalimu Diamond ambaye ni mlezi wa vijana wa Kiislamu katika shule ya biashara (Shycom) mjini hapa alisema katika nasaha zake kwenye hafla hiyo kuwa mabinti wa Kiislamu waliomo mashuleni ambao bado hawavai hijabu washone vazi hilo kwani hiyo ni amri ya Mola wao na ni kitambulisho cha dini yao tukufu.

Aliwaonya vile vile mabinti wa Kiislamu ambao wamezua tabia ya kuwaazima mavazi yao (hijab) wanafunzi wa kike wasio Waislamu ambao hutoka wamevaa mavazi hayo hadi nje ya shule na huko kuonekana wakifanya maovu mbalimbali, kuwa tabia hiyo ni matusi kwa Uislamu.

Aliita kuwa ni mbinu za maadui wa Uislamu na akasema kuwa huenda wafanyao hivyo wanatumwa na wako kazini kuutukanisha Uislamu.

Aliahidi Mwalimu huyo adhabu kali kwa yeyote atakayebainika anamwazima mwenzie hijaab yake hali anajua kuwa mwenzie si Muislamu.

Mahafali hayo yalifanyika katika ukumbi wa kituo cha kulelea watoto yatima kinachosimamiwa na Mama Ayyam. Kituo kilichopo eneo la viwanda mjini hapa na yaliwajumuisha pamoja na wanafunzi wa shule tatu zenye kidato cha tano na cha sita za Shycom, Buluba na Buhangija.

Walikuwepo pia wanafunzi wa Kiislamu wa Uhuru sekondari yenye kidato cha nne na baadhi ya waalikwa wengine toka katikati ya mji huu.

Idadi ya wahitimu wa shule zote tatu ambao hivi sasa wanafanya mtihani wa kidato cha sita ni 46. Kati ya hao 44 wanatoka Shycom yenye jumla ya wanafunzi 164.


Mihadhara yasilimisha 473 Burundi
 
 

Na Mtaita M.
 

MIHADHARA inayoendeshwa na tawi la AL-MALLID yawavutia maelfu ya wananchi nchini Burundi.

Imearifiwa kuwa tawi la AL-MALLID nchini Burundi limekuwa likiendesha mihadhara katika sehemu mbalimbali nchini humo kwa miaka kadhaa sasa ambapo mada mbalimbali hutolewa.

Kivutio kikubwa katika mihadhara hiyo ni namna wadhahiri wa Kiislamu wanavyolizungumzia suala la ukabila na namna Uislamu unavyolichukulia suala hilo.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi, Katibu Mkuu wa tawi la AL-MALLID nchini Burundi Bw. Siraj Mohamed amesema kuwa watu wa dini mbalimbali wamekuwa wakivutiwa na mihadhara hiyo na kwamba katika mhadhara uliofanyika katika mkoa wa Muyinga mwezi Aprili, mwaka huu watu 200 walirejea katika Uislamu.

Mihadhara ilianza rasmi mwaka 1994 kwa ruhusa ya serikali lakini kutokana na kuzuka kwa mapigano ya kikabila nchini humo ilisimama kwa muda, hadi kufikia mwezi wa Mei mwaka huu inasadikiwa kuwa watu 473 walikwisha rejea katika Uislamu.


Wahitimu kidato cha sita waambiwa hakuna ajira
 

Na Habiba Swedi, Arusha

VIJANA wanaohitimu masomo wametakiwa wawe wabunifu wa kujianzishia miradi isiyohitaji fedha nyingi ili waweze kujiajiri wenyewe badala ya kupoteza muda wao kwa kutafuta ajira.

Wito huo umetolewa na mgeni rasmi, Bwana Agrey Mwanri katika mahafali ya kwanza ya kuwaaga wanafunzi kumi na tano wa kidato cha sita yaliyofanyika katika shule ya sekondari ya Bondeni hivi karibuni.

Bwana Mwanri ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini amesema kuwa kijana atathaminiwa kwamba ana elimu endapo ataitafsiri elimu yake kwa vitendo, akabadili tabia akayajua na kuyatatua matatizo ya jamii yake.

"Tuna tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana, msije hangaika huku na huko kutafuta ajira. Nendeni mkaunde vikundi vidogo vidogo muanzishe miradi inayohitaji nguvu kazi zaidi kuliko pesa kama vile kilimo cha bustani, ususi wa nywele na kadhalika", alisisitiza Bwana Mwanri.

Aidha, aliifananisha elimu waliyoipata vijana hao na sadaka kutoka kwa wazazi, walezi na waalimu kwa ujumla. Hivyo aliwataka vijana kuwa waadilifu kama njia ya kuienzi na kuitoa sadaka hiyo kwa jamii.

"Hii ni shule ya Kiislamu ingawa wanafunzi wote sio wa Kiislamu. Waislamu wana maadili mema ambayo nina uhakika mmeyapata hapa shuleni hivyo nendeni basi mkaishi kwa mujibu wa maadili hayo ya dini", alisisitiza Bwana Mwanri aliyeonekana mchangamfu wakati wote na nasaha zake kufurahiwa.

Katika risala ya kumkaribisha mgeni rasmi iliyosomwa na Sheikh Idi Kateta kwa niaba ya meneja wa shule ya Bondeni ambaye ni Katibu Mkuu wa Bakwata mkoa, Alhaj Mohamed Mollel, ilielezwa historia fupi kwamba shule ilianza rasmi kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano mwaka 1997.

Risala hiyo pia ilitaja baadhi ya matatizo ya shule ikiwa ni pamoja na ukosefu wa viwanja vya michezo, hosteli ya wanafunzi, kompyuta na mashamba ya miradi ya kilimo.

Nao wanafunzi walioagwa walisema katika risala yao kuwa shule ingali changa kitaaluma kwa upande wa 'A Level', hivyo walikumbana na uhaba wa vitabu, vifaa vya maabara na maktaba, matatizo ambayo waliomba yatatuliwe mara moja.

Hata hivyo waliwashukuru waalimu wao kwa kujitolea kiasi kikubwa kuhakikisha matatizo hayo hayawaathiri.

Kutoka kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo yao hapo (kidato cha tano) nasaha zilizotolewa kwamba wamche Mwenyezi Mungu ili wapate mafanikio ya maisha duniani na akhera.


Ulaji wa nguruwe waingizwa Tanga
 

Na Mwandishi Wetu, Tanga
 

KUNA habari zilizozagaa mjini hapa kuwa mtindo wa ulaji nyama ya nguruwe kwa shangwe tayari upo mjini Tanga.

Mtindi huo umekuwa ukisikika kwa muda jijini Dar es Salaam hufanyika hapa kila mwishoni mwa wiki eneo la Majani Mapana jirani na kituo cha kukuzia nguvu za umeme kwenye njia ielekeayo shule ya sekondari ya Galanos.

Mkusanyiko huo ambao huambatana na kuchoma mishikaki na kuchukua kwa ajili ya kitoweo huwavuta hata Waislamu wa jirani na kutoka katikati ya mji.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook