Na Mwandishi Wetu, Arusha
WATOTO saba (7) yatima pamoja na mama yao Bi Zena Saidi wamekuwa katika hali ngumu ya maisha toka baba yao Bw. Dosa Salimu Dosa (48) alipouliwa na polisi mwaka jana.
Bi Zena ameeleza kwamba mume wake alikuwa ndiye nguzo pekee ya maisha yao ni hivyo kuuliwa kwake kumewafanya wakose namna ya kupata chakula na mahitajio mengine muhimu ya maisha.
Amesema hali inayomkabili ni ngumu sana hasa ikizingatiwa kwamba watoto wake bado ni wadogo.
Kutokana na hali hiyo Bi Zena amekuwa akiwasiliana na vyombo vya dola kudai msaada au fidia lakini hakuna ushirikiano wa aina yoyote unaoonekana kutolewa.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi mkoani hapa wiki iliyopita lilimfukuza kazi askari PC Elimboto Elias (28) baada ya kuthibitika kuwa alimuua kizembe Bw. Dossa Salim Dossa baada ya kufyatua risasi akijaribu kumkimbiza mahabusu aliyekuwa anatoroka wakati akipanda karandika la polisi kuelekea mahakamani mwishoni mwa mwaka jana.
Akithibitisha habari hizo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Bwana Juma Ng'wanang'waka alisema askari huyo PC Elimboto mwenye nambari C. 7992 amefukuzwa kazi kutokana na uzembe huo uliopelekea mauaji ya Dossa Salim Dossa aliyekuwa mkazi wa Olmatejo.
Alisema Kamanda huyo kuwa, siku hiyo ya tukio askari Elimboto alipangiwa kazi ya kusindikiza mahabusu watokao katika mahakama ya mwanzo ya Maromboso iliyoko eneo la Kilombero.
Aliendelea kusema kuwa wakati karandinga la polisi linaanza kuondoka, mahabusu Leminganya John, mtuhumiwa wa kosa la kugoma kulipia bia sita alizokunywa, aliruka na kuanza kukimbia, ndipo PC Elimboto alipoanza kumkimbiza huku akifyatua risasi ovyo, mojawapo ikampata marehemu aliyekuwa akipita na safari zake na kufariki papo hapo.
Sambamba na hatua hiyo ya kufukuzwa kazi, Kamanda huyo alisema, Jeshi la Polisi litamfikisha mahakamani askari huyo ili kujibu mashitaka ya mauaji hayo.
Nao Waislamu mbalimbali waliohojiwa juu ya hatua hiyo ya jeshi la polisi, pamoja na kuipongeza, lakini bado walionyesha wasiwasi wao juu ya hatma ya familia ya marehemu Dossa.
Wamesema kuwa tokea mwanzo wa tukio hilo, hadi kutangazwa kwa hatua hiyo dhidi ya muuaji, si polisi mkoa wala polisi binafsi walioonyesha ushirikiano na familia hiyo ya marehemu, jambo ambalo linaonyesha umbali uliopo kati ya raia na chombo chao cha dola chenye dhamana ya kulinda usalama wao.
Aidha, wamesema hali hiyo inaleta wasiwasi wa kesi itakayoendeshwa mahakamani kwamba huenda isiwe ya muafaka kwa mjane ya yatima walioachwa.
Naye mjane wa marehemu Bi Zena Said alikiri kutokuwepo kwa ushirikiano wowote kati ya polisi na yeye hata ile kupewa pole tu ya mdomo.
Anasema Desemba 22, mwaka jana alimwandikia barua mkuu wa polisi mkoa akiomba maelezo ya ofisi hiyo amna itakavyomsaidia kuwalea yatima aliachiwa na marehemu mumewe lakini hajapata jibu lolote.
--
|
|