IFUATAYO ni hotuba iliyotolewa kwa wahitimu Waislamu wa Stashahada ya juu Chuo cha Uongozi wa Maendeleo Mzumbe (IDM) wakati wa mahafali ya kuwaaga iliyofanyika Mei 15, mwaka huu Chuoni hapo.
Ndugu Waislamu nilitaka niwakumbushe kisa kimoja cha sahaba anaitwa Ka'b. Nadhani wengi mnamfahamu. Huyu Bwana alikuwa ni miongoni mwa Sahaba mkubwa kabisa. Na ukiangalia katika Tarekh ya Kiislamu alishiriki karibu katika vita vingi sana.
Lakini kuna vita moja huyu Sahaba pamoja na wenziwe kwa bahati mbaya na kwa sababu tu za kibinaadamu wakawa hawakwenda katika ile vita. Walipomaliza shughuli wanataka kwenda vitani, kwa bahati mbaya kwa upande wao Waislamu wamekwisha rudi.
Kwa hiyo ikawa wao ile vita imewakosa. Badala yake wakaenda kwa Mtume (s.a.w.) wakamkuta yupo Msikitini. Wakamwambia Yaa Rasulullah wewe tunajua ni Mtume wa Mwenyezi Mungu hatuna sababu ya kukuongopea. Tumeshindwa kwenda katika vita kwa sababu tu za kibinaadamu bila ya udhuru wowote wa kisheria.
Basi Mtume (s.a.w.) akasema, nyie nendeni. Na kuanzia leo akapiga marufuku watu wasiwashirikishe wale Mabwana katika hali yoyote. Na kwa kuanzia marufuku kuzungumza nao. Akikupigia salamu hakuna kumuitikia. Na kwa kweli kipindi kile ilichukua kama siku arobaini hivi wale Masahaba ambao hawakwenda vitani walikuwa katika hali ngumu sana.
Fundisho ambalo ningependa tulichukue ni kwamba katika Tarekh ya Kiislamu na ni Sunnah kwa ushahidi huu kwamba kama kuna watu au kikundi cha watu kama hawafuati au wanahujumu harakati (za Waislamu) inafaa watu hawa kuwapiga pande. Akikualika harusini kwake usende, ukifanya shughuli yako usimwalike, maana yake kama hamuwezi kustahiana katika dini zenu, hatuwezi kuheshimiana katika dini, basi tusiheshimiane kwa mengine yoyote.
Hakuna sababu. Lakini kinyume chake leo sisi, hawa watu kila siku wakikaa kwenye majukwaa yao, ima ya siasa, ima iwe ya Maulid au ya Khitma Uislamu kwao ndio kama nini wanaita ile "Door mat", kitu cha kupangusia miguu mlangoni kabla hujaingia ndani.
Hawapati faraja hawaoni raha katika majukwaa, katika mikutano yao mpaka wawabughudhi (Waislamu) au waubughudhi Uislamu. Na ndio hao wakija katika Misikiti yetu tunawapisha safu za mbele. Ndio hao hao wakitualika mafutari tunakuwa wa kwanza, tunagombania kwenda. Na ndio hao hao kwenye harusi zetu tunawaalika. Wakati kwa ushahidi huu wa Mtume (s.a.w.) watu kama hawa hawafai kushirikiana nao kwa hali yoyote. Mpaka watakaporudi katika mstari kama ni Waislamu.
Unaweza ukadhani kwamba haya mambo ni mepesi hayana athari. Mimi nitakupeni mfano mmoja, mfano hai yupo Bwana mmoja alikuwa hapendezi mtaani kwake Kariakoo. Watu wengi hawampendi kutokana na visa vyake, Muislamu.
Sasa kuna Bwana mmoja kafanya shughuli, alikuwa na harusi ya binti yake, akaalika watu wengi sana. Miongoni mwa aliowaalika ni yule ambaye hapendezi pale mtaani.
Khabari zikawafikia watu, kwamba jamani eh miongoni mwa watu walioalikwa ni fulani na fulani nyinyi si mnamjua! Watu wakasema basi vizuri kama huyu Bwana akija, sisi tunainuka, hatukai.
Akija kwenye shughuli sisi tunaondoka. Mwenye shughuli alifadhaika sana. Akamweka mtu kenda akatafuta Mobiteli, kumpigia simu, Bwana wee, tafadhali Bwana, chonde chonde usije. Kwa sababu ukija umenivunjia shughuli. Ukiingia watu wataondoka. Hali imefikia hivyo hadi yule Bwana akarudi katika mstari. Kwahiyo haya mambo hufanyika na yanawezekana kwa sababu yamefanyika katika historia, kwenye Tarekh ya Kiislamu yapo na hakuna sababu leo kwanini Waislamu tuwe mbali na Sunnah hii.
Muislamu anawabughudhi Waislamu kama ni Imamu huna lazima wewe kuswali Msikiti ule. Na kama kwa shughuli yako huna lazima ya kumwalika na akikualika usende, Mumnasihi kama hataki basi mumpige pande kama ambavyo hawa maswahaba, hawa ni maswahaba wa Mtume (s.a.w.) na Mtume aliwapiga pande, na jamii nzima ya Madina iliwapiga pande. Sikwambii mimi na wewe.
Na kama mtu huyu si Muislamu na mifano ipo. Basi Waislamu mmeshindwa kuonyesha kwamba mmechukizwa (na vitendo vyake). Tunashindwa hata kususia kununua vitu vyake. Hilo nalo linahitaji labda kuwa na Organisation, hata wewe binafsi nyumbani kwako lazima (utumie bidhaa zake?). Kwa sababu ukinunua (bidhaa zake) ndio unazidi kumuimarisha kiuchumi. Sasa kadiri unanunua bidhaa zake ndivyo anavyozidi kuimarika kiuchumi na kuwatukana Waislamu.
Nyumbani mama umeshindwa kumwambia mumeo ukileta mafuta fulani mimi sipiki. Kwani lazima upikie mafuta hayo.
Sasa haya ni mambo ambayo tunaweza kuyafanya mmoja mmoja, katika familia na "Community" (Jumuiya) ndogo ndogo na yanaweza kuwa na athari kubwa sana katika jamii yetu.
Nitakupeni mfano mmoja wa Mayahudi. Wayahudi kama mtakumbuka mwaka 1947, haya yanayozungumzwa siku zote holocoast, wameuliwa na Wajerumani, Hitler na kadhalika. Juzi juzi Wayahudi wakapeleka madai katika serikali ya Switzerland, serikali ya Uswisi, wakati wanauawa Ujerumani na sehemu nyingine za Ulaya, palikuwa na dhahabu nyingi sana ambayo iliibwa.
Kwa hiyo Wayahudi waliokuweko Marekani wakawa wameiandikia serikali ya Uswiss kuwaambia lazima walipe fidia, zile dhahabu zilizokuwa zimeibwa mwaka arobaini na saba. Dhahabu ambazo hakuna anayejua idadi yake, dhahabu ambazo si rahisi kujua zilikuwa za nani na nani lakini bado wamesema 'tulipwe fidia'.
Serikali ya Uswiss ikajaribu kukataa. Kwamba kwanini tulipe fidia. Kwanza miaka mingi imepita, haijulikani dhahabu hiyo ilikuwa ni ya nani, haijulikani wingi kiasi gani hata kama tunalipa tunalipa kiasi gani na tunamlipa nani. Wakajaribu kutetea hoja.
Wayahudi wakawaambia sawa, kama hamtaki kutupa , sisi tunasema mmetudhulumu, mmekwiba dhahabu zetu, kama hamkutulipa, tunawapiga vita kiuchumi. Kwa kuanzia Gavana wa New York akasema mimi kuanzia mwakani sitowapa leseni za kufanya biashara zenu hasa za kibenki hapa New York City. As long as mimi ni Gavana wa hapa hamtopata leseni yenu ya kufanya biashara ya Benki. Na sote tunafahamu Switzerland ni mambo ya Benki. Ukishawafungia leseni zao mahala kama New York umewamaliza.
Wao baada ya kuona hivyo mwaka jana mwishoni serikali ya Switzerland ikakubali kwamba "tutawapa fidia na hivi sasa wako katika kufanya 'Negotiation' kiasi gani na watazilipa katika taratibu zipi. Lakini kimsingi wamekubali watalipa fidia. Kwanini kwa kuogopa kwamba wasije wakapigwa vita kiuchumi na Wayahudi wachache tu walioko New York.
Sasa sisi leo Waislamu tuko hapa kwa mamilioni (pengine) sixty percent. Asilimia sitini ya milioni thelathini watu wangapi!
Leo mtu anauza Grocery, ana duka lake pale anauza ulevi, anauza nguruwe na mambo mengine na bado na wewe unakwenda kununua pale pale. Lazima ununue pale? Hakuna duka lingine?
Leo Wakristo mashuleni wanafika kusema kwamba, nakumbuka mimi pale Chuo Kikuu Dar es Salaam. Zamani University tulikuwa tunasoma mpaka Jumamosi. Wakristo wakasema sisi hatuwezi kusoma Jumamosi, kuna hawa wanaitwa SDA wakasema sisi Jumamosi kwetu ni siku ya ibada hatuwezi kusoma. Na wakati mwingine kama ni mitihani wanasema hatuwezi sisi kufanya mitihani Jumamosi kwa sababu ni siku ya ibada. Na ni wachache.
Kwa sababu katika demography ya Wakristo, wengi ni Waroma, wamefuatiwa na nani Anglikani, S.D.A. ni wachache sana mahala kama Chuo Kikuu ndio wachache zaidi, lakini bado wameweza 'ku-demand' kwenye utawala wa Chuo, hatuwezi kusoma Jumamosi, hatuwezi kufanya mtihani Jumamosi. Wamerekebisha.
Leo hii mpaka hivi tunavyozungumza, Chuo Kikuu siku ya Ijumaa saa sita mpaka saa saba kuna kipindi. Badala 'ku-Force Administration' kwamba kwanini tuwe na kipindi saa sita mpaka saa saba tunakuwa 'acomodative' tumekwenda 'ku-adjust time' ya swala. Leo Ijumaa Chuo Kikuu pale MSAUD wanaswali saa saba na nusu. Ili nini watu watoke darasani saa saba ndio wakimbilie kuswali, ukishamaliza kuswali una nusu saa ukimbilie kafeteria saa nane darasani.
Kwanini tusiwaambie Administration sisi ni Waislamu, na 'community' kubwa kuliko hata S.D.A. Na sisi Ijumaa vipindi viishe saa sita. Lakini ... haya mambo tunayaona madogo, hatuko 'conscious' na mambo yetu.
Imefikia hatua leo CCM katika uongozi CCM vijana, leo ukitaka kugombea uongozi kujaza fomu kuna mahala unaambiwa uambatanishe cheti cha Ubatizo. Sasa hebu niambieni. Wale vijana wa CCM nadhani mnalijua hilo.
Lakini leo vijana wangapi wa CCM, hao wa CCM ambao wamejitokeza kusema jamani, kwanini cheti cha ubatizo! Kwa sababu kama ni hoja tunataka kujua huyu ni Mtanzania au si Mtanzania, unaweza kutumia cheti cha kuzaliwa. Na kama cheti cha kuzaliwa huyu mtu hana, unaweza kwenda kuchukua 'affidavit mahakamani au kwa wakili inatosha. Sasa kwanini cheti cha ubatizo!
Waislamu mambo mengi sana tunayachukulia 'For granted' (hatujali) tumeona ah Bwana we, hatuwezi Bwana! Haya mambo tutaweza wapi. Hata mambo madogo madogo tunashindwa ku-question (kuhoji, kuuliza); kwanini cheti cha ubatizo, kwanini tufanye mtihani siku ya sikukuu, kwanini tufanye vipindi Ijumaa viende mpaka saa saba! Unaweza kuyaona ni madogo, lakini athari yake baadae inakuwa ni kubwa sana.
Lazima, lazima tuwe 'very conscious' (makini) na 'Inquisitive (wenye kudodosa mambo). Na hili tunajifunza kutoka kwa wenzetu. Kwa sababu wenzetu katika utawala wa awamu ya pili, kila kitu walikuwa wanakihusisha na Uislamu. Walifika kuandika makala hapa Misikiti inaibuka kama uyoga, kitu kidogo kwa sababu Mwinyi Rais, anawapendelea Waislamu.
Hata kama mtu ana sifa mi nakumbuka wakati marehemu Profesa Malima Waziri wa Fedha, marehemu Rutihinda gavana wa Benki Kuu wakati ule ndio amefariki nafasi yake inataka kujazwa kama Waziri akapendekeza nafasi apewe Dk. Idrisa Rashid.
Sasa Dk. Idrisa Rashid kwanza ana Ph.D ya Economics, pili huyu Bwana amefanya kazi Benki Kuu mpaka akafikia ngazi ya Ukurugenzi. Alikuwa Director (Mkurugenzi) wa Research and Information. Akahama akaenda National Bank of Commerce (NBC) kama Mkurugenzi Mkuu. Kwa hiyo kwanza ana 'qualification' (sifa), pili ni Banker tena wa muda mrefu. Alipopendekezwa yeye kujaza ile nafasi magazeti yote na Wakristo wote wanasema Malima anataka kumpa ile nafasi Muislamu mwenziwe.
Wakati ambapo palikuwa na Gavana Rutihinda 'Diploma International Relation', palikuwa na Gavana Mtei ana B.A. ya Literature , wapi na wapi. Alikuwa Gavana (wa Benki) Charles Nyirabu, mwanafunzi wa Malima, lakini alipopendekezwa Idrisa ikawa balaa kubwa, kwamba ooh Muislamu! Sasa na sisi tujifunze katika kila kitu. Katika kila 'aspect' lazima tuwe na tabia ya 'ku-question' (kuhoji). Kwanini iwe hivi, kwanini isiwe vingine.
Baada ya kuyasema hayo nawashukuru sana. Lazima sasa hivi tuwe, wamesema 'practical Muslims'. Twende vijijini tuzungumze na wazee (tuuhami Uislamu).
--
|
|