Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya wanafunzi Waislamu mkoani Ruvuma wameelezea masikitiko yao juu ya ubaguzi unaofanywa dhidi ya wanafunzi Waislamu mashuleni.
Taarifa ya Jumuiya hiyo RUMUSA imedai kuwa wakati wanafunzi Waislamu wamepigwa marufuku kuvaa hijaab katika baadhi ya mashule wanafunzi watawa Wakikatoliki (masista) wanaosoma shuleni huvaa magauni yao na vilemba bila ya bughudha.
Aidha, imeelezwa kuwa katika shule ya sekondari ya wavulana ya Songea (Songea Boys) masomo yamekuwa yakiendelea wakati wa swala ya Ijumaa. Hali hizo huwafanya wanafunzi Waislamu ama wakose swala au vipindi.
Jumuiya ya RUMUSA inawajumuisha wanafunzi Waislamu wa shule za sekondari za Songea wavulana na Songea wasichana, Ruvuma sekondari, Ruhuwikopamoja na vyuo vya Ualimu Songea (TTC) na Afya (COTC).
Hivi karibuni RUMUSA iliandaa mahafali ya kuwaaga wanafunzi Waislamu wanaomaliza kidato cha sita katika mahafali hizo mgeni rasmi Bw. Abbasi Hussein kutoka CRDB aliwataka wahitimu kuitumia elimu yao vyema kutekeleza wajibu wao katika dini.
Baadhi ya Masheikh waliohudhuria sherehe hiyo walikuwa Sheikh Shaibu ambaye ni mshauri wa vijana wa Kiislamu mjini hapa, Sheikh Shaabani Mbaya ambaye amerejea hivi karibuni akitokea Makka katika ibada ya Hija, Sheikh na Imamu wa Msikiti wa Mkoa Masjid Hudaa Sheikh Mpaka, Imamu wa Msikiti wa Majengo, Sheikh Juma Sanga na Katibu wa Msikiti wa wilaya Masjid Nuru.
Wageni kutoka katika taasisi za dini ni uongozi wa AL-MALLID kanda ya Kusini ukiongozwa na Sheikh Mohammed Kawangu.
Pia Mwalimu wa kujitolea ambaye anasaidia kwa wanajumuiya wa sekondari kuwafundisha masomo ya ziada, Ustadh Yasini Mwaegamile ambaye pia ni mwanachama wa TAMPRO alihudhuria mahafali hiyo.
--
|
|