Na Mwandishi Wetu
WAKATI serikali ikiendelea kushutumiwa ndani na nje ya nchi kwa mauaji ya raia Mwembechai, jeshi la polisi linahaha kusaka kwa siri kanda zilizonasa kadhia hiyo kwa madai kwamba zimehaririwa na baadhi ya watu ili kupandikiza chuki dhidi ya jeshi hilo.
Katika tukio moja la wiki hii, muumini mmoja aliyefahamika kwa jina la Khamis Shemtoi alikamatwa na polisi katika kituo cha Bus mjini Tanga akituhumiwa kumiliki kanda moja iliyosemekana kuonyeshwa ndani ya Bus la Raha Leo likiwa safarini kutokea Dar es Salaam kwenda Tanga.
Imedaiwa kuwa muumini huyo aliyekuwa abiria wa Basi hilo alimuomba dereva aweke mkanda huo ili wasafiri wapate fursa ya kuona yaliyotokea Mwembechai.
Kwa mujibu wa baadhi ya abiria waliopanda Basi hilo, Dereva huyo alikubali kuuweka mkanda huo unaoonyesha mauaji ya kuhuzunisha yaliyofanywa na jeshi la polisi mkoa wa Dar es Salaam.
Abiria hao wameeleza kuwa karibu wasafiri wote waliokuwemo kwenye Basi hilo walisononeshwa kuona polisi wakilenga na kufyatua risasi zilizoacha watu zaidi ya wanne wakikata roho.
Tukio hilo na yale ya polisi kupiga virungu, kumkejeli na kuburuza maiti hizo yaliibua maoni tofauti kutoka kwa wasafiri wa Basi hilo.
Mpaka Basi hilo linaingia Tanga mjini wasafiri hao walikuwa wameona karibu mkanda wote na kuzua gumzo kubwa lililodumu kwa dakika kadhaa wakati wasafiri wakiteremka kituoni.
Haikuweza kufahamika kama Sheikh Shemtoi alikamatwa mara tu baada ya kuteremka katika Basi hilo au hatua chache kutoka kituoni hapo, hata hivyo, habari kutoka kwa jamaa wa karibu wa muumini huyo zinasema kuwa alivamiwa na watu waliojitambulisha kuwa ni maaskari na akalazimishwa kuelekea kituo cha polisi Chumbageni.
Gazeti lilipowasiliana na ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga lilielezwa kuwa Kamanda huyo alikuwa safarini Arusha na Afisa Msemaji (Staff Officer) kwa niaba yake alikuwa akihudhuria kikao cha kikazi.
Hadi ANNUUR inakwenda mitamboni ofisa huyo hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo.
Wakati huo huo kukamatwa kwa muumini aliyetuhumiwa kumiliki kanda ya mauaji ya Mwembechai kumezusha zogo kubwa mjini Tanga.
Taarifa ambazo ANNUUR imezipokea zinaeleza kwamba waumini wamekuwa wakihoji uhalali wa hatua ya polisi kukamata watu wanaowatuhumu kumiliki kanda ya Mauaji ya Mwembechai.
"Kama hawapendi kanda hiyo ionyeshwe kwa sababu yanayoonekana humo yanalidhalilisha jeshi hilo mbona hawajawachukulia hatua watendaji wale waliokiuka sheria za jeshi hilo", amehoji Bwana Adamu Salum mwenyeji wa Lushoto mkoani humo.
Aidha watu wengi wamehoji sababu ya "kuzuiliwa" kanda hiyo wakati ambapo kuna mikanda kadhaa yenye kuonyesha matukio yasiyopendeza ambayo haionekani kulishughulisha jeshi hilo.
Waliitaja baadhi ya mikanda hiyo kuwa ni pamoja na ule wenye kuonyesha mauaji ya Rwanda (1994) ambao miezi michache kabla ya uchaguzi wa mwaka 1995 ulikuwa ukionyeshwa kupitia kituo kimoja cha TV jijini, mingine ni onyesho la mauaji ya Soweto na Uganda wakati wa utawala wa Idd Amin.
Halikadhalika wananchi hao walionyesha kushangazwa na kauli ya afisa mmoja wa polisi iliyoripotiwa na gazeti moja binafsi la kila siku kwamba ubaya wa kanda hiyo ni kule kuhaririwa na kuondolewa baadhi ya matukio.
"Badala ya kuwaghasi watu wanaotazama kanda hizo zinazodaiwa kuhaririwa, polisi ionyesha kanda ya kweli ili uongo ubainike", amedai Mwalimu wa shule moja ya sekondari mjini hapa.
Mauaji ya Mwembechai yameliweka jeshi la polisi nchini katika hali ngumu ambapo hadi sasa haijafahamika ngazi za juu zimechukua hatua gani ingawa zimeonyesha kukiri kuwepo kwa uvunjaji wa sheria za jeshi hilo katika tukio hilo.
Akihojiwa katika kipindi cha Generali on Monday hivi karibuni afisa mmoja (Mwalimu) wa chuo cha polisi alisema polisi kumuua au kumpiga mtuhumiwa ni kuvunja sheria za jeshi hilo na ni kosa la jinai.
Afisa huyo alikuwa akijibu swali kuhusu watu wanaowarushia mawe polisi katika ghasia na wale waliowekwa chini ya ulinzi.
Akithibitisha kuwa polisi kumpiga mtuhumiwa ni kosa, Mwalimu huyo wa Chuo cha Polisi aliwaomba wananchi waathirika wapeleke taarifa za vitendo hivyo polisi na kwamba jeshi hilo litachukua hatua dhidi ya watendaji wake wanaovunja sheria.
--
|
|