Na Abu Kalam
IMAMU Abu Hanifa jina lake kamili ni Nu'man bin Thabit Abu Hanifa. Yeye alizaliwa kufa huko Iraq mwaka wa 80 Hijiria. Yeye ni katika watu wa kipindi cha Tabiin kwani aliwashuhudia maswahaba wa Mtume (s.a.w.) ikiwa ni pamoja na Khalifa Ali bin Abi Taalib na Anas bin Malik.
ALIPATA elimu yake katika miji ya Kuba, Basra, Makka na Madina. Miongoni mwa waalimu wake walikuwa Abdallah bin Umar mtoto wa Khalifa Umar bin Khattaab.
Pamoja na kujikusanyia elimu nyingi na umaarufu kutokana na elimu na ucha Mungu wake; Imamu Abu Hanifah alibakia kuwa mnyenyekevu na mwenye msimamo usiotetereka katika dini.
Mwaka 146 Khalifah Mansour alimteua Abu Hanifah awe Kadhi, lakini alikataa akitoa hoja kuwa nafasi hiyo ni nzito kuliko uwezo wake. Mansour alikarisika kama vile hakuridhia uteuzi wake upuuzwe.
Akizingatia ujuzi na uwezo wa Abu Hanifah, Mansur alimwambia Abu Hanifah kwamba itakuwa kasema uongo akisema kuwa hawezi kuwa Kadhi kwa madai kwamba hana elimu . Jibu la Abu Hanifah lilikuwa jepesi. Alimwambia; "kama mimi ni mwongo basi kauli yangu kuwa sifai ni sahihi kwani mwongo hawezi kuchaguliwa kuwa Kadhi". Kwa jibu hilo alitupwa jela.
Kutokana na maombi ya watu Mansur alimruhusu Imam Abu Hanifah kuendesha darsa hapo hapo jela. Watu wakazidi kufurika jela kuhudhuria darsa. Abu Hanifah alikufa katika mwezi wa Rajab 150 A.H.
Jeneza lake liliswaliwa mara sita na kila mara watu zaidi ya hamsini elfu walisimama kumswalia. Na hata baada ya kuzikwa watu toka sehemu mbalimbali duniani walifurika kuja kuswali swala ya jeneza.
Kwa muhtasari; huyo ndiye Imam Abu Hanifah ambaye Masheikh wengi humnukuu katika darsa zao za Fiqh.
Lakini Masheikh wangapi wanadarsa? Masheikh wangapi wanasomesha?
Imam huchaguliwa na waumini kutokana na elimu yake na sifa nyingine muhimu, Maimam wangapi hung'ang'ania Uimam hata kama waumini hawamtaki. Masheikh wangapi hugombea na kung'ang'ania Usheikh wa Wilaya, Mkoa na Umufti hata kama kuwepo kwao hakuwasaidii lolote Waislamu.
Masheikh wangapi vikao vyao ni pamoja na makada wa vyama vya siasa na viongozi wa serikali badala ya Waislamu kufurika majumbani mwao kutafuta nasaha na miongozo.
Tunapoona baadhi ya Masheikh wetu wakijikurubisha kwa viongozi wa vyama vya siasa na serikali badala ya waumini (wakiyaelewa na kuyatatua matatizo yao), ndio hapo tunajiuliza; hivi hawa hawakuwaelewa Masheikh wao? Masheikh wetu wana hiari, ama kuzikwa na maelfu ya Waislamu au watawala na makada wa vyama vya siasa.
--
|
|