Na Mwandishi Wetu
HISTORIA ya ustaarabu wa mwanaadamu imeshuhudia kupanda na kuporomoka kwa mifumo mingi. Imeshuhudia kusimama na kuanguka kwa serikali nyingi na pia kustawi na kusambaratika kwa jamii kadhaa.
Migogoro, migongano na harakati ni tabia zilizoandamana na ustaarabu wa mwanaadamu na mabadiliko yake katika vipindi vyote vya historia.
Upinzani, vurugu na harakati kama si mambo ya msingi basi ni hali za lazima kuweza kuleta mabadiliko kwa jamii na muruwa wake.
Imejitokeza mara nyingi ulimwenguni ama kwa watu mmoja mmoja au kijamii kwamba amani, utulivu wa kweli na kuheshimiana hupita mkondo mrefu ambao hutoka kwenye chanzo cha kuoneana yakafuatia malalamiko, kujitoa muhanga, hamkani, sulhu au mapambano na vifo.
Wengi tunafahamu yaliyotokea Ufaransa karne ya 19 kwamba ni matokeo ya wengi kutumikishwa kibwege. Walipolalamika na kupuuzwa ulifuatia umwagaji mkubwa wa damu ambao hivi sasa umewaweka watu wa huko katika hali ya kuheshimiana. Hakuna anayemwangalia mwingine kwa jicho la dharau, kejeli na kupuuzana.
Hali ni hiyo hiyo sehemu zote zile zilizoonja matokeo ya kudanganyana, propaganda na kutojali malalamiko ya wengi au wachache.
Ubinadamu hauna kawaida ya, labda pawepo wasiojitambua, kukubali na kususuwaa mahali ambapo shida, dhiki, ufukara, maonevu na ukandamizaji ndio habari za kila siku.
Pengine mtu angeweza kufikiria namna ambavyo wachache au wengi wanyonge wanavyoweza kujiunga na kujiimarisha wakaanza kutafuta njia, namna au uwezekano usio rasmi wa kuondokana na ustaarabu usioridhisha.
Hapa ndipo pasipoweza kutabirika. Na kwanini asifikirie hivyo ilhali milango yote ya kidiplomasia na taratibu rasmi imefungwa, "wenyewe" hawataki masikilizano wala majadiliano.
Kwa muda mrefu hapa nchini umedumu ustaarabu usiovumilika wa baadhi ya wananchi kutotendewa haki, kunyimwa wanayostahiki, kupuuzwa, kukejeliwa, kubaguliwa na kukandamizwa.
Kumejengwa 'System mchujo' ambapo zaidi ya asilimia 50 ya wananchi huishia mitaani. Ni mfumo wa utawala ulioridhika kukosa uwakilishi wa kundi kubwa la wananchi kisha bila ya aibu ukatangaza kuwepo amani na utulivu.
Asilimia hiyo imedumu katika hali ya kutazama wenzao wakipaa katika anga za elimu, hatimaye kukamata nafasi nyeti za maamuzi na utendaji. Wale wenye vipaji vyao wamekoseshwa kwa makusudi fursa ya kuendelezwa na wachache waliobahatika wameshindwa kutoa mchango wao ipasavyo. Jamii hii haina tofauti na mifugo ambayo huswagwa machungani asubuhi na kurudishwa jioni.
Huu ni mwaka wa 30 tangu Waislamu waanze kuhoji nafasi na hatima yao katika Tanzania huru. Serikali imekuwa ikikumbushwa kuhusu ustaarabu huu ili ichukue hatua zifaazo, hata hivyo si tu haijaweza kufanya hivyo bali imekuwa ikienda mbio kuwafanyia vitimbi wale wenye kujipa'vilimilimi' na umbele mbele.
Sambamba, wamekuwa wakijitokeza watu au baadhi ya vyombo vya habari au madhehebu kupotosha ukweli kuhusu upogo wa ustaarabu wetu. Hukataa katakata kukiri kwamba nchini hapa upo mgogoro unaotishia kuliporomosha taifa. Hukataa madai yenye ushahidi ya kundi kubwa la wananchi kwamba haliridhishwi na ustaarabu uliopo. Hukanusha kuwepo mgogoro wa kijamii unaoweza kuiangamiza jamii yetu ambao serikali imekuwa ikiulea kwa hila na mbinu ambazo mara nyingine huwa vichekesho.
Hivi karibuni nilibahatika kujumuika na 'wanene' fulani, nikapata fursa kusikia wasemavyo kuhusu mchemko uliopo mitaani na Misikitini. Lahaula! Niliyoyasikia yalinipa ishara kuwa kuna wanaocheza 'makida makida' jirani na simba mwenye njaa!
Mimi nilihisi hatari inayozidi kupiga hodi kadri wasiotendewa haki wanavyozidi kuelewa. Lakini kwa wenzangu wale hakuwepo hata mmoja aliyevuta taswira ya nchi jirani ambapo kulala na kuamka aliyekuwa Mheshimiwa au tajiri mkubwa hivi sasa anapanga foleni kigoma kupata mlo ambao hapo awali kule kuuona tu angechefukwa.
Hata hivyo, kwa jinsi walivyojipanga ilionekana dhahiri asingekuwepo wa kujisumbua kufikiria na kushauri vinginevyo! Nilikata tamaa kabisa na kuona kwamba hakuna kinachongojwa ila msiba mkubwa mbeleni ambao hautachagua Mheshimiwa, tajiri, afisa, tarishi, mtwana, maskini, mtoto, mama, baba, muislamu, mkristo au mpagani.
Hiyo ndiyo hali ya watu ambao wangepaswa kuumiza vichwa kutafakari na kuchambua mambo ambayo hayaelekei kabisa kuinufaisha jamii yetu. Kama wangekuwa na chembe ya ubinaadamu ungewafanya wavute hisia kuona kwamba hakuna ambaye shida, mateso, kejeli na manyanyaso ni hali zilizozoelekea kwake.
Chini ya mazingira haya ndipo ninapoona haja kwa watanzania kujadiliana mitaani, mashuleni, vyuoni na kila eneo lenye mkusanyiko wa watu kuhusu hatima ya nchi yao. Sishauri kupita njia iliyowafanya Wafaransa na watu wote wa Ulaya waheshimiane lakini kama hapana budi basi isije ikasemwa watu hawakusema.
--
|
|