MAKALA
 
 
Nini siri ya kuzeeka?

Na Hawra Shamte
 

KATIKA kudra zake Mwenyezi Mungu ni kumuumba mwanaadamu katika umbo na sura aliyoipenda Yeye Allah (s.w.) kisha akampa akili, fahamu, macho na masikio.

Na mwenyewe akasema hakika nimemuumba mwanadamu katika umbo lililo bora kabisa.

Hivyo katika ibra hii ya kuumbwa mwanaadamu ni alama tosha kuwa yupo muumbaji.

Katika umbo la binadamu kuna mengi ya kujiuliza ambayo wengine hata watafiti kama watayachunguza kwa kiasi gani bado kitabaki ni kitendawili kwao.

Hebu tuchukulie mfano wa roho imeumbwa kwa kitu gani na inaingiaje katika mwili wa binaadamu na inatokaje na kumwacha binadamu akiwa mfu ni kitendawili cha kuumiza akili za wachunguzi wa mambo.

Na wakusanyike madaktari wa kila aina na wajaribu kuyanusurisha maisha ya mgonjwa kwa baadhi wawezavyo, wamzunguke na wamwekee ulinzi bado kudra ya Mwenyezi Mungu itapita bila ya wao kuwa na habari. "Na sisi tuko karibu naye zaidi kuliko hata mshipa wake wa shingo". - Qur'an.

Hebu tuchukue mfano wa tumbo, tumbo ni mashine ambayo haijawahi hata kuigwa na mtaalamu yeyote duniani awe wa sayansi au wa teknolojia ni mashine ya ajabu iliyo mwilini mwa mwanaadamu, inafanya kazi saa 24 tena kwa mpangilio maalumu. Je alishawahi kutokea mtaalamu ambaye anaweza kutengeneza angalau tumbo la spea ili kama mwanadamu atapata hitilafu ya maradhi katika tumbo lake basi angalau awekewe jingine?

Mwanaadamu anapotaka kuchunguza rehema za Mungu mwisho hufikia kikomo na kukiri kwamba tumeshindwa kutambua, lakini hapo ndipo anapopaswa akiri kuwa Muumba yupo na kutupilia mbali dhana isiyoingia akilini kuwa hivyo ndivyo ilivyo ni kwa sababu ya maumbile "Nature".

Wanayansi wa Japan wanafanya utafiti kutaka kujua nini siri ya kuzeeka.

Walimdunga panya sindano ya tosgene (genetic inayotokea na mnyama mwingine) ambayo waliita klotho, katika utafiti huo waligundua kuwa klotho inasababisha panya kuwa na dalili za kuwa na umri mkubwa kama vile kuwa na ugonjwa wa mifupa, maisha mafupi, kutolewa na uwezo wa kuzaa na magonjwa yanayotokea nyakati za uzeeni.

Kutokana na utafiti wao wanadhani kuwa uzee huenda ukawa na mahusiano ya moja kwa moja na Genes za Genetic mutation.

Kwa ufupi mpaka hivi sasa hawajaijua siri ya viumbe kuzeeka. Katika kudra zake Allah amejaalia hatua tatu katika viumbe vyote vyenye uhai, huanza na uchanga, udogo, ujana/ukubwa na uzee/ukongwe. Hata miti nayo hupitia hatua hizo, je wanasayansi wameshachunguza sababu zinazopelekea miti kuzeeka.

Je, hawatafakari jinsi Mungu Muumba alivyoumba miti na akaijaalia matunda ya kila aina na ladha tofauti tofauti , je, haijatosha tu hiyo kuwa alama kwa watu wenye akili.

Kipi ni kigumu zaidi kuumba?

Binadamu au mbingu na ardhi na nyote vilivyomo? Mwenyezi Mungu ameumba mbingu na ardhi na viumbe wote na anaweza kuumba ulimwengu kama huu tena bila hesabu.

Mwenyezi Mungu ameuumba ulimwengu na vilivyomo kwa kanuni na sababu maalumu ili wanadamu wapate kutafakari.

Utafiti juu ya maumbile ni mzuri iwapo lengo la utafiti ni kutaka kumjua Allah zaidi ili amuabudu.

Mtaalamu wa viumbe bahari wa Ufaransa Jack Jaques alifanya utafiti wa mwenendo wa bahari na kugundua kuwa katika bahari kuna maji baridi na ya chumvi yanayopishana bila kuingiliana na alipoisoma Qur'an akakuta kuwa jambo hilo limeelezwa bayana katika Surat Arrahman.

Na katika bahari kuna bahari mbili, moja ina maji machungu yenye chumvi na nyingine baridi yenye kukata kiu, baina yake kuna kizingiti kinachofanya yasiingiliane.

Je ni kitu gani enyi wanaadamu na majini kinachowafanya mkadhibishe?

Hadi leo wanasayansi wameshindwa kuwelewa ni kizuizi gani kilichopo baina ya maji hayo ya bahari kinachosababisha yasichanganyike.

"Hakika tumemuumba mwanadamu katika umbo lililo bora kabisa kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini".

Binadamu anapokuwa mzee sana anarudi uchanga na anakuwa chini kuliko mtoto mchanga, anakuwa hana fahamu tena wala raha ya dunia tofauti na mtoto ambaye pamoja na udogo wake waweza kumsemesha akatabasamu. Mtu anapokuwa mzee hupoteza wajihi na haiba yake, nguvu mwilini humalizika na akili hupungua hilo ni fundisho tosha kwa mwanadamu kukumbuka atokako na anakokwenda. Je, ana hiari juu ya hilo?

Je, mwanaadamu haangalii jinsi alivyoumbwa na akastaajabu?

Tumemuumba mwanaadamu kutokana na maji yachupayo. Yanayotoka mgongoni kwa mwanamume na katikati ya kifua cha mwanamke, kisha tukayabadilisha na kuwa pande la damu, kisha tukaiweka mifupa na kwisha nyama, je atatushinda kumzeesha na kumfisha na kisha kumuumba kwa mara nyingine tena tutakapomfufua hali ya kuwa hata mifupa yake ilishasagika sagika na kugeuka vumbi?

Jibu ni dogo sana kwa Muumba kwani Yeye anapotaka kitu kiwe hukiamrisha tu "kuwa na huwa".

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook