Tupeni kanda zisizohaririwa
Ndugu Mhariri
TUMEFAHAMISHWA na gazeti la Mtanzania la Jumapili Mei 23, mwaka huu kwamba polisi wanawasaka watu wanaozifanyia uhariri kanda za mauaji ya Mwembechai.
Tunaomba polisi itusambazie ambazo hazijahaririwa kabisa ili tupate taarifa sahihi kabisa.
Na kama Kamati inavyosambaza zile zilizohaririwa duniani kote, basi polisi (serikali) nayo isambaze zake zisizohaririwa kote huko.
Jaafar Khalfan,
Kilosa.
Ndugu Mhariri
TUNAYO matatizo na agenda zetu muhimu kwa maendeleo yetu. Hatuoni Masheikh wetu wakikutana kusoma khitma ya waliokufa Mwembechai wala hatusikii katika khutba zao wakiligusia hilo. Lakini watatueleza ya Kossovo.
Waliokufa kwa njaa Ulanga karibu asilimia 90 ni Waislamu, hatuwasikii wakipitisha mchango kwa Waislamu kuwanusuru ndugu zetu hao.
Lakini hao hao hutumia mimbari za Misikiti yao kuhimiza umoja, upendo na mshikamano bila kujali dini na madhehebu.
Masheikh wanaruhusiwa kuozesha Kiislamu lakini talaka wanaambiwa lazima iwe ya mahakama ya kikafiri. Hatuoni Masheikh wakikutana kulijadili hili ila waweza kusikia wameitwa kujadili mikakati ya kudhibiti baadhi ya Misikiti inayoonekana kero kwa watawala.
Ni vyema Waislamu tuwajue mapema Masheikh wetu ni wapi.
Muhsin Ahmad,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
HAKIKA inasikitisha sana inapofikia hatua Muislamu kuchukua jukumu la kwenda kusoma dua na kumswaliaMtume Mtukufu wa Daraja (s.a.w.) ndani ya nyumba ya asiyekuwa Muislamu.
Katika taarifa mbalimbali za bahari kupitia televisheni na magazeti zilielezea habari ya zawadi ya nyumba aliyopewa Rais Mstaafu wa awamu ya kwanza J.K. Nyerere na jeshi la Wananchi wa Tanzania, nyumba ambayo iko katika mkoa wa Mara.
Inasemekana kuwa baadhi ya Maustadh katika mkoa huo waliwakusanya wanafunzi wao na kwenda kuomba dua ikiwa ni pamoja na kumswalia Mtume yaani Maulid makubwa yalisomwa ili Mwalimu Nyrere aitumie kwa usalama nyumba yake hiyo.
Swali linakuja, ruhusa hii tunaipata wapi? Au ni kwa sababu tu ya maslahi kidogo watupayo wasiokuwa Waislamu na je, yatatufikisha wapi mambo hayo? Kwani Mtume wetu Muhammad (s.a.w) anasema; "Hayakuwa haya maisha ya dunia isipokuwa ni starehe kidogo kabisa na zenye kuisha".
Hivyo ndugu zangu Waislamu tusidanganywe na starehe hizi zenye kupita na tufanye mambo ambayo yatakuwa ni nusra kwetu mbele ya Allah (s.w.). Wala tusihangaike katika kuwafurahisha wasiokuwa Waislamu kwani Allah (s.w.) anatueleza ndani ya Qur'an kuwa; "Wala hawatakuridhieni Mayahudi na Manaswara mpaka mfuate mila zao". (2:120)
Rahman bint Salum,
P.O. Box 72740,
DSM.
Madai ya msingi ya Waislamu
Ndugu Mhariri
KWANZA namshukuru sana Bwana Abu Burhanuddiin katika makala yake iliyosema "Madai ya msingi ya Waislamu" iliyoandikwa katika toleo No. 200 la gazeti hili tukufu la ANNUUR.
Nikiikumbuka ziara ya Mheshimiwa Makamu wa Rais alipotembelea Manzese katika yake ya mkoa wa Dar es Salaam alipojitokeza kijana wa Kiislamu na kuuliza swali la msingi kabisa, wafuasi wake wana CCM wakaanza kumzomea yule kijana mpaka akashindwa kujieleza zaidi.
Watukufu Waislamu mimi nilishangaa sana ila sikupata jibu la mshangao wangu, kwamba katika kundi lile la wana CCM hivi pale hakuna Waislamu ama labda wote wale ni Wakristo?
Ila nakumbuka Bw. Mrema waliokuwa wanachama wake walipoandamana na hatimaye kumwagiwa maji na gari la F.F.U. Bw. Mrema alisema "nilifikiri nagombana na Bw. Marando, kumbe nagombana na serikali". Tayari ameshamjua adui yake.
Inawezekana kabisa Waislamu wanamjua adui yao mkubwa lakini bado hajajitokeza vizuri, lakini katika hali kama hii ya kuzomeana basi adui atajitokeza.
Watukufu Waislamu, Bw. Abu Burhanuddin kwa mtizamo wangu labda alikuwepo Manzese alipotoka hapo tu alienda kushika kalamu na kuandika.
Ndugu yangu Abu amezitaja dhulma kewnye makala yake kuwa, Waislamu tunataka kulinda na kuhifadhi Uislamu wetu nchini kwetu ambako kunahitaji makubaliano ya msingi kabisa ya namna ya kuendesha nchi baina ya sisi Waislamu na Wakristo, kwamba tutaongoza nchi hii kwa misingi ya dini zetu bila kudhulumiana na kulinda mazingira ambayo huenda yatakuja kuparaganya nchi. Tushikamane na kulipigania hili.
Jambia Bilali,
Salasala,
Mtongani.
Ndugu Mhariri
NAOMBA nafasi katika gazeti letu hili la ukombozi wa wananchi ili niweze kueleza mtazamo wetu Waislamu katika kudai haki zetu kutoka kwa serikali yetu ya Tanzania.
Kwanza kabisa napenda kumfahamisha Mh. Makamu wa Rais Dk. Omar Ali Juma na wengine wenye mtazamo kama wa kwake, sisi Waislamu tunajaribu kuomba haki zetu isidhaniwe tunaomba kufunga na kwenda kuhiji tu, kwanza suala la kufunga, kuhiji au tunataka kufunga kwa sababu ni amri kutoka kwa Mola wetu (s.w.) haiitajiki kumuomba kiumbe yeyote yule si jini au binadamu, hizi ni mbinu za kutaka kuwazubaisha Waislamu na sisi tunasema tupo macho htukubali propaganda yoyote ile.
Katika ziara ya Dk. Omar huko Manzese wakati wa kukagua shughuli za wananchi iliyomalizika alisema serikali haijawaingilia Waislamu haki zao zinazohusu kuabudu, kama kufunga na kwenda kuhiji, siyo haki hizi tu zipo zingine ambazo zinapodaiwa zinaitwa ni nyeti sijui unyeti huu unakuja vipi na wakati na sisi Waislamu ni raia wa Tanzania tunawajibu wa kudai haki zetu kama raia wengine lakini haki zetu zinaitwa ni nyeti maana yake hazistahiki kudaiwa.
Daima kuna wajibu na haki kwa hiyo haki haiwezi kupatikana bila ya kutekeleza wajibu na wajibu unapotekelezwa ni lazima haki itekelezwe na ikiwa haitekelezwi ni lazima matokeo mabaya yatatokea baina ya mdai na mdaiwa, kwa maana hiyo sisi Waislamu kama raia wengine wa Tanzania tunatekeleza wajibu wetu juu ya serikali kwa hiyo lazima tupewe haki zetu nazo zinajulikana kwani si lazima kuzitaja hapa.
Kama kuzitaja zimekwisha kutajwa kila siku isipokuwa zinafumbiwa macho na kuwaita wale wanaozidai siasa kali, lakini hayo yote tumekwisa yang'amua ni mbinu tu hizi za kumpa adui apate kukunyamazisha lakini tutaendelea kudai haki zetu mpaka damu ya Muislamu wa mwisho kwani hii ni kheri kwetu mbele ya Mola.
Khamis Kassim Khamis,
Al-Furqan Muslim Sc.
School,
Dar es Salaam.
Ndugu Mhariri
NAPENDA kutoa maoni yangu katika gazeti lako lenye nuru kwa wasomaji kuhusiana na tabia mbovu iliyoota mizizi katika jamii yetu.
Allah (s.w.) ametujaalia muongozo usiopitwa na wakati na hakutufunulia kuwa tujipangie sheria wenyewe kwa matamanio yetu.
Leo hii tunakwenda kinyume kabisa na muongozo huu, jamii yote imelifumbia macho na kulizibia masikio suala la hijab kiasi cha kujishushia hadhi. Mfano mzuri ni watangazaji wa Televisheni Zanzibar (TVZ), siku nyingi nilibahatika kuwangalia televisheni hiyo, ni jambo la kusikitisha sana pale watangazaji wa kike wa televisheni hiyo ambao ni Waislamu, zamani walikuwa wanavaa hijab siku zote, siku hizi hawavai hijab tena isipokuwa siku ya Ijumaa tu.
Hiki ni kielelezo kizuri jinsi tulivyoyageuza matamanio yetu kuwa Mungu na kuamua kujifuatia sheria kinyume na za Allah (s.w.) na matokeo yake ni kupotea na kuangamia.
Hebu tuzingatie Qur'an 24:31 na tuiingize aya hiyo katika vitendo sio kuisoma tu na kuikariri kisha tujirekebishe kwani sheria za Allah (s.w.) zipo katika misingi ya kimaumbile na hazipitwi na wakati.
Mwisho napenda kuwakumbusha wana-TVZ hao pamoja na wote wenye sifa kama zao kuwa Allah (s.w.) yupo kila sekunde na kila siku sio siku ya Ijumaa tu. Kama wenzetu hao wanavyofikiri. Wanaotanabahi ni wale wenye akili tu.
Zulekha S. Issa,
Ubungo Islamic High School,
Dar es Salaam.
--
|
|