Fahari toleo la 1. No. 002/3 Februari 28, 1989
WAZIRI Kiongozi wa zamani wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ndugu Seif Sharrif Hamad, amemwandikia Mwenyekiti wa CCM, Mwalimu Nyerere barua ambayo yeye mwenyewe ameiita "ya kuweka kumbukumbu kuwa sahihi". Kwenye ufunguzi wa barua hiyo, Ndugu Hamad anasema kwamba madhumuni ya barua hiyo sio kulalamika, wala kuomba radhi maana hakubali kuwa amefanya kosa.
Barua hiyo yenye kurasa 20 na madondoo 46, inaonekana kuwa Ndugu Hamad kaiandika kwa niaba ya viongozi wengine sita wa Zanzibar ambao walifukuzwa uanachama wa CCM pamoja nae katika mwezi Mei mwaka jana. Sehemu nyingi katika barua hiyo anazungumzia juu ya "wenzangu".
Barua hiyo ambayo iliandikwa Agosti 21, 1988, siku mia tangu afukuzwe uanachama, imetumwa kwenye anuani ya Mwalimu Dodoma ikiwa na kumbukumbu SSH/28/88 na licha ya kunakiliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano Ndugu Mwinyi, Waziri Mkuu na Makamu wa Rais, Ndugu Warioba, Rais wa Zanzibar ambaye pia ni Makamu wa pili wa Rais wa Muungano Ndugu Wakili na Katibu wa CCM, Ndugu Kawawa; pia amewatumia nakala viongozi sita waliofukuzwa uanachama na Rashid Hamad Hamad, aliyevuliwa Uenyekiti, ambao anawaita "wazalendo wa kweli".
Ndugu Hamad kwenye barua hiyo anadai kwamba tuhuma juu yake zilibuniwa na "waasi" na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu wa CCM, kwa maelekezo ya Mwenyekiti.
Aongeza kuelezea kwamba ziara ya Katibu Mkuu wa CCM katika mikoa ya Zanzibar mnamo Mei, mwaka wa jana iliandaliwa kwa madhumuni ya kutoa kisingizio cha kuwafukuza.
Pia anaelezea kwamba kuchukuliwa hatua ya kinidhamu kwa viongozi wa Bara, Ndugu Paul Sozigwa, Meja Jenerali Mayunga na Ndugu Macha zilikuwa ni hila za Mwenyekiti za kujenga hoja dhidi yao, na madhumuni hasa yalikuwa kuweza kumpa Mwenyekiti kisingizio cha kudai baadaye kuwa wao sio peke yao waliochukuliwa hatua za nidhamu na chama.
Ndugu Hamad katika barua yake hiyo aelezea kwamba yeye ni mmoja wa Wazanzibari wachache waliojaliwa kushika nyadhifa nzito katiak chama na serikali, na alielezea kwamba moja ya sababu ya kuyapata madaraka hayo ni kwamba "Mwenyezi Mungu alikwisha mwandikia". Lakini pia akubali kwamba viongozi wakuu hasa Mwalimu Nyerere walimwezesha kupata uongozi huo.
Aongeza kusema kwamba Rais Wakil alimteua kwa shingo upande kuwa Waziri Kiongozi na isingekuwa Mwalimu Nyerere pengine asingeteuliwa. Kuhusu kampeni ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Ndugu Hamad anadai kuwa yeye hakupangiwa majukumu yoyote isipokuwa kufungua kampeni hiyo tuu.
Barua hiyo pia ililalamika kutoteuliwa kwa Seleman Seif Hamad, Khatib Hassan Khatib na Shaban Mloo, kugombea nafasi ya NEC kwenye uchaguzi wa taifa wa chama uliopita.
Ndugu Hamad kwenye barua hiyo alikiri kuwa yeye na "wenzake" walipewa nafasi ya kujitetea pia akubali kwamba ukimwondoa Ndugu Yusuf Rajab Makamba ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa CCM wa wilaya ya Wete, hakuna mjumbe hata mmoja wa NEC wa Tanzania Bara ambaye alichangia mjadala huo.
Kwenye barua hiyo ndugu Hamad alikiri kwamba mnamo mwaka 1985 alifanya kosa, na baada ya kukubali kosa lake alipewa onyo na Kamati Kuu.
Kwenye dondoo la 23 la barua hiyo, Ndugu Hamad asema, "Mheshimiwa Mwenyekiti, kusema kweli, chama chenu kina kasoro ya kupenda mno na kuchukia mno. Mno kwa njia yeyote ile, mbaya".
Uchunguzi wa jarida hili huko Zanzibar umeonyesha kwamba barua hii imewafikia zaidi ya walionakiliwa, Mwandishi wa makala haya, makala yangu niliipata si kutoka kwa mmoja wa hao walionakiliwa. Pia inaeleweka kuwa wajumbe wa Halmashauri kuu ya Taifa kwenye mkutano wao uliofanyika huko Dodoma mapema mwaka huu, walionyesha nakala hiyo.
--
|
|