Na Mujahid Mwinyimvua
WIKI iliyopita vyombo vya habari vimeripoti kauli ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuhusu maji ya kunywa ya kwenye chupa aina ya "MASAFI".
Gazeti la Mtanzania la Mei 25, mwaka huu limeripoti kuwa: "Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaonya wananchi wa Zanzibar dhidi ya matumizi ya maji ya chupa aina ya "MASAFI" yanayotoka nje ya Zanzibar, kwamba si masafi kwa matumizi ya binadamu".
Gazeti hilo linaendelea kuripoti kuwa: "Ofisa mmoja wa Wizara ya Afya Zanzibar alitangaza juzi kupitia televisheni ya serikali ya Zanzibar (TVZ) kuwa maji aina ya "MASAFI" yanayoingizwa kutoka Dar es Salaam yamechunguzwa na mkemia mkuu wa serikali ya Zanzibar na kugundulika kuwa si masafi".
Kauli hii ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni nzito na inaweza kuleta huzuni siyo tu kwa wafanyabiashara walioathirika bali pia kwa wananchi wote wanaojali haki.
Kuna mazingira kadhaa katika tukio hili yanayochangia wapenda haki kuwa na huzuni.
Zaidi ya hayo, wawekezaji walio makini na ambao wanafanya kazi zao za uwekezaji (Investment) kisayansi, haitakuwa rahisi kuwashawishi na wao kukubali kuwa, serikali ya Zanzibar inafanya mambo yake kisayansi licha ya kuwa na idara ya Mkemia Mkuu.
Kama mtaalamu naona ninawajibu wa kuliweka jambo hili wazi zaidi ili serikali kwa upande wake ione wapi, "imeteleza" na wafanyabiashara walioathirika na wananchi kwa ujumla nao waweze kuelewa zaidi ili wachukuwe hatua zitakazoweza kuondoa dosari iliyojitokeza.
Kwa ujumla tunaweza kusema kuwa, azma ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa kauli nzito juu ya maji ya chupa aina ya "MASAFI" yanayotengenezwa Dar es Salaam (Barabara ya Mandela) na kampuni ya Maji Masafi Limited ni kutaka kulinda afya za wananchi wake.
Hata hivyo, unapofanya jambo lolote kwa nia nzuri, lakini katika mazingira ya utata kama ilivyotokea katika suala hili tunalolijadili ni vigumu sana walengwa (wananchi) wako kukuelewa kuwa ulikuwa na nia nzuri ya kuwasaidia.
Katika suala hili, eneo la kwanza linalozaa maswali mengi ni pale serikali iliposema kuwa: "Maji ya chupa aina ya "MASAFI" si masafi kwa matumizi ya binadamu".
Unaposema maji fulani sio masafi maana yake ni kuwa maji hayo ni machafu. Swali linakuja: Uchafu wa maji ya chupa aina ya "MASAFI" ni yapi?
Swali hili ni muhimu kwa sababu akili ya mwanadamu haitaki " kuburuzwa", na hasa katika zama zetu hizi za sayansi na teknolojia. Si hivyo tu bali pia, mwananchi anawajibu wa kujua kwa kina uchafu wa kitu fulani (au ubaya wa jambo fulani) ili aweze kuelewa vizuri na hatimaye aweze kujiepusha siyo tu na kitu hicho bali pia na vitu vingine vya sampuli hiyo.
Kwa kuzingatia ukweli huo, nachukua nafasi hii kugusia kwa kifupi ubora au uchafu wa maji yaliyokusudiwa kwa matumizi ya kunywa.
Katika taaluma ya sayansi ya maji, ubora wa maji ya kunywa hutazamwa kwa kuzingatia sifa kuu tatu.
Sifa ya kwanza ni ile inayojulikana kwa kimombo kama 'Physical characteristics'. Katika kundi hili mambo yanayotazamwa katika maji ni harufu na ladha ya maji.
Sifa nyingine katika kundi hili la kwanza ni uchafu unaoonekana kwa macho ya kawaida (bila darubini n.k.). Sifa za kundi hili la kwanza huweza kujulikana kama hata na mtu ambae siyo mtaalamu wa mambo ya maji (Layman).
Sifa ya pili inayotumika ili kujua ubora wa maji ni ile ya kemikali. Kwa Kiingereza inaitwa 'Chemical charateristics'. Mambo yanayozingatiwa katika kundi hili ni vitu kama vile kemikali, sumu n.k.
Kemikali katika maji zinaweza kugawanywa katika makundi makubwa mawili, zile zinazohitajika mwilini (lakini kwa kiwango maalumu) na zile zisizohitajika kabisa.
Kemikali zinazohitajika mwilini na ambazo zimo katika maji ya chupa, mara nyingi huonyeshwa katika lebo inayobandikwa kwenye chupa. Mfano wa kemikali hizo kama vile Calcium, Magnesium, Sodium, Chloride, n.k.
Kama maji yana kiwango kikubwa cha kemikali za kundi la hapo juu zaidi ya kile kilichokubalika kitaalamu, yanaweza kudhuru afya ya mnywaji.
Kemikali zisizohitajika mwilini mara nyingi husababisha madhara makubwa kiafya na hata kifo kinaweza kutokea. Mfano wa kemikali za aina hiyo ni Arsenic, Cyanide, Lead, Mercury, Pesticides, Organophosphorus Compounds, n.k.
Ili maji yawe safi na salama kwa matumizi ya binadamu (hasa kunywa) lazima yawe na kiwango kidogo kabisa, kama haiwezekani kutokuwa kabisa na kemikali hizo katika maji.
Kemikali si rahisi kuziona kwa macho, bali huonekana kwa kutumia vifaa na utaalamu maalumu kwenye maabara.
Sifa ya tatu ambayo ni muhimu kupima ubora wa maji ya kunywa ni Biological Characteristics.
Ukizingatia ukubwa wa tatizo la uchafuzi wa maji (Water pollution) hasa katika nchi zinazoendelea kama vile Tanzania, sifa hii ya tatu (Biological characteristics) kwa umuhimu inazidi sifa ile ya kwanza na ile ya pili tulizoziona hapo awali.
Katika kundi hili la tatu sifa inayozingatiwa zaidi ni vijidudu visivyoweza kuonekana kwa macho ya kawaida. Kwa Kiingerza vijidudu hivi hujulikana kama Microorganisms.
Vijidudu katika maji hugawanya katika makundi makubwa mawili. Kundi la kwanza ni vile vinavyoweza kusababisha maradhi, na kundi la pili ni lile lisiloweza kusababisha maradhi.
Mfano wa vijidudu ambavyo si rahisi kusababisha maradhi ni Coliforms. Na vile vinavyoweza kusababisha maradhi ni kama vile Salmonella typhi (husababisha homa ya matumbo) na Vibrio cholerae (husababisha ugonjwa wa kipindupindu).
Kutokana na sababu za kiutaalamu na kiuchumi (umaskini) mara nyingi ubora wa maji hupimwa kutazama vijidudu vinavyoitwa Coliforms, kama wawakilishi (Indicators) wa vijidudu vile vya hatari (Salmonella, Vibrio, n.k.).
Utafiti wa hivi karibuni wa kisayansi umeonyesha kwamba, mara nyingine Indicators hawapo lakini vijidudu vya hatari vipo.
Kutokana na maarifa hayo mapya, watafiti wanapendekeza kuwa japo siku chache katika wiki ubora wa maji utazamwe pia kwa kuvichunguza vijidudu hatari (Salmonella, Vibrio, n.k.).
Ili maji yawe safi na salama kwa matumizi ya kunywa, lazima yasiwe na kijidudu cha hatari japo kimoja katika maji yenye ujazo wa mililita mia moja (100 mls). Hii ni kwa nchi karibu zote duniani, pamoja na Tanzania.
Kwa upande wa vijidudu vya Coliforms navyo havitakiwi kuwepo japo kimoja katika kila mililita mia moja (100 mls) ya maji ya kunywa.
Baada ya uchambuzi wa hapo juu ni wakati sasa unaofaa turudi katika hoja yetu ya awali, ambayo ni: Maji ya chupa aina ya "MASAFI" si masafi kwa matumizi ya binadamu; uchafu wake ni upi? Physical chemical or Biological?
Wataalamu wa maji, wafanyabiashara walioathirika pamoja na wananchi kwa ujumla wanasubiri majibu ya serikali ya mapinduzi ya Zanzibar.
Vinginevyo, wananchi watalazimika kuamini maneno ya 'mtaani' kuwa uamuzi huo ulikuwa na lengo la kuyadhoofisha maji ya "MASAFI" na kutoa soko bila ushindani kwa maji ya chupa aina ya Drop. Maneno hayo ya mtaani pia yana madai kuwa kampuni inayotengeneza maji hayo aina ya Drop inamilikiwa na watu kadhaa (wa ndani na nje ya Tanzania) akiwemo mtoto mmoja wa mzito mmoja wa serikali ya Zanzibar.
Eneo lingine ambalo nalo linazua maswali, ni uamuzi wenyewe ulivyochuliwa na serikali ukilinganisha na taarifa ya mkemia mkuu wa serikali.
Kama ilivyonukuliwa na vyombo vya habari, uamuzi wa serikali siyo kuyafungia maji ya chupa aina ya "MASAFI" kuingizwa Zanzibar (kama ilivyofanya kwa mifuko laini ya plastiki), bali imewatahadharisha wananchi wa Zanzibar.
Taarifa ya Mkemia Mkuu inasema maji si masafi kwa matumizi ya binadamu. Kwanini serikali haiyafungii maji hayo kama kweli si masafi. Au serikali inafanya mchezo na afya za Wazanzibari?
Kwa uchambuzi tuliuona tujaalie kuwa unatosha kwa serikali ili itazame upya kauli yake, na pia wananchi nao wachangie watakachokiweza.
Lakini pia, tukio hili liwe changamoto kwa wafanyabiashara wa Tanzania, bara na visiwani kuwa waongeze ubora wa bidhaa zao ili kama kweli kuna dosari ziondoke na afya za walaji zisiathirike.
Ili kufanikisha hilo, wafanyabiashara hasa za vyakula na vinywaji wawe na Maabara za kisasa na wataalamu wenye ujuzi wa kutosha kinyume na hivyo wataziona serikali zinawaonea.
--
|
|