Kuweka kali halali? (Sapoti)
Bismillahir naanza, kwa jina
lake jaalia,
Nataka kuwaeleza, yale yalotangulia,
Mwenzetu katueleza, Mungu
alomjalia,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Amri ni yake Mola, Jabiri
nakuambia,
Mola kaiharamisha, na Mtumewe
pia,
Laana wameahidiwa, wale
walokaidia,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Wanashangaza hakika, wale
wanaojisifia,
Eti wao wanataka, mume kumfurahisha,
Huku linaharibika, umbo
lao asilia,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Laana ikikupata, nani takusalimisha,
Faida utayopata, hakuna
wakumshirikisha,
Madonda utayapata, nani
atakuponesha,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Mola katutunukia, umbo linalopendeza,
Na nywele akatujalia, ili
kichwa kukijaza,
Wala hakutuambia, kali kuitumbukiza,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Hijab inawatoka, kali wanapojitia,
Kote kote watataka, kali
kujionyeshea,
Madhara yatawafikia, si
yakujijutia,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Mungu ametuambia, yale aliyokataza,
Naye akatuambia, sheria
zenye kuongoza,
Nakuweka pia, Mungu ametukataza,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Tamati natamatia, ujumbe
huu siku,
Jabiri kumsaidia, yale alohubiria,
Dini kuizingatia, kwa mujibu
wa sheria,
Kuweka kali haramu, kwa
amri yake Mola.
Fatma Saleh,
Kibasila Sec. School,
P.O. Box 20378,
Dar es Salaam.
Nuun, Walkalamu, sisitizo
maalum,
Nakumbusha ile damu, ilomwagwa
ki haramu,
Ni kina cha dhalimu, kuuwa
Islamu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Amani kweli ni tamu, tena
haitaki hamu,
Amani, dhuluma sumu, huifanya
isidumu,
Amani sitege bomu, itakua
ni adimu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Nasema kwa baragumu, nifike
Dar es Salaam,
Waikulu na Makamu, sikieni
mfahamu,
Kufukia majukumu, huo si
utalaamu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Kukumbusha kwa kalamu, malenga
yanilazimu,
Sera hii ni muhimu, dhuluma
iseje dumu,
Uhai wa binadamu, polisi
wa uheshimu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Mmepewa majukumu, siyo ya
kutudhulumu,
Msifanye kichwa ngumu, kupindisha
gurudumu,
Katiba muiheshimu, itengemae
kaumu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Raia kuwadhulumu, mwatega
nchini bomu,
Msije mkalaumu, Usama kumshutumu,
Mkae mkifahamu, wenyewe
metega bomu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Litakapo fumuka bomu, maisha
itagharimu,
Hatapona Muhashamu, wala
alo mkarimu,
Itakuwa ni karamu, yakutaja
marehemu,
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Yadola hii nidhamu, yapanda
mbegu yasumu,
Iweje siwe vigumu, kumwaga
za watu damu?
Tena yafanya karamu, kupongeza
udhalimu?
Wale walomwaga damu, wamefika
kwa hakimu?
Nuun chini kalamu, YOB jihadi
muhimu,
Nuun zangu salamu, Sabala,
Nolo jihimu,
Nuun letu jukumu, kutetea
Islamu,
Nuun Walkalamu, nimefika
kwenye qhatamu.
Yusuf A. Juma,
Dar es Salaam.
Tumejionea kweli, Bakwata
si taasisi,
Kwani hudhoofisha hali,
kwa dini kuwa nyepesi,
Yakiukwa maadili, Qur’ani
kuiasi,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Ni chombo cha serikali, Bakwata
si taasisi,
Tunayo mambo mawili, nukau
tukidadisi,
La kwanza Idd kusali, ingekuwa
Jumamosi,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Mauaji kikatili, Mwembechai
ni mkosi,
Haikutoa kauli, ama suala
kufosi,
Na wala kulijadili, lau
dua Ikhilasi,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Tulifanya muhimili, kama
chombo mkutasi,
Matatizo kukabili, kusimamia
kesi,
Tunafanya ujahili, kuyapongeza
maasi,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Bakwata ni chetu chombo,
kilichoshika hatamu,
Ingeshika yake fimbo, kutetea
Isilamu,
Ilishikilia tumbo, kuubwaga
Uislamu,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Chombo cha Waislamu, weupe
pia weusi,
Chakuongoza kaumu, twakipamba
na lebasi,
Sasa chageuka sumu, ni shetani
Ibilisi,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Lazima tujilaumu, kwa makundi
na vikosi,
Na tuchagueni timu, tupunguze
hii kasi,
Viondolewe haramu, vile
tunavyo vihisi,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Tuchunguzeni ujinga, baadhi
kutosubutu,
Bakwata walivyopanga, Idd
mfungo tatu,
Na hali tukielewa, hatufungi
siku mbili,
Bakwata si taasisi, ni chombo
cha serikali.
Kamati ya Wanawake wa
Kiislamu,
Tawi la Gongo la Mboto,
Dar es Salaam.
Habari zinasikika, kupitia
gazetini,
Wake kudai talaka, madai
mahakamani,
Hivi kweli tutafika, hasa
sisi waumini,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Mahakama kitwaghuti, kuamuwa
waumini,
Hamuoni tafauti, tunajitowa
Manani,
Wakati hautupiti, sasa tujikwamueni,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Ndoa zetu madhubuti, sheria
za vitabuni,
Amri hiyo thabiti, tangu
enzi za zamani,
Na ndani ya Taurati, imenenwa
usizini,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Wake kwenda kwa pilati, talaka
kuzibaini,
Huwa kwetu misibati, kama
sisi tuna dini,
Sawa wale Wagalatia, hawana
matumaini,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Nimefanya utafiti, sababu
zake ni duni,
Kama sale hawapati, wanaanzisha
uhuni,
Na ngoma ya benibati, ruhusa
mukiwahini,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Temeke na katikati, kwingine
kote nchini,
Kila mwenye hisabati, ndoa
kitu cha thamani,
Tuacheni usharati, mabalaa
hamuoni,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Sisi wanaharakati, sasa tukae
makini,
Dini iwe katikati, kwa sheria
hukumuni,
Tusipitwe na wakati, itakuwa
mtihani,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Hapa mimi ni tamati, enyi
wake waumini,
Mkae mjizatiti, ndoa zenu
heshimuni,
Na muzifatie shuruti, waume
zetu tiini,
Wake kudai talaka, sheria
au ubabe?
Zuberi Mohammed Mwinyi
(Amir),
S.L.P. 61428,
Dar es Salaam.
Leo nashika kalamu, ili niwaulizeni,
Munijibu Islamu, siwaulizeni
misheni,
Masheikh na Maimamu, talamidhi
darasani,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Mwafata Imamu gani, nawauliza
kaumu,
Au ni Mtume gani, hayo ameyahukumu,
Mubaini aya gani, kwenye
kitabu adhimu,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Siyo ninawalaumu, walosoma
Arabuni,
Bali nimepata hamu, nielewe
kwa makini,
Ni kauli ya Imamu, kufunga
swala shingoni,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Kugawanyika kaumu, kwa mote
Misikitini,
Kama hatuna elimu, jambo
hili kitu gani?
Mwisho tuende Jahimu, kwenye
nari abadan,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Selemani na Salimu, komesheni
ushindani,
Kwa barua hata simu, mueneze
mikoani,
Aliosema Karimu, humo kwenye
Qur’ani,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Kwa matangazo adhimu, yaliyotoka
zamani,
Kwa yeyote Islamu, swala
ifungwe tumboni,
Leo twaona jukumu, vipi
mwafunga shingoni?
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Yameanza humu humu, au nchi
za kigeni?
Ni kweli yana muhimu, ni
mbinu za Marekani,
Wao wameshika zamu, nia
yao farakani,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Kama yametoka Rumu, ni vizuri
mbaini,
Ikiwa Darisalaamu, au Pemba
mkoani,
Au ni Mombasa Lamu, ushahidi
elezeni,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Mimi si mwenda wazimu, nina
akili kichwani,
Kama nimewadhulumu, nawaomba
samahani,
Nia yangu ni elimu, Injili
na Kuruani,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
Kaditama ninazamu, nakwenda
zangu chuoni,
Nawangojea Ghulamu, walio
Bara na Pwani,
Wanijibu kielimu, yatulie
akilini,
Kufunga swala shingoni,
mwafata Imamu gani?
--
|
|