TUITION
 
Elimu ya Dini ya Kiislamu shule za Sekondari
 
Muundo wa Dola ya Kiislamu na uendeshaji wake
 

Kazi za Warasimu (Ulul-Amri)

Wenye mamlaka (Ulul-Amri) ndani ya dola ya Kiislamu ni wasimamizi wa utekelezaji wa maamrisho na makatazo ya Allah (s.w.), ambapo huiandaa jamii kuyapokea, kuyakubali, kuyatii na kuyatekeleza maamrisho hayo katika maisha yao ya kila siku. Utaratibu huu wa Urasimu wa dola ya Kiislamu unatofautiana na ule wa dola za kitwaghuti ambao huwafanya Warasimu kuwa waheshimiwa na watawala.

Utii kwa wenye mamlaka (Excutives) ndani ya dola ya Kiislamu hutanguliza sharti la wao kwanza (Ulul-Amri) kuwa watiifu kwa Allah (s.w.) na Mtume wake. Kinyume na hivyo, Qur'an ina maelekezo yafuatayo:

"Wala msitii amri za wale maasi, (wenye kupindukia mipaka ya Mungu)." "Ambao wanafanya uharibifu tu katika ardhi wala hawaitengenezi." (26:151-152)

Kazi za Mahakama

Wajibu wa Mahakama katika dola ya Kiislamu ni kufafanua, kusimamia na kuhakikisha hukumu na sheria za Allah zinatekelezwa ili kulinda haki; kuzuia maovu, ufisadi na dhulma katika jamii:

"Na tumekuteremshia Kitabu kwa (ajili ya kubainisha) haki, kinachosadikisha vitabu vilivyokuwa kabla yake, na kuvihukumia (kama haya ndiyo yaliyoharibiwa au ndiyo yaliyoasalimika). Basi wahukumu baina yao kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, wala usifuate matamanio yao kwa kuacha haki iliyokufikia. Na kila (uma) katika nyinyi (binadamu) tumeujaalia sharia yake na njia yake. Na kama Mwenyezi

Mungu angalitaka angekufanyeni kundi moja (la kufuata sharia moja),lakini anataka kukujaribuni kwa hayo aliyokupeni. Basi shindaneni kuyafikilia mambo ya kheri. Nyinyi nyote marudio yenu ni kwa Mwenyezi Mungu; naye atakwambieni (yote) yale mliyokuwa mkikhitilafiana." "Je, wao wanataka hukumu za Kijahili (ya zile siku za ujinga kabla ya kuletwa Mtume)? Na nani aliye mwema zaidi katika hukumu kuliko Mwenyezi Mungu; (yanafahamika haya) kwa watu wenye yakini." (5:50).

Kuhukumu kinyume na hukumu za Allah (s.w.) ni kueneza dhulma katika jamii. Ni kwa msingi huu Allah (s.w.) anatuasa:

"... Na wasio hukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu,basi hao ndio madhalimu". (5:45).

Uraia katika Dola ya Kiislamu

Dola ya Kiislamu ina raia wa aina mbili ndani ya mipaka yake:

(1) Waislamu (2) Dhimmi (wasiokuwa Waislamu)

Qur'an inatufahamisha kama ifuatavyo:

"Hakika wale walioamini na wakahama na wakapigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao, (Nao ni wale Muhajiri - Waislamu wa Makka). Na wale waliowapa (Muhajiri) mahala pa Mungu); hao ndio marafiki, wao kwa wao (katika kurithiana na mengineyo). Na wale walioamini, lakini hawakuhama, ninyi hamna haki ya kurithiana nao (wala ya mengineyo) hata kidogo mpaka wahame katika nchi ya kikafiri wake wakae nchi moja na nyinyi). Lakini wakiomba msaada kwenu katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipokuwa wao, (hapo msiwasaidie wao mkapigana na waitifaki wenu. Lakini jitahidini kupatanisha). Na Mwenyezi Mungu anayaona (yote) mnayoyatenda. (8:72).

Kutokana na aya hii, sifa za kustahiki uraia ndani ya Dola ya Kiislamu ni Uislamu na asili au uzawa ndani ya mipaka ya Dola Kiislamu.

Muislamu yoyote yule hata kama ni mhamiaji toka nje ya mipaka ya wakati fulani, ni raia anaetambulika na kukubalika na Dola bila ya kujali rangi, taifa au lugha yake. Dola ya Kiislamu inawatambua Waislamu wote kama ni raia zake na wote hao ni ndugu:

"Kwa hakika Waislamu wote ni ndugu; basi patanisheni baina ya ndugu zenu, na Mcheni Mwenyezi Mungu (msipuuze jambo la kupatanisha) ili mrehemewe." (49:10).

Kuhusiana na wale ambao si Waislamu lakini ni wazawa ndani ya mipaka ya Dola ya Kiislamu, uraia wao utatambuliwa iwapo wakubali kutii maamrisho ya Dola. Raia hawa watiifu kwa Dola katika sheria ya Kiislamu huitwa dhimmi hupata haki zote kama raia( Abul Al'a Maududi: First Principles of the Islamic State pg. 16)

Msonge wa Dola ya Kiislamu

Msonge wa Dola ya Kiislamu umebainishwa wazi katika Qur'an na kufasiriwa vyema na Mtume Muhammad (s.a.w) katika Dola ya Kiislamu aliyoiunda. Hebu turejee aya zifuatazo:

Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtiini Mtume na wenye mamlaka juu yenu walio katika nyie. Na kama mkihitilafiana juu ya jambo lolote basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume; ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hiyo ndiyo heri na ina matokeo bora kabisa.(4:59)

Katika aya hii tunajifunza kuwa aliye juu na anaestahiki kupewa utii wa kwanza au anayestahiki kupwekeshwa kwa utii ni Allah (s.w.), kisha hufuatia Mtume wake ndipo hufuatia viongozi wa jamii (Warasimu) wa ngazi mbalimbali. Viongozi hawa wa jamii, kwa mujibu wa aya hii, watastahiki kutiiwa tu pindi watakuwa ni Waislamu wanaoongoza kwa mujibu wa Qur'an na Sunnah.

Msonge wa uongozi katika Uislamu

Msonge wa uongozi katika jamii yoyote ya Kiislamu.

1. Allah (s.w.) (Qur'an)

2.Mtume (s.a.w.)(Sunnah)

3.Majlis Shura(Bunge)

4.Viongozi wa Jamii wa ngazi zote (Msonge wa uongozi utatiririka kuanzia Taifani hadi kwenye familia

5.Umma wa dola ya Kiislamu
 

Msonge wa uongozi katika Dola ya Kiislamu wakati wa Mtume

1. Allah (s.w.)

2. Mtume Muhammad (s.a.w.)

3.Shura ya (Sekretariat)(Mtume)

4. Viongozi wa Mikoa na viongozi wengine katika ngazi na nyanja mbali mbali.

5. Umma wa Kiislamu (wenye mchanganyiko wa Mayahudi, Wakristo na Washirikina)

(wenye mchanganyiko wa Waislamu na wasiokuwa Waislamu)


Somo la Fiqhi-Form IV:
 
 
Uchumi katika Uislamu
 

UTARATIBU wa maisha wa Kiislamu unamwongoza mtu kujenga na kudumisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu, uhusiano wake na vinavyomzunguka katika ulimwengu huu na uhusiano wake na wanadamu wenzake. Pia unaratibu na kutoa mwongozo katika kila eneo la maisha ya mwanadamu. Eneo mojawapo la maisha ya mwanadamu ni uchumi. Yaani uzalishaji, usambazaji na utumiaji wa mali na huduma.

Uislamu umelipa suala la uchumi nafasi muhimu, umeweka taratibu zinazohakikisha kuwa haki inatendeka kwa wote ili kuleta amani, utulivu na mshikamano wa kweli katika jamii. Katika kuuangalia uchumi wa Uislamu tutajihusisha na maeneo yafuatayo:

1. Nadharia ya uchumi wa Kiislamu

2. Umuhimu wa uchumi katika Uislamu

3. Kanuni za uchumi katika Uislamu

4. Sera ya uchumi wa Kiislamu

5. Uhuru wa kuchuma

6. Mgawanyo wa mali

7. Mfumo wa benki katika Jamii

8. Tatizo la Riba

9. Haki ya kuhalalisha na kuharamisha

1. Nadharia ya uchumi wa Kiislamu

Mfumo wa uchumi wa Kiislamu si fani inayochunguza mwenendo wa mambo ya kiuchumi na kujaribu kuona kanuni zinazoratibu uchumi japo kuna kukaribiana kwa kiasi fulani mawili hayo. Mfumo wa uchumi katika Uislamu ni utaratibu utokanao na Qur'an na sunnah juu ya uzalishaji, umilikaji, usambazaji, na utumiaji wa mali na huduma pamoja na miiko yake. Kwa msingi huo, uchumi huo umejengwa juu ya fikra ya ukati na kati (Iqtisaad), hivyo umetofautiana na mifumo mingine iliyobuniwa na watu.

Dhana (concept) ya Iqtisaad katika shughuli za kiuchumi ni kule kutoa uhuru kwa mtu binafsi (sekta binafsi) kuchuma na kumiliki mali ili iwe motisha kwake ya kuchapa kazi wakati huo huo serikali kusimamia, na kutoa miongozo katika uendeshaji na ugawaji, na vile vile serikali kuwa na sekta zake ili kila mwana jamii atoe mchango wake wa nguvu, ufundi na utaalamu na apate haki na mahitaji ya kimsingi. Mifumo iliyobuniwa na watu imeathiriwa na udhaifu wa kibinadamu wa kuelemea upande huu au ule.

Ipo mifumo ya kiuchumi kama vile ya uchumi huria (Anarchism), umwinyi, ukabaila, ubepari, usoshalisti, ukomunist na ufashisti. Ubepari kwa mfano umeelemea mno katika ubinafsi kiasi ambacho umepuuza kabisa haki za kijamii. Katika mfumo huu (ubepari) umma hauna chake; mali, huduma na shughuli mbalimbali hubinafsishwa. Wachache chini ya mfumo huu ndio hunufaika na rasilimali za Taifa. Hujilimbikizia mali, na motisha yao ya uzalishaji ni ile faida waipatayo. Serikali kuu chini ya mfumo huu wa kibepari hushirikiana na wachache hao waliohodhi mali, kunyonya walio wengi(Islamic Economics: Theory and practice(A comperative study) by M.A.Manna.

Pia, kuna mfumo wa uchumi wa Kikomunist au Kijamaa ambao nadharia yake imeelemea mno katika "usawa" wa sare kiasi cha kudhoofisha mno motisha ya watu binafsi na hivyo kupelekea kukosekana kwa ufanisi katika uzalishaji. Katika mfumo huu mali na shughuli mbalimbali hutaifishwa (toka milki ya watu binafsi kuwa milki ya taifa) . Ukweli ni kwamba huwa si mali ya taifa kama inavyotangazwa bali mbiu ya "usawa" na "mali ya uma", chini ya mfumo huu, ni mwavuli tu unaokinga kikundi cha watu(system) kilichojipa mamlaka ya uendeshaji wa nchi kwa sura ya chama au serikali ambapo wachache hunufaika zaidi na rasilimali za nchi. Humiliki na kutafuna mali kwa hila mbalimbali huku wananchi walio wengi (proletariat majority) wakiendelea kuvuja jasho la damu viwandani, maofisini, mashambani na kwenye makampuni na mashirika ya "umma", kwa ujira hafifu usioweza kukidhi mahitaji ya lazima. Hivyo hakuna usawa wowote ulio chini ya mfumo huu bali ni ule ule ubinafsi wa kuhodhi mali na madaraka ambao hubadilika toka kuwa wa watu binafsi kwenda kwa kikundi (system) fulani.

Tofauti kati ya mfumo wa uchumi wa Kiislamu na ile ya Kijahili

Zipo tofauti kuu tano kati ya mwelekeo wa kiuchumi wa Kiislamu na ile ya Kijahili. Tofauti hizi ni:

(1) Dhana ya mafanikio:

Katika mtazamo wa uchumi wa Uislamu mafanikio yanatazamwa kwa kuzingatia hatima ya ama mtu kupata radhi za Mwenyezi Mungu au kubeba laana ya Mwenyezi Mungu. Mafanikio hayapimwi kwa wingi wa mali. Katika uchumi wa Kijahili mafanikio maana yake ni mafanikio ya kiuchumi. Ni kiasi gani cha mali mtu amefanikiwa kukipata. Jinsi atakavyojilimbikizia mali ndivyo itakavyoonyesha "mafanikio" yake. Katika Uislamu kufuzu kwa kweli ni kupata radhi za Mwenyezi Mungu na kufeli kukubwa ni kule kukosa radhi hizo. Hivyo ili binadamu afanikiwe hana budi kuishi kwa uadilifu. Mtazamo huu unaathiri pia mizani yake ya wakati.Muislamu anapozitumia rasilimali zilizomo katika ardhi hafikirii tu mahitaji yake ya binafsi ya sasa bali pia matokeo ya vitendo vyake kwa vizazi vijavyo. Kwa mtazamo huu mtu anakuwa hana haki ya kufuja mali au rasilimali za ardhi, kwa vile anazingatia maslahi yake katika maisha haya, huko akhera na maslaha ya vizazi vijavyo.

Vile vile mafanikio katika Uislamu ni kule kulijua lengo la maisha hapa ulimwenguni, kuwa na kumbukizi ya kisimamo mbele ya Mola siku ya hesabu, kukinai moyoni na kukiona kila kitu cha ulimwengu huu kuwa ni cha kawaida. Kujitahidi kuyaendea mambo mema bila ya kuchelea chochote na kujiepusha na yale yote yanayoweza kukhasirisha katika maisha yajayo hata kama yana "manufaa" kwa mtazamo wa wengi katika maisha haya. Kujali shida na matatizo ya wengine na kuweza kutoa kuwasaidia wenye dhiki kwa kadiri ya wasaa. Kuwa na huruma, mapenzi na bashasha isiyobagua taifa, kabila, nasabu wala ukoo wa mtu. Kutokuwa na chuki, majivuno, kibri, utesi, usengenyi, ulimbukeni, kujiona, kujitukuza au kujidhalilisha na kujitweza kwa yeyote yule iwe kihali au kimali.

Aliyefanikiwa katika Uislamu ni yule ambaye neema yoyote aliyonayo haiwi kero na huzuni kwa wengine bali huitumia mwisho wa uwezo wake kuondoa Dhulma inayostawishwa na taratibu kinyume na Uislamu.

(2) Dhana ya mali:

Katika Uislamu mmiliki wa hakika wa mali ni Mwenyezi Mungu, mwanadamu kama Khalifa wa Allah hapa duniani anamiliki mali kwa dhamana tu siyo kwa hakika na kwa sababu hiyo ataulizwa jinsi alivyotumia hiyo mali. Pamoja na hivyo mali katika Uislamu si kitu kiovu bali kinachosisitizwa ni kuwa ichumwe na kutumiwa kwa kuzingatia maelekezo ya Mwenyezi Mungu. Kuhusu kutafuta mali Qur'an inatueleza kama ifuatavyo:

"Na utafute - kwa yale aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi mazuri ya akhera wala usisahau sehemu yako ya dunia" (28:77).

(3) Dhana ya bidhaa:

Katika uchumi wa kijahili kitu chochote chaweza kuwa ni bidhaa maadam kinaweza kutumiwa na mtu au mahali fulani. Kwa mfano pombe pamoja na madhara yake huitwa bidhaa kwa kuwa hutumiwa na baadhi ya watu.

Katika uchumi wa Kiislamu "bidhaa" huitwa ama "Atwayyibaati" au "Rizk". Atwayyibaat ni kitu kizuri, safi, Twahara . Rizk ni neema, au hidaya itokayo kwa Allah. Hivyo katika uchumi wa Kiislamu bidhaa ni vile vitu halali tu kwa mujibu wa sheria ya Kiislam. Kisichokuwa halali si bidhaa. Kwa mfano Pombe ni haramu hivyo si bidhaa.

(4) Dhana ya uadilifu katika utumiaji:

Kwa kuwa Allah ndiye muumba wa watu na rasilimali zote katika ulimwengu, sera ya uchumi ya Kiislamu haimpi mtu fursa ya kufuja mali apendavyo pamoja na uhalali atakaokuwa nao katika dhamana ya milki ya mali hiyo. Kinyume chake, katika uchumi wa Kijahili mtu anayo fursa kufuja mali apendavyo maadam ni mmiliki wa mali hiyo.

(5) Mizani ya wakati katika utumiaji:

Mtu anapofanya maamuzi yoyote hujiuliza nini matokeo au matazamio ya kitendo hiki au uamuzi huu baada ya saa moja au wiki moja au mwezi mmoja au mwaka mmoja au miaka mitano au kumi n.k. Kipimo cha wakati katika uchumi wa Kijahili na ule wa Kiislam ni tofauti. Katika ujahili mtu hujiuliza mali kiasi gani awe amepata atakapofikia umri fulani, kinyume chake Muislam anapofikiria jambo lolote, pamoja na masuala ya uchumi, kipimo chake cha wakati hukipa upeo mpana sana. Hujiuliza je, hiki kitendo ninachofanya kitakuwa na matokeo gani siyo tu kwa wiki hii au mwezi huu au mwaka huu au ujao bali kina matokeo gani siku ya kiyama.Muislamu anaamini kuwa ipo siku ya malipo na kwamba kuna pepo na moto.Watu watahesabiwa na kulipwa kwa mujibu wa matendo yao. Kila mtu binafsi atasimamishwa peke yake mbele ya Mwenyezi Mungu na kutoa hisabu yake. Imani hii ina athari kubwa kwa Muislamu na maamuzi yake anayochukuwa.

Itaendelea toleo lijalo

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook