JIFUNZE SHERIA
 
Uendeshaji wa Mashitaka - 6
 

Na Dkt. Abdallah J. Saffari
 

Wagonjwa wa Akili

Mtu yeyote ambaye anatenda kosa wakati akiwa ana maradhi ya akili ambayo humfanya asielewe analotenda au kuelewa kuwa kitendo hicho ni kibaya, hana hatia ya kosa hilo (F.12, Kanuni ya Adhabu, i.h.j). Kuna dhana kwamba kila mtu ana akili timamu mpaka pale itakapothibitishwa vinginevyo (Hata hivyo ithibati yenyewe sio lazima iwe kwa ushahidi unaothibitisha bila shaka yoyote ya maana. Itatosha iwapo mshitakiwa anayedai kuwa mgonjwa wa akili atathibitisha kuwa madai yake hayo huenda yakawa kweli kutokana na uwelekea wa ushahidi. Angalia Masiku v. R. 1975 L.R.T.. N.12, Ramadhani v. R. 1968 H.C.D. N. 340, Tendwa v. Uganda 1967 E.A. 102 na Onyango v Uganda 1967 E.A. 286). Wajibu wa ithibati hiyo imo mikononi mwa mshitakiwa mwenyewe (F.216(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Lakini ni dhahiri kuwa kuna baadhi ya vichaa ambao kwa muda mrefu huweza wasiweze kutafakari vizuri matendo yao. Watu kama hao wakishitakiwa huenda wasimudu kujitetea kuwa wana maradhi ya akili. Hivyo basi inakuwa ni wajibu wa watu wenye akili timamu kutoa taarifa ya hali hiyo mahakamani ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria. Mahakama yenyewe, kama tutakavyoona punde, yana dhima kuwa katika kuchunguza iwapo mshitakiwa ni mgonjwa wa akili au vipi.

Jambo la kwanza muhimu kuzingatia ni je, siku ambayo mshitakiwa anatakiwa kujibu mashitaka, anaweza kuelewa mwenendo wa kesi dhidi yake? Kama anaweza kuelewa kila linalozungumzwa pale mahakamani na hasa ushahidi unaotolewa basi kesi itaendelea kusikilizwa. Iwapo mwisho wa kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka mahakama yatamtaka mshitakiwa ajitetee, basi hapo ndipo mshitakiwa huyo anapoweza kudai na kuthibitisha kwa uwiano wa ushahidi, kuwa wakati alipokuwa akitenda kosa linalodaiwa alikuwa mgonjwa wa akili kwa mujibu wa sheria.

Hivyo basi mbali na mshitakiwa mwenyewe, mahakama yana wajibu wa kuhakikisha kuwa tuhuma yoyote kwamba mshitakiwa haelewi mwenendo wa mashitaka kutokana na maradhi ya akili, inaangaliwa kwa makini ili kuona kama ni kweli au la.

Kwa muhtasari utaratibu ambao unastahili kufuatwa katika hatua mbalimbali wakati wa kusikiliza shitaka dhidi ya mgonjwa wa akili ni kama ifuatavyo:

Kwanza, ikiwa wakati wa kusikiliza kesi dhidi ya mshitakiwa mahakama yanahisi kuwa mshitakiwa ana maradhi ya akili na kwamba hawezi kujitetea, bila kujali kuwa mshitakiwa huyo amejibu shitaka lake au la, mahakama yatasikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka kabla ya kuchunguza vizuri suala la akili za mshitakiwa (F.216(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Ikiwa mwisho wa ushahidi wa mashitaka mahakama yataona hakuna ushahidi wa kutosha kumtaka mshitakiwa kujitetea, yatamwachia huru (Sura ya 98, Sheria za Tanzania). Halafu yanaweza kumshughulikia mshitakiwa huyo kwa mujibu wa Sheria ya Maradhi ya Akili ambapo mshitakiwa anaweza kuwekwa chini ya ulinzi wa hospitali ya vichaa (K.h.j).

Lakini ikiwa mahakama yataona mshitakiwa anawajibika kujitetea basi yataamuru kwanza mshitakiwa achunguzwe na wataalamu wa maradhi ya akili (F.216(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Amri hiyo inaweza kumweka mshitakiwa huyo chini ya uchunguzi na ulinzi wa hospitali ya wagonjwa wa maradhi ya akili inayosika. Au mshitakiwa huyo anaweza akaachiwa kwa dhamana ili aende kufanyiwa uchunguzi wa akili yake kwenye hospitali ya maradhi hayo (I.H.J).

Katika muda wa siku arobaini tangu amri ya mahakama kumpeleka mshitakiwa katika hospitali ya vichaa kutolewa, Daktari wa maradhi ya akili katika hospitali hiyo atapeleka taarika kwenye mahakama yaliyotoa amri ya awali. Taarifa itaeleza iwapo mshitakiwa ana maradhi ya akili au la na iwapo anaweza kujitetea au la. Taarifa ya Daktari huyo itakuwa ni ushahidi kuhusiana na hali ya akili ya mshitakiwa ili muradi imetiwa saini ya Daktari huyo.

Ikiwa mahakama yataona kuwa kwa kutilia maanani taarifa hiyo ya Daktari wa maradhi ya akili, pamoja na ushahidi mwingine wowote ule uliopo, mshitakiwa ana maradhi ya akili, na kwamba hamudu kujitetea, yataandika hivyo katika kumbukumbu za mwenendo wa shauri hilo, yataahirisha tena shauri dhidi ya mshitakiwa kisha yataamuru mshitakiwa huyo awekwe chini ya ulinzi, mahali na kwa namna ambayo yanafikiri inastahili (F.216(60) Sheria ya Mwenendo wa Jinai. i.h.j). Kumbukumbu au nakala ya amri hiyo ya mahakama itapelekwa kwa Waziri wa Sheria. Waziri atachunguza kumbukumbu hiyo ya mahakama na kuyaamuru mahakama hayo yatoe amri ya kumweka mshitakiwa huyo kama kichaa mkosaji katika hospitali ya maradhi ya akili au mahali pengine popote panapofaa. Mahakama yatatoa amri hiyo.

Bali iwapo taarifa ya Daktari wa maradhi ya akili itaeleza kwamba mshitakiwa ana akili timamu na kwamba anaweza kujitetea, mahakama yataendelea kusikiliza shauri dhidi ya mshitakiwa na kumtaka kujitetea, kama inastahili (F.216(1), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Endapo mshitakiwa aliyewekwa chini ya ulinzi anapona maradhi ya akili kiasi cha kuweza kujitetea, Daktari wa maradhi hayo atapeleka taarifa yake kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai kumfahamisha kuwa, kama sio kosa analokabiliwa nalo, mshitakiwa alistahili kuachiwa huru bila masharti yoyote (F.217(3), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Baada ya kupokea taarifa ya Daktari, Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai atayaeleza mahakama yaliyokuwa yanasikiliza shauri dhidi ya mshitakiwa iwapo ana nia ya kuendelea na mashitaka dhidi ya mshitakiwa huyo au vipi. Kama Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai ataelezea nia yake ya kuendelea na mashitaka dhidi ya mshitakiwa, mahakama yatatoa amri mshitakiwa afikishwe mahakamani kutoka kule alikowekwa ili kuendelea na mashitaka dhidi yake (I.h.J).

Ikiwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai ataeleza kuwa hakusudii tena kuendela na mashitaka dhidi ya mshitakiwa basi mahakama yanapoendelea kusikiliza shauri dhidi ya mshitakiwa basi mahakam yatamwachia huru mshitakiwa bila ya masharti yoyote yale. Mshitakiwa anayeachiliwa huru atashughulikiwa kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Maradhi ya Akili (I.h.J).

Kuachiwa huru kwa mshitakiwa kwa mujibu wa masharti hayo sio kizuizi cha kufungua mashitaka dhidi yake (F.217(5), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Wakati mahakama yanapoendelea kusikiliza shauri dhidi ya mshitakiwa yanaweza kuanza upya au kuendelea na pale yalipoachia kabla uchunguzi wa akili mintaarafu ya mshitakiwa kuanza (218 (2), Sheria na Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Lakini ikiwa mshitakiwa anaonekana hana akili timamu wakati wa uchunguzi wa awali, mahakama yataendelea na uchunguzi huo wa awali na kuipeleka kesi ya mshitakiwa kusikilizwa mahakama kuu.

Ikiwa kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani, uwe umetokana na uchunguzi wa mahakama au mshitakiwa mwenyewe, itaonekana kuwa wakati wa kosa linalodaiwa mshitakiwa alikuwa na maradhi ya akili kwa mujibu wa sheria basi yatamuona mshitakiwa hana hatia ingawa ametenda kosa aliloshitakiwa (F.219(2), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Viziwi-Bubu

Mabubu wengi huwa hawasikii kabisa. Athari hizo mbili, kutosema na kusikia hufanya vigumu kuweza kuelewa mwenendo wa mashitaka dhidi yao.

Wakati mahakama yanataka kuanza kusikiliza shauri dhidi ya kiziwi - bubu lazima yajiulize iwapo kiziwi-bubu huyo anaweza kuelewa mwenendo wa shitaka hilo. Jawabu na mwongozo sahihi kuhusiana na suala hili ulitolewa katika shauri la R. v. Bubu (1959) E.A. 1094) kwa maneno yafuatayo: "...kwanza lazima Hakimu aamue iwapo mshitakiwa kiziwi - bubu anaelewa mwenendo wa mashitaka dhidi yake au la. Kuelewa mwenendo wa mashitaka ni kuelewa kiasi kikubwa cha mashitaka hayo".

Halafu mahakama hayo yalielezea namna ambavyo kiziwi-bubu anaweza kueleweshwa mwenendo wa shauri dhidi yake; ya kuwa:

"Kiziwi-bubu anaweza kueleweshwa mwenendo wa mashitaka dhidi yake ikiwa anajua kusoma na kuandika au iwapo anaweza kuwasiliana kwa lugha ya ishara. Na kwa madhumuni ya mawasiliano ya lugha ya ishara ndugu au rafiki aliyeapishwa rasmi anaweza kuajiriwa kuwa mkalimani ikiwa Hakimu ataona kwamba mshitakiwa huyo anaweza kueleweshwa au kutafsiriwa maelezo yote".

Lakini ikiwa mshitakiwa hawezi kuelewa mwenendo wa mashitaka dhidi yake mahakama yatasikiliza ushahidi dhidi yake, na kama mshitakiwa ametakiwa kujibu mashitaka hayo, mahakama hayo yatasikiliza pia ushahidi wake. Kama ushahidi uo haukuthibitisha mashitaka dhidi ya mshitakiwa, yatamwachia huru. Bali iwapo yatamwona ana hatia yatapitisha uamuzi huo na kuamuru mshitakiwa awekwe kizuizini kwa ridhaa ya Rais (F.221(1)(a), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j)

Utaratibu huo wa juu aidha utafuatwa na Makama Kuu iwapo mshitakiwa kiziwi-bubu amepelekwa mbele ya mahakama hayo ili shauri lake lisikilizwe F.217(1)(b), Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Kuitwa kujitetea

Baada ya kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka mahakama yatamtaka mshitakiwa ajitetee ikiwa yanaona uko ushahidi wa kutosha dhidi yake (F.231, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j). Aghalabu inasema: Mshitakiwa ana kesi ya kujibu. Lakini iwapo mahakama yataona hakuna ushahidi wa kutosha dhidi ya mshitakiwa kumtaka ajitetee, yatamwachia huru. Kuachiwa huru huko ni kizuizi cha mashitaka tena dhidi ya mshitakiwa mintaarafu ya kosa hilo kwa maelezo yale yale.

Kutokana na hali hiyo basi daima upande wa mashitaka na utetezi husubiri kwa hamu uamuzi wa mahakama iwapo mshitakiwa atatakiwa kujitetea au sio. Aghalabu mawakili wa utetezi huhutubia mahakama katika hatua hiyo kudai na kuyataka yatoe uamuzi kuwa mshitakiwa hana kesi ya kujibu. Jambo hili limeleta mgogoro na mjadala mkali miongoni mwa mawakili na wanasheria wengine. Katika Bhatt v. R (1957) E.A. 332. Angalia pia F.230, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j) mahakama yalisema kuwa: "Inaweza kuwa vigumu kuelewa maana ya 'kesi ya kujibu', lakini kwa uchache ni ile ambayo mahakama yanayozingatia vizuri sheria na ushahidi uliotolewa yangeweza kumtia hatiani mshitakiwa kama hakujitetea (K.h.j).

Katika kuamua kama mshitakiwa anayo kesi ya kujibu au vipi mahakama haiangalii tu lile kosa ambalo mshitakiwa ameshitakiwa nalo. Huenda ushahidi uliotolewa usionyeshe kuwa mshitakiwa ana kesi ya kujibu mintaarafu ya kosa hilo pekee lakini anahusika na kosa jingine. Tuseme awali alikuwa ameshitakiwa kwa kosa la wizi wa kutumia nguvu. Ushahidi unaweza usidhihirishe kosa hilo kiasi cha kumtaka mshitakiwa ajitetee. Lakini ushahidi huo huo unaweza kudhihirisha kosa la wizi wa kawaida au shambulizi la kimwili. Kama ni hivyo basi mahakama humtaka mshitakiwa ajitetee mintaarafu ya mashitaka hayo madogo ingawa awali hakushtakiwa nayo rasmi (F.231(1) na 300, Sheria ya Mwenendo wa Jinai, i.h.j).

Kwa ujumla uamuzi iwapo mshitakiwa ana kesi ya kujibu au la ni lazima uchukuliwe kwa tahadhari sana hasa kwa vile mshitakiwa akiachiwa huru kutokana na uamuzi huo hataweza tena kushitakiwa kwa kosa hilo hilo kama ilivyokwisha elezwa.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook