TAHARIRI

.

Damu haimwagiki bure bure bila ya haki
 

KATIKA moja ya maswali ambayo polisi wamekuwa wakiwauliza watu wanaotuhumiwa kusambaza au kuonyesha kanda za mauaji ya Mwembechai ni pamoja na kuhoji "mnaonyesha ili iwe nini".

Aidha, baadhi ya askari wamekuwa wakijenga hoja kwamba kuonyeshwa kwa kanda hiyo kutachochea chuki baina ya wananachi na serikali yao.

Lilipotuka tukio la Mwembechai serikali ilijitahidi sana kutoa maelezo juu ya kilichokuwa kinatokea (kwa mtizamo wake) na uhalali wa vyombo vya dola kuchukua hatua vilivyochukua.

Haikuishia hapo lakini ikazipongeza hatua hizo baada ya watu kuuliwa. Na hata Waislamu walipodai iundwe tume huru ya uchunguzi baadhi ya viongozi wa serikali walidai kwamba hakuna haja kwani kila kitu kipo wazi.

Uwazi huo ndio leo watu wanauonyesha katika kanda. Kwa hiyo "mnaonyesha ili iwe nini" ili wananchi waone huyo mazingira yaliyolazimisha polisi wamwage damu ya Waislamu na wastahiki kupongezwa na chama tawala CCM.

Na kiongozi mmoja wa serikali aliwahi kusema kwamba polisi wao sio mbwa (wapopolewe mawe tu wasijibu mashambulizi). Mkanda huo basi unaonyeshwa ili kuona hayo mawe yalivyo katika mizani sawa na risasi za moto.

Moja ya sera muhimu za serikali ya Mh. Rais Benjamin William Mkapa ni ukweli na uwazi. Tunadhani ni kuihujumu sera hii ya Mh. Rais kwa vyombo vya dola kuwabughudhi watu wanaoeleza kwa ukweli na uwazi tukio la Mwembechai.

Kama ilichofanya polisi ilikuwa sahihi kwanini leo ione vibaya na jambo la hatari tukio hilo kuonyeshwa hadharani, wakati tangu hapo ilishapongezwa!

Polisi walishatetewa kwamba wao si mbwa na kwamba walikuwa wakipambana na maadui wa amani na usalama wa Taifa letu, kwanini wasione wamesaidiwa kwa maadui hao kuonyeshwa hadharani na jinsi walivyokuwa wamewakaba polisi!

Kuonyeshwa kwa kanda ya mauaji ya Mwembechai hakuchochei chuki dhidi ya serikali bali matendo ya serikali yenyewe dhidi ya wananchi.

Na kuchangia kuwabughudhi wanaoonyesha kanda hizo hakutosaidia kitu. Kwa mujibu wa taarifa za baadhi ya vyombo vya habari kanda hizo zipo London, Washington, Nairobi, Mombasa, Kanyigo, Nanyamba, Masaka na kwingineko duniani.

Muhimu hapa ni kuangalia haki, sheria na katiba ya nchi vinasema nini juu ya tukio hilo. Kinyume cha hivyo tukae tukijua damu haimwagiki bure bure bila ya haki. 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook