Na Mtoa hoja
SI kila afanye uchokozi ahesabike kuwa ni mtu mbaya asiyeitakia mema jamii. Uzuri ama ubaya wa uchokozi unategemea aina ya uchokozi utakaofanywa pamoja na malengo ya uchokozi huo. Ikiwa unafanywa uchokozi wa kulichochea bongo la mtu kwa lengo la kulifanya bongo hilo lifikiri kimantiki na kuliwezesha kujenga hoja zenyewe zinazokubalika mbele ya watu wenye fikra zilizopevuka utakuwa ni uchokozi halali. Ni uzuri ikiwa utafanikiwa kulichokoa chokoa bongo la mtu likaweza kuzing'amua hoja zenye mashiko kutoka katika hoja lemavu zinazotolewa na watu wa aina mbalimbali katika maisha yetu.
KILA mtu aliyemkamilifu kwa maana ya ubinadamu na asiye kuwa na matatizo ya kiakili, basi atakuwa anao uwezo wa kufikiri kimantiki endapo atachokozwa. Kufikiri namna ya kujenga hoja zenye nguvu katika kufikiria ni jambo muhimu sana katika kuonyesha upevu watu katika kuyatazama na kuyachambua mambo.
Pamoja na kuweza kufikiri kimantiki bado hakumaanishi kuwa mtu anaweza kuzichambua hoja na kubainisha udhaifu wa hoja hizo, vile vile hawezi kujenga hoja katika misingi imara isiyotetereka bila ya kuwepo na uchokozi kwanza. Mathalan mtu ambaye si mgonjwa anao uwezo wa kupiga 'push-up' kumi au zaidi, lakini kama hakupatikana mtu wa kumchokoza kimazoezi katu uwezo huo hautaonekana kimatendo.
Vivyo hivyo, akili za watu wengi kama siyo wote, hazitumiki kuyatafakari mambo kwa kuzama kimantiki. Katika hali hii kumejitokeza umuhimu wa kuwepo kwa wachokozi ili kuvichokoachokoa vichwa vya watu viweze kuyatazama mambo upya kwa kutumia jicho la ndani zaidi.
Kuna msemo usemao kuwa watu waliokomaa kifikra ni wale wanaojadili hoja wala sio kumjadili mtoa hoja. Na katika ufinyu wa hoja ni kujiegemeza katika msingi wa fulani kasema au kafanya bila ya kuangalia ukweli wa kitu kinachofanywa au kusemwa. Ikiwa mtu ataegemeza hoja yake katika msingi wa kilichosemwa au kufanywa na kiongozi, akaacha kuishughulisha akili yake katika kuchambua umadhubuti wa hoja inayohalalisha kile kinachofanywa au kusemwa, bila shaka atakuwa amejining'iniza kwenye nyumba ya buibui.
Kwa kuwa watu wengi wamejenga utamaduni wa kufuata mambo kibubusa kwa sababu tu yamesemwa na viongozi, mafisadi wanaitumia vyema fursa hii kwa kuziingiza sera za kuiharibu jamii kupitia migongo ya viongozi. Wanachofanya ni kumkatia fungu ili auhalilishe mradi. Basi hapo usishangae unapowakuta watu wamejaza makondom kwenye mifuko na kuwagawia watoto wa shule eti kwa sababu viongozi wenyewe wanatangaza na kuzigombania katika mgao.
Akiwa katika harakati za kuwalingania wamtambue Muumba, Nabii Ibrahimu (a.s.) alizua chokochoko ya kuzichokoa akili zilizofubaa kutokana na ukungu wa Shirk uliotanda kwenye bongo za watu wa jamii yake. Nabii Ibrahimu alifanya uchokozi mkubwa ulizozisugua akili zilizolala mpaka zikatoka usingizini.
Alikaa nao na kuanza kuzivuta fikra zao kidogo kidogo ili ziamke na kufikiri kimantiki. Na usiku ulipoingia, Nabii Ibrahimu aliona nyota, hapo akawaambia watu wake kuwa: "Nyota hii ndiyo Mungu wangu". Nyota ile ilipopotea wakati kulipokucha akawaambia kuwa"sipendi miungu wanaopotea".
Na usiku wa pili alipouona mwezi unachomoza, Nabii Ibrahimu alisema kuwaambia watu wake kuwa: "Mwezi huu ndiyo mungu wangu". Ulipotua akasema: "Asiponiongoza Mola watu, bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu waliopotea".
Na siku ya tatu alipoliona jua linachomoza, akawaambia watu wake kuwa: Huyu ndiye mungu mkubwa kabisa". Lilipotua akasema: "Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayomshirikisha nayo Mwenyezi Mungu. Mimi ninauelekeza uso wangu kwa yule aliyeumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimeacha dini zote za upotevu".
Kimantiki, Nabii Ibrahimu aliijenga hoja yake katika misingi (premises) mikuu mitatu madhubuti kabla hajatoa hitimisho la uchokozi wake. Lakini pamoja na hoja yenye mashiko aliyoitoa bado vichwa vya watu vilikuwa vizito sana katika kufikiria umadhubuti wa hoja aliyoibuka nayo Ibrahimu.
Badala ya wao kuijadili hoja iliyotolewa na kuonyesha udhaifu wake kwa kutumia misingi iliyotumika, walimwandama Nabii Ibrahimu kwa kumshutumu kuwa anakwenda kinyume na utaratibu uliozoeleka ambao ni wa tangu zama za mababu zake.
Kama nilivyosema awali kuwa ikiwa utafanikiwa kuzichokoa bongo za watu hata zikaweza kujenga hoja zenye nguvu katika kukataa au kukubali jambo, basi utakuwa umefanya uchokozi wenye manufaa makubwa. Ni uchokozi mzuri kwa kuwa unafutilia mbali ububusa na kuwawezesha watu kukubliana na kuyafuata mambo kisomi.
Akiwa na azma yake ile ile Ibrahimu (a.s.) akauendeleza uchokozi wake. Safari hii akaachana na nadharia, alichokifanya ni kuziingiza nadharia kimantiki katika vitendo. Akachukua shoka na kuyavunjavunja masanamu yote yaliyokuwa yakiabudiwa isipokuwa moja. Kisha akaliweka shoka katika mikono ya sanamu kubwa. Hii ni misingi miwili (premises) ya hoja anayotaka kuijenga Ibrahimu (s.a.) dhidi ya ububusa.
Uchokozi ukawa umeiva na akili za watu wake zikaanza kuitikia kimantiki. Mambo yakawa hivi! "Wakasema: "Ni nani aliyefanya hivi miungu yetu? Hakika huyo yu miongoni mwa madhalimu". Jibu likawa: "Tulimsikia kijana mmoja akiwataja vibaya anayeitwa Ibrahimu". Wakasema: "Mleteni mbele ya macho ya watu ili wamshuhudie kwa ubaya wake".
Ibrahimu (a.s.) akawekwa kwenye malumbano ya hoja yakaanza kuchukua nafasi. Wakasema: "Je! Wewe ndiye umeifanya hivi miungu yetu, ee Ibrahimu?' "Hapana, bali ameyafanya haya huyu mkubwa wao, basi mwulizeni na waulizeni hawa waliovunjwa kama wanaweza kusema". Hapa Ibrahimu (a.s.) akaweka msingi wa tatu wa hoja atakayoitoa.
Alipowatwanga kwa hilo swali, watu wake wakajirudi nafsi zao na kuanza kufikiria kimantiki kwa kujenga hoja za ndani kwa ndani mpaka wakagundua udhaifu wa misingi ya imani yao. Wakaibuka na hitimisho lililowasuta wao wenyewe. Kwa hakika ninyi mlikuwa madhalimu wa nafsi zenu.
Kutokana na misingi mitatu madhubuti aliyoiweka Ibrahimu, watu wake wakainamisha vichwa vyao na kuukiri ukweli uliojidhihirisha akili mwao. Wakasema kumwambia Ibrahimu (s.a.) "Hakika umekwisha jua kuwa hawasemi". Hapo Ibrahim akaisimamisha hoja iliyowakinaisha watu wake. Akasema. "Je! Mnaabudu badala ya Mwenyezi Mungu miungu isiyo kufaeni chochote wala kukudhuruni. Akili zenu zimedumazwa kiasi hicho?
Kwa kweli Waislamu tumekuwa wafuataji wazuri wa nyayo za Nabii Ibrahimu (a.s.). Kama vile Ibrahimu (a.s.) alivyojenga hoja kuonyesha dhulma iliyoshamiri kupitia mfumo wa maisha wa kishirikina, ndivyo hivyo hivyo Waislamu nchini tumekuwa tukijenga hoja kuonyesha dhulma inayotendwa dhidi yetu.
Uchokozi mbaya sio wa kimantiki uliozushwana Paroko Camillus Lwambano mnamo Februari 8, 1998 ni ushahidi tosha unaothibitisha kuwa ipo dhulma ya wazi dhidi ya Waislamu. Kwa kutumia hoja lemavu iliyojengwa kwenye misingi butu, akadai kuwa amepita katika baadhi ya Misikiti na kusikia kuwa eti Yesu (a.s.) anatukanwa sana. Akaishinikiza serikali kwa kuishutumu kuwa imeshindwa kuidhibiti mihadhara aliyoidai kuwa ni ya kashfa.
Mnakumbuka msemo usemao kuwa watu waliopevuka kifikra ni wale wanaoijadili hoja (great mind discuss ideas). Hakuna jitihada zozote zilizofanywa kujadili kama kuna ukweli katika maneno ya Paroko ikaaminika tu "kichwa kichwa" kuwa maadamu kauli imetoka kinywani mwa Paroko basi haina mushkeli. Ulemavu wa hoja ya fulani kasema ukawasukuma wenye nyadhifa zao katika utendaji.
Kwa hoja ya fulani kasema ikamnyanyua mtu kwenye kiti alichokabidhiwa kwa niaba ya wananchi. Rasmi mnamo Februari 9, 1998 akatangaza kuomba radhi na kuahidi kuchukua hatua.
"Nachukua nafasi hii kuwaomba radhi waumini na wanachi wote ambao kwa namna moja au nyingine wameumizwa na jambo hili. Nawahakikishia tatizo hili litakwisha. Naomba mvumilie, mniamini na mnipe muda".
Kilichofuatia kukamatwa kwa Masheikh na vijana wa Kiislamu wakifuatwa majumbani kwao na Misikitini. Ukavunjwa Msikiti na kuwashambulia kwa mabomu watu waliomo ndani yake. Na kikomo cha yote haya yaliyofanyika kwa kuegemea hoja ya fulani kasema ni yale mauaji ya kinyama ya Februari 13, 1998 pale Mwembechai.
Kuwepo kwa nyota, mwezi na jua pamoja na namna ya utendaji kazi wa vitu hivyo ni premisia (premises) zinazoisimamisha hoja madhubuti ya kuwepo kwa Muumba wa ulimwengu asiyekuwa na mshirika. Kadhalika kauli ya Paroko, hatua alizozichukua Bwana Makamba, kuuawa kwa Waislamu na ukimya uliopigwa na Mhe. Rais ni 'premisia' halisi zinazothibitisha kuwepo kwa agenda malaum dhidi ya Waislamu inayotekelezwa na viongozi wa serikali ya chama tawala kinyume cha katiba na sheria za nchi.
Waislamu wamekwisha iwasilisha hoja yao Ikulu kwamba utendaji wa serikali ya chama tawala unadhihirisha ukweli wa kuwepo kwa mpango mahususi dhidi yao na mtiririko wa matukio yaliyohitimishwa kwa umwagaji wa damu za Waislamu wa makusudi pale mwembechai ni premisia zinazoisimamisha hoja na kuifanya isivunjwe kwa namna yoyote iwayo.
Hali inayoendelea inaonyesha kuwa hoja wanayoitoa Waislamu bado imekuwa ni nadharia ya kimantiki isiyo wawezesha wahusika kuitazama dhulma wanayoifanya jinsi inavyowasha moto karibu ya mapipa yaliyojaa petroli yaliyo ndani ya nyumba. Kama hivi sivyo basi huu ukimya unaoendelea, kamatakamata na harakati za kumsaka Sheikh Ponda tafsiri yake sahihi ni ipi?
Mwenzetu Ibrahimu (a.s.) aliingiza mantiki katika matendo pindi alipoona kuwa akili za madhalimu hazichokozeki kiasi cha kuwawezesha kuyachanganua mambo kimantiki. Alijitwisha shoka lake na kuyaendea masanamu. Hapo alijulikana kuwa yupo na anastahiki kuitwa ili aonyeshe kiini cha matatizo.
Je! Sisi tutaitumiaje hii sehemu ya pili ya mantiki iliyokokotezwa na kigezo chetu Nabii Ibrahimu (a.s.)? Tuingie kwa kura ya pamoja ili tutambulike kuwa kuna binadamu, wananchi Waislamu wanaostahiki haki? Sijuwi!
Fikra zilizokomaa zinajadili umadhubuti wa hoja iliyotolewa, na ulemavu wa hoja ni kujiegemeza katika msingi wa fulani kasema au kafanya, bila kuangalia ukweli na uimara wa misingi (premises) inayotumika katika kuhalalisha.
--
|
|