Makala
 
 
Serikali ilinde amani ya kweli
 

Na Mwandishi Wetu
 

HISIA za hofu ya kujitokeza uhasama wa kidini hapa nchini zilianza kujitokeza dhahiri katika utawala wa awamu ya pili. Tunaweza kusema hisia hizo zilitokana na mabadiliko ya uongozi wa juu wa nchi kutoka Rais Mkristo Mwalimu Nyerere na kuja Rais Muislamu Ali Hassan Mwinyi.

Inawezekana yale mazoea ya kuwa na kiongozi Mkristo tangu kupatikana kwa uhuru wa nchi hii yalijenga kujiamini zaidi kwa watu wa dhehebu fulani na hivyo kusababisha hisia na hofu pale kiongozi alipobadilika na kuwa Muislamu.

Lakini kuna walioshuku kuwa kwa sababu ya hisia hii ya hofu ni kuwepo kwa ukweli kuwa katika awamu ya kwanza hapakuwa na uwiano ulio sawa na wa haki kati ya Waislamu na Wakristo ambapo Wakristo walikuwa na nafasi zaidi na kuwazidi Waislamu katika nyanja mbalimbali kielimu na kimaendeleo, japokuwa idadi ya Waislamu na Wakristo wa nchi hii inakaribiana na japokuwa watu wa dini fulani walishiriki kikamilifu kudai uhuru kutoka kwa wakoloni.

Yapo madai kwa Waislamu wengi kuwa pamoja na kutokuwepo kwa uwiano huo uongozi wa awamu ya kwanza uliwafanya Waislamu kubaki vipofu na mabubu. Hivyo ilionekana kwamba utawala wa awamu ya pili ambao ulikuwa na kiongozi Muislamu ungeweza kuleta mabadiliko yatakayowawezesha Waislamu kupata nafasi sawa na Wakristo.

Hisia hizi za hofu zilijidhihirisha kutokana na malalamiko mengi yaliyojitokeza kuwa utawala wa awamu ya pili ulikuwa na udini na maneno kama "tulinde amani yetu... tujifunze kutoka Burundi na Somalia" ndipo yalipoanza kutawala kwenye majukwaa ya kisiasa na baadhi ya vyombo vya habari.

Kwa vile lawama nyingi hazikuwa na msingi wa haki ni wazi kuwa zilitolewa nguvu kwa lengo la kuutia hofu utawala huo ili usitimize kile ambacho ni wajibu wake kwa Waislamu kama raia wenye haki sawa na wengine.

Pamoja na Waislamu kuzindukana na kulalamika kuwa wanakandamizwa pamejengwa hoja ya kisayansi ya kurudisha mapigo kwa Waislamu kwamba madai ya Waislamu ni ya kuleta udini na uchochezi hivyo kufanywa hayana msingi.

Uzoefu umetuonyesha kuwa zile harakati za Waislamu kudai kile wanachokiona ni haki kwao huchukuliwa kama uchochezi unaoweza kuhatarisha amani na tayari baadhi ya Waislamu wameshapachikwa majina kama vile "Mujahidina" wanaotumiwa kuleta machafuko, "siasa kali" na mengineyo kwa lengo la kupotosha jitihada zao.

Lakini kinachochachafya zaidi ni kuwa kuna shutuma zinazotolewa na watu wasiouelewa Uislamu vilivyo ambazo ni kinyume na ukweli. Maneno yanasikika kwamba eti Waislamu hawapendi kuwaona watu wasio Waislamu na huwaita makafiri. Kwamba Waislamu wanatamani nchi hii siku moja iwe Jamhuri ya Kiislamu. Kwamba harakati za Waislamu ni za kutaka kuleta vita vya kidini kwa vile Muislamu akiuawa huamini kuwa kafa shahidi na madai mengine mengi ya aina hiyo.

Ninachotaka kusisitiza hapa ni kuwa Uislamu si dini ya vita. Kama lilivyo jina Islamu, Uislamu maana yake ni utii, amani na kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu wa Haki. Ni kweli kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.) ambaye ndiye kiigizo kikuu kwa Waislamu alipigana vita kwa ajili ya Uislamu. Lakini hii haimaanishi kuwa Waislamu ni watu wa vita. Mtume (s.a.w.) alipigana vita kwa kuamrishwa na Mola ili kuuhami Uislamu baada ya Waislamu kuteswa na kunyanyaswa.

Mbali na hayo upo ushahidi wa Hadithi kuwa Mtume (s.a.w.) alikaa na watu wasio Waislamu katika miji bila kutokea tafrani yoyote. Na wala si kweli kuwa Muislamu hutamani umwagaji wa damu bila haki kwa vile akiuawa atakufa shahidi.

Kwa kweli hizi ni shutuma zinazolenga kupotosha ukweli na maana ya harakati za Waislamu ikiwa ni pamoja na kuviza madai ya Waisalmu na kusababisha hisia za hofu isiyo na sababu kwamba siku moja nch hii itageuka Burundi au Somalia.

Watanzania sote huku tukithamini dini zetu ni wapenda amani lakini amani hii tunayoihubiri usiku na mchana itakuwa na maana iwapo hapatakuwa an nung'unung'u wala malalamiko miongoni mwa wananchi.

Wakati serikali ikisisitiza hili neno 'amani' ni vyema ikachukua kila hatua kuhakikisha kuwa amani ya kweli inapatikana kwa kukisikiliza kile wanacholalamika Waislamu. Mungu aibariki Tanzania.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook