Uchambuzi/hoja binafsi
 
Je, Yehova na Allah ni miungu tofauti ? - 9
 

Na Muhibu Said
 

KATIKA toleo lililopita, tuliona jinsi Biblia tukufu ikimdhihirisha wazi mungu-mtu anayeabudiwa na Wakristo. Kwa muktadha huo, tuliona jinsi muasisi wa dini ya Kikristo, Bwana Paulo alivyoibadilisha majina "miungu-Zeu" na "Herme" ya wapagani na kuiita "Yesu" kwa kuhubiri desturi na sifa za mungu wake huyo kwamba zi sawa na za miungu hiyo (ya kipagani). Kwa kutilia mkazo mafundisho yake hayo juu ya mungu wa dini yake ya Kikristo, tuliona jinsi Bwana Paulo asivyomtambua kabisa Yehova au Allah kwa kumhubiri mungu wake huyo (aliyemwita Yesu) kuwa ni mkuu, aliye juu ya mambo yote! Aidha, tuliona kwa uchache pia kwamba, baada ya Bwana Paulo kuichukua imani ya mungu wake huyo mwenye asili ya miungu ya wapagani na ibada zao na kuziandika kwenye nyaraka zake na kudai kuwa zinamhusu Yesu (a.s.), kazi ya pekee iliyofanywa baadae na waandishi wa agano jipya katika Injili zao na nyaraka zao ni kusherehesha mafundisho hayo ya Paulo kwa mapana na marefu kama yalivyo kwenye nyaraka zake. Endelea...

Uhusiano kati ya ibada za dini ya Kikristo na ibada za dini ya Kipagani

Katika toleo Na. 202 la gazeti hili tuliona kwa uchache jinsi muasisi wa dini ya Kikristo, Bwana Paulo alivyokuwa akimshutumu Petro, Barnaba na Wayahudi wengine alipokutana nao huko Antiokia (kwa watu wa mataifa au wapagani) kwa kutofuata kwao moja kwa moja desturi (ibada) za watu wa mataifa (wapagani), kinyume na walivyokuwa wakifanya hivyo kabla ya Wayahudi wenzao waliotoka kwa Yakobo (Myahudi) kufika hapo Antiokia. (Rejea Wagalatia 2:11-14).

Zaidi ya hivyo, tuliona pia Bwana Paulo jinsi alivyokuwa akimlaumu Petro kwa kitendo chake cha kuwashurutisha watu hao wa mataifa, yaani wapagani kufuata desturi za Wayahudi (yaani kufuata Torati ya Nabii Musa a.s.) akidai kwamba mwanadamu hatohesabiwa haki kwa matendo ya sheria (Torati); lakini kwa imani ya Kristo Yesu! (Wagalatia 2:14-16)

Kwa maelezo yake hayo, ikadhihirika kuwa Bwana Paulo alikwenda kwa watu wa mataifa (wapagani) kufuata dini yao ambayo kama tulivyoona, pia ilikuwa ina ibada zake wanazoifanyia miungu yao (miungu-watu) walioiamini kuwa ina desturi ya kujigeuza kuwa wanadamu.

Kwa hali hiyo, kwa kuwa Bwana Paulo anafuata mia kwa mia desturi za dini ya watu wa mataifa, yaani wapagani, tuliona kuwa huo ndio lazima utakaokuwa msimamo pia wa ibada za dini yake ya Kikristo.

Na ili kuthibitisha uhusiano huo (kati ya ibada za dini ya Paulo ya Kikristo na ibada za dini ya kipagani) hapana budi hapa nikazirejea japo kwa uchache ibada hizo za watu wa mataifa (wapagani) kama zilivyotajwa na Yehova; kisha tuzilinganishe na ibada za dini ya Kikristo, tuone jinsi kimsingi zinavyolingana.

Ibada hizo (za watu wa mataifa au wapagani) zimetajwa kwa uchache na Yehova alipokuwa akiwakemea wanadamu wajiepushe nazo kama ifuatavyo:

"Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako, usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA, kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako". (Kumbukumbu la Torati 18:9-12).

Bali walijichanganya na mataifa, wakajifunza matendo yao. Wakazitumikia sanamu zao, Nazo zikawa mtego kwao. Naam, walitoa wana wao na binti zao kuwa dhabihu kwa mashetani. Wakamwaga damu isiyo na hatia, damu ya wana wao na binti zao, Waliowatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani; Nchi ikatiwa unajisi kwa damu". (Zaburi 106:35-38).

Katika maandiko hayo, Yehova kwa uchache tunaona amezitaja ibada hizo zisizopungua nane ambazo hufanywa na watu wa mataifa (wapagani) akiwataka wanadamu wajiepushe nazo mbali kabisa ili waweze kupata radhi yake hapa duniani na kesho huko akhera.

Kati ya ibada hizo za wapagani alizozikemea Yehova hapo juu, amezitaja pia ibada nne ambazo nimeziwekea alama ya maandishi meusi sana (bold) kwa ajili ya mazingatio katika uchambuzi ujao hapo punde.

Ibada hizo ni pamoja na kuua wana na binti (kama kafara), kupandisha pepo, kuwaomba wafu na kuzitumikia (kuabudu) sanamu.

Tuzitazamapo ibada hizi, tunaona ndizo leo zimekuwa ibada za msingi katika dini ya Kikristo mpaka dakika hii na hivyo kudhihirisha wazi uhusiano wa kimsingi kati ya ibada zake (Ukristo) na ibada za dini ya kipagani ambazo Yehova amewakemea vikali wanadamu kujishughulisha nazo kwa namna yoyote ile.

Mfano wa ibada kama hizo za wapagani zilizomo katika dini ya Kikristo mpaka leo ni kama zifuatazo:

Kuua wana

Hii ndiyo ibada kuu ya msingi katika dini ya Kikristo mpaka dakika ya leo.

Licha ya Yehova kuwakemea vikali wanadamu kujihusisha nayo, lakini sambamba na kuanzisha dini yake hiyo (Kikristo), Bwana Paulo aliamua pia kuifundisha ibada hiyo kwa kuunga mkono dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu (Nabii Isa au Yesu a.s.) kama kafara ya dhambi kwa waumini wa dini yake hiyo (Ukristo), kwa kusema:

"Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi" (Warumi 5:8).

"Kristo alitukomboa katika laana ya Torati kwakuwa alifanywa laana kwa ajili yetu, maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti". (Wagalatia 3:13)

Kwa uchache, hivi ndivyo Bwana Paulo aifundishavyo ibada hiyo (ya kuua wana) akiunga mkono dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu kama kafara ya dhambi za Wakristo wote.

Sambamba na mafundisho hayo ya Bwana Paulo juu ya ibada hiyo (kuua wana) waandishi wa agano jipya kwa kuwa nao walidhamiria kuuandikia Ukristo wa Paulo, kama ilivyo kazi yao (kusherehesha mafundisho ya Paulo) katika kusherehesha ibada hiyo kama ilivyofundishwa na "mwalimu wao" Bwana Paulo, katika Injili zao na nyaraka zao wamediriki hata kupenyeza maneno kinywani mwa Bwana Yesu (a.s.) wakisimulia kuwa Yesu mwenyewe (a.s.) ati aliwahi kutabiri kuuliwa kwake msalabani (Tazama Mathayo 12:40, 20:17-19; Marko 10:32-34; Luka 18:31-33 na kadhalika)!

Nasema waandishi hao wamepenyeza ibada hiyo (ya kuua wana) kinywani mwa Yesu (a.s.) kwa sababu siyo wao tu, bali hata 'mwalimu wao' Bwana Paulo anajua wazi kuwa Bwana Yesu (a.s.) kamwe hawezi akathubutu kufundisha ibada potofu za watu wa mataifa, yaani wapagani, zilizokemewa vikali na Yehova.

Kwa upande mwingine, kutokana na mafundisho hayo ya Paulo yanayounga mkono ibada hiyo ya wapagani ( ya kuuwa wana), katika kuunga kwao mkono na kutilia mkazo mafundisho hayo (ya Paulo), Wakristo pia wameibua kitu kiitwacho "Ekaristi takatifu", "Chakula cha Bwana", "Meza ya Bwana" na kadhalika. Hapo hula mikate na kunywa divai wakiashiria kuula mwili wa Yesu (a.s.) na kuinywa damu yake wakijifariji kwa dhana ya kuuliwa mwana wa Mariamu! Sambamba na hilo, pia wamezua "sikukuu ya Pasaka ya Yesu" kama kumbukumbu ya kutukuza dhana ya kuuliwa mwana huyo wa Mariamu kama kafara ya dhambi zao! Kwa ujumla, ibada hiyo ya kipagani inaungwa mkono mia kwa mia na dini ya Kikristo.

Kwa uchache, ibada hiyo (ya kuua wana) ni chukizo kubwa kwa Yehova kwa kuwa alikwishaikemea vikali. InshaAllah upotofu wa ibada hii nitauelezea zaidi katika makala zangu zijazo nitakapokuwa nikiwajibu wapinzani wote wa neno la Mungu waliojitokeza kuzidandia makala zangu zile zilizohusu "Pasaka wa kweli wa Mungu" ijapokuwa waliteleza kwa kufinyangafinyanga maneno wakitoa hoja dhaifu zisizokuwa na msingi wowote.

Kujishughulisha na pepo

Hii ni ibada nyingine ya msingi katika dini ya Kikristo. Hata hivyo, katika kutilia mkazo makemeo yake dhidi ya ibada hiyo potofu, Yehova aliwaambia wanadamu kama ifuatavyo:

"Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu". (Mambo ya Walawi 19:31)

"Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu; ... Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawa sawa na machukizo ya mataifa; ... akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, ... akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha". (2 Wafalme 21:1-6)

"Tena mtu mume na mtu mke aliye na pepo au aliye mchawi, hakika atauawa, watawapiga kwa mawe, damu yao itakuwa juu yao". (Mambo ya Walawi 20:27)

Kulingana na maandiko hayo juu, hapo Yehova kwa ujumla anawataka wanadamu wasishirikiane kabisa na watu wenye pepo, bali wajitenge nao mbali kabisa. Zaidi ya hivyo, mbali ya amri hiyo pia Yehova ameamuru wenye pepo wauawe kabisa na si kuacha kujishughulisha nao tu.

Pamoja na makemeo hayo ya Yehova dhidi ya yeyote anayejishughulisha na pepo, lakini muasisi wa Ukristo, Bwana Paulo anasema:

"Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka; juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho".(Waefeso 6:12)

Kulingana na maelezo hayo ya Paulo hapo juu, tunaona wazi kwamba wakati Yehova amefikia kuamuru kuuawa yeyote atakayebainika akijishughulisha na pepo, hapo juu Bwana Paulo anawataka watu wajishughulishe na pepo kwa kushindana nayo!

Na kama ilivyo desturi yao kuuandikia Ukristo wa Paulo, waandishi wa agano jipya katika kusherehesha mafundisho hayo ya 'mwalimu wao' (ya kuruhusu watu washindane na pepo), wamethubutu kuonyesha katika Injili zao kuwa ati Bwana Yesu (a.s.) aliwahi kujishughulisha na pepo na kuwaagiza wafuasi wake wafanye hivyo! (Tazama Mathayo 8:28-32; 15:21-28; Marko 5:1-13; 7:24-30; 9:38-40; 16:17; Luka 8:26-33).

Pamoja na Paulo na washereheshaji wa mafundisho yake hayo kuhubiri mafundisho hayo ya dini yao ya Kikristo, lakini wanafahamu fika kwamba Bwana Yesu (a.s.) kamwe hawezi kusema au kutenda jambo lolote lililokatazwa na Yehova aliyemtuma, kama hilo la kujishughulisha na ibada hiyo (ya kujishughulisha na pepo) ambayo imetokana na wapagani.

Kwa ujumla basi, katika kufuata mafundisho hayo ya Paulo, ndio utaona mpaka leo Wakristo hasa walokole hujishughulisha sana na pepo katika mikutano yao ya wazi wanayoiita ya "neno la Mungu", "December Crussade", "November Crussade" na kadhalika. Huku wakijua wazi kwamba asili ya ibada hii imetokana na wapagani na Yehova ameikemea vikali sana!

Kuwaomba wafu

Hii vile vile ni ibada ya msingi katika Ukristo, ambayo hudhirika pale dini hiyo (ya Kikristo) inapowafundisha waumini wake kutumia sehemu ya sala zao kuwaomba watakatifu wao waliokufa! Kwa mfano, Wakristo wanayo sala maalum ya kumwomba Bikira Mariamu ambaye inafahamika wazi kuwa mtu huyo kishakufa tokea zamani. Mfano wa sala yao hiyo ni kama ile wasemayo:

"Kumbuka, ee Bikira Maria mpole sana, haijasikika kamwe kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, aliyeomba msaada na maombezi yako. Kwa matumaini hayo, nakukimbilia, ee Mama, Mkuu wa mabikira, Ninakuja kwako, nasimama mbele yako nikilalamika mimi mkosefu, ewe mama wa Neno wa Mungu. Naomba usikatae maneno yangu, bali uyasikilize. Amina. Tunakimbilia ulinzi wako, mzazi mtakatifu wa Mungu, usitunyime tukikuomba katika shida zetu; utuokoe siku zote kila tuingiapo hatarini, ewe Bikira mtukufu mwenye baraka. Amina".(Tazama Chuo kidogo cha sala na nyimbo uk. 34).

Sambamba na sala hiyo, Wakristo pia wanayo sala maalum ya kumwomba mtakatifu Yosefu (Saint Joseph) ambaye naye pia ni mfu. Kupitia sala hiyo, wanamwomba Yosefu kama ifuatavyo:

"Ee Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu, na kisha omba shime ya mchumba wako mtakatifu, tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako...". (Chuo kidogo cha sala na nyimbo uk. 37)

Kwa uchache haya ni baadhi tu ya maombi katika dini ya Kikristo ambayo wafuasi wake (Wakristo) huwaomba wafu. Na yapo maombi mengi ambayo Wakristo huyatumia kuwaomba watakatifu wao wengi waliokufa, kama vile Petro (Saint Peter), Bernard (Saint Bernard) na kadhalika. Ibada hii vile vile kama nyingine nilizozibainisha hapo awali, Yehova amewakemea vikali wanadamu kuzitenda kwa kuwa hazitokani na Yeye bali zinatokana na watu wa mataifa yaani wapagani.

Wakristo kuzitenda ibada hizi ni uthibitisho wa wazi kwamba hawamwabudu Yehova, Mungu wa Nabii Ibrahimu, Ismaili, Isaka, Yakobo, Yesu, Muhammad na Mitume na Manabii wake wengine wote aliowatuma duniani. Kinyume chake wanatenda ibada za dini ya mungu-mtu ya Kikristo.

InshaAllah katika makala ijayo nitahitimisha makala hii ya "je, Yehova na Allah ni Miungu tofauti" kwa kuzibainisha ibada nyingine zaidi za dini ya mungu-mtu ya Kikristo zinazohusiana kimsingi na ibada za dini ya kipagani; na kuonyesha msimamo wa Yehova au Allah (s.w.) kuhusu ibada za wapagani.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook