Na Mwandishi Wetu
TOFAUTI kati ya walionacho na wasionacho ni kubwa hali inayoweza kuiingiza nchi katika machafuko.
Kauli hiyo imetolewa na Mshauri Mkuu wa Chama cha CUF, Prof. Ibrahim Lipumba Jumapili iliyopita katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Temeke Mwisho.
Prof. Lipumba amesema wakati Watanzania wengi hulazimika kulala na njaa baadhi ya siku kutokana na kuishi maisha ya dhiki, wachache walionacho wanaishi maisha ambayo ni vigumu kuamini kama wako Tanzania.
Lipumba amesema hali hiyo imetokana na chama tawala kutokuwa na sera zenye muelekeo wa kuleta haki sawa kwa wote na kuboresha maisha ya wananchi.
"Msiendelee kuikumbatia CCM, kuikumbatia CCM ni kuendeleza dhiki na njaa", Prof. Lipumba aliuambia umati mkubwa wa wakazi wa Temeke waliokuwa wakimsilikiza kwa utulivu mkubwa.
Aidha alihadharisha kuwa nchi inaweza kuingia katika migogoro ya wenyewe kwa wenyewe iwapo CCM itaendelea kuongoza nchi.
"Tuiokoe nchi na hatari ya mapambano kati ya walionacho na wasionacho, tofauti ni kubwa sana", alisisitiza mtaalamu huyo wa maswala ya uchumi duniani.
Akizungumzia kuhusu malipo ya wazee waliokuwa wafanyakazi wa mashirika yaliyokuwa chini ya jumuiya ya Afrika Mashariki, alisema anashangazwa na jinsi wazee hao wanavyoendelea kusumbuliwa wakati wenzao wa Kenya na Uganda walishalipwa muda mfupi tu baada ya kuvunjika jumuiya hiyo.
Mashirika yaliyokuwa katika jumuiya hiyo ambayo ilivunjika mwaka 1977 ni pamoja na Bandari, Railways, Posta na Ndege.
Prof. Lipumba alihoji kwa nini wazee hao hawajalipwa wakati serikali ya awamu ya tatu inadai kulipa madeni ya ndani na ya nje ya nchi.
Aidha, aliikumbusha serikali wakati ikiendelea na zoezi la ulipaji wa madeni iwafidie walionyang'anywa mali isivyo halali wakati wa kamata kamata ya wahujumu uchumi.
"Walionyang'anywa mali zao warejeshewe huku ndiko kulipa madeni ya ndani", alisisitiza Mshauri huyo wa chama cha CUF.
Katika hotuba yake hiyo iliyochukua saa moja, Prof. Lipumba alizungumzia pia haki ya wananchi kuchagua madiwani ambao wao pamoja na Meya huunda Halmashauri ya Jiji.
Alisema jiji kuendelea kuendeshwa na Tume ni kinyume na demokrasia hivyo akawataka wananchi kutoruhusu hali hiyo.
Aidha alionyesha jinsi serikali isivyowajibika kwa kutaja ubovu wa barabara, ukosefu wa maji na uchafu wa mazingira.
"Serikali ni wajibu wake kujenga mabarabara sio kusubiri itoe ahadi wakati wa kuomba kura", alisema Prof. Lipumba.
Halikadhalika alilaumu tabia ya serikali kukwepa wajibu wa kujenga mashule na kuweka madawati badala yake kuwashawishi wananchi kujijengea wenyewe.
Kuhusu ajira kwa vijana, Lipumba aliishauri serikali kuandaa mazingira yatakayopelekea watu kujiajiri badala ya kuendelea kutoa kauli za kisiasa kuhimiza ajira binafsi huku mazingira hayaruhusu.
Alimaliza hotuba yake kwa kuwaambia wananchi kuwa anamuunga mkono Rais Benjamin Mkapa kwa kauli yake kuwa sera za CCM hazitekelezeki, lakini akasisitiza kuwa matatizo ya wananchi yanatatulika.
Hotuba ya Profesa Lipumba
Temeke ilifuatia ziara yake wilaya hiyo ambapo pamoja na mambo mengine
alifungua matawi mapya 40 ya chama hicho.
Na Musa Ally
KATIBU wa Bakwata Mkoa wa Morogoro Mzee AbdulHamid Hassan Abubakar (79) alifariki dunia wiki moja iliyopita nyumbani kwake na kuzikwa mjini humo.
Marehemu alikuwa Katibu wa Bakwata wa Mkoa huo, wadhifa aliodumu nao tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo miaka 31 iliyopita.
Mamia ya Waislamu wa mji wa Morogoro na vitongoji vyake walijumuika pamoja nyumbani kwa marehemu kona ya mtaa wa Uhuru na Tuwa Tugawe katikati ya mji huo kuungana na ndugu kwa ajili ya mazishi yaliyomalizikia katika makaburi ya Kilima cha Kola (Kola Hill) nje kidogo ya mji huo.
Marehemu AbdulHamid ni mzaliwa wa kwanza kati ya watoto sita wa aliyekuwa Sheikh maarufu mjini humo marehemu Hassan Abubakar aliyefariki miaka ya 70 mwanzoni.
Kati ya ndugu aliozaliwa nao ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Polisi (RPC) wa Mkoa wa Iringa aliyelazimika kujiuzulu kufuatia kuuwawa kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo miaka ya 70 Dr. Willbert Klerruu.
Klerruu aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake siku ya Krismasi na aliyekuwa mfanyabiashara na mkulima mkubwa mkoani Iringa Bwana Mwamwindi kufuatia mzozo uliotokana na hatua ya Mkuu wa Mkoa huyo kutaka kumega sehemu ya shamba la tajiri huyo kuingiza katika mpango wa vijiji vya ujamaa.
Kabla ya kujiunga na Bakwata hayati AbdulHamid alikuwa mfanyakazi katika Hospitali Kuu ya Mkoa wa Morogoro.
Akiwa Katibu wa Bakwata alishiriki katika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Msikiti wa Ijumaa wa Boma Road ambao licha ya michango ya hali na mali kutoka kwa waumini; sehemu kubwa ulifadhiliwa na marehemu Taj Mohammed.
AbdulHamid (Mzee Modibo) alifahamika kama "mzizi" wa Bakwata Morogoro hivyo kifo chake kitakuwa kimeliachia Baraza hilo pengo ambalo huenda lisiweze kuzibwa.
Alifahamika kwa ushupavu wa kupambana na kila aliyejaribu kuipinga Bakwata mkoani humo.
Marehemu ameacha watoto 11 (wa 12 ni murtadi) na wajukuu kadhaa.
Mwenyezi Mungu amghufirie.
Inaa lillahi wainna ilahi
raajiun.
Na Bakari Mwakangwale
WAISLAMU wa kijiji cha Mambo, tarafa ya Mtae wilaya ya Lushoto wametakiwa kurejea kwa Mwenyezi Mungu wanapokutwa na majanga wala si kwend kwa mtu yeyote, "Zumbe", yoyote au mtoto wa "Zumbe".
Hayo yameelezwa na Ustadh Abbas Salim kijijini humo hivi karibuni baada ya mgongano na mzozo mkubwa (mawaidha) kuhusu ubaya wa kumshirikisha Allah (s.w.).
Aliwalaumu Waislamu kuamini kuwa kuna mtu mwenye uwezo wa kuleta mvua, na bila kumpelekea mapesa mvua haitonyesha na madudu (viwavi jeshi) kutotoweka.
Aidha, aliwaeleza kuwa hayo majanga yanatokana na makosa yao waliyotenda ndio Mwenyezi Mungu atawajulisha. Hivyo tabia hiyo alitaka ikomeshwe ya kuchangia mvua (kutoa mapesa kumpelekea mtu alete mvua na kuondosha madudu).
Akielezea mgongano na mzozo huo Ustadh Abbas alisema: " Kuwa mbaya zaidi ni pale waliposomewa aya kuwa hakuna Mwenye uwezo wa kuleta mvua, kwani baadhi ya watu walidai hizo aya zinazohusu maswala hayo zifutwe, sababu mambo hayo ya kuchangia mvua wanayo tangu enzi za mababu na kudai kama mmekosa mawaidha mengine muache, lakini maswala ya mvua ni utamaduni wetu tangu kale".
Hali hiyo ilipelekea mpaka kushitakiana katika uongozi wa kijiji (ofisi za CCM) kwamba wanabughudhiwa kuwa kuchangia mvua ni kosa kubwa!
Pia aliwaomba Masheikh, waalimu wa kweli wawasaidie kuelimisha suala hili kuwa mvua ni ya Mungu (s.w.) na mabalaa, kama ukame, madudu ni balaa alioleta Mungu (s.w.) na kuwaelimisha nini Uislamu, nini shirki na nini ubaya wa shirki.
Hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti kuna wadudu (viwavi jeshi) miongoni mwa mikoa iliyoathirika ni Tanga na vitongoji vyake.
Mwisho alimalizia kwa kusema
Uislamu wa majina hautasaidia bila kuwa na Uislamu wa moyo na itiqad.
Na A.S. Chachika
TARAFA za Usangi na Ugweno wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro zimekumbwa na wimbi la uvamizi, uvunjaji na wizi katika Misikiti.
Sakata moja ilitokea hivi karibuni ambapo milango mitatu ya Msikiti wa Kighare katika tarafa ya Usangi ilivunjwa. Wezi hao waliweza kuvunja kishubaka kilichojengwa kwa nondo na zege kuhifadhia mashine ya sauti na kuiba mashine yenye thamani ya shilingi laki tano na sitini elfu.
Walichukua jora moja la kitambaa cha sanda pamoja na shuka za jeneza. Haikupita muda kikosi hicho kiliuingilia Msikiti wa Ndanda katika tarafa hiyo hiyo na kuiba mashine nyingine yenye thamani kama hiyo, na Msikiti wa Lomboni katika tarafa ya Ugweno.
Msikiti wa Mfinga katika tarafa ya Ugweno ulivunjwa na mashine ikaporwa na madawa na vifaa kadhaa vya zahanati ya mtaa.
--
|
|