Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameaswa kuepuka tabia ya kujitenga na siasa badala yake wajiimarishe kuing'oa CCM ambayo imedumu madarakani kwa muda mrefu bila ya kuwaletea maendeleo.
Kauli hiyo ni sehemu ya aliyoyazungumza mshauri mkuu wa chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba katika mkutano wa hadhara uliofanyika jumapili iliyopita katika uwanja wa Ukombozi Manzese Jijini Dar es Salaam.
Lipumba amesema si busara kwa wananchi kujitenga na siasa kwani kufanya hivyo ni sawa na kuruhusu nchi na rasilimali zake zifujwe na waharibifu.
" Kususia siasa ni sawa na mkulima anayewasusia nguruwe shamba lake la mihogo", alisema kwa msisitizo.
Aidha, alisema mahali penye njaa na dhiki hapana amani, hivyo aliwataka wananchi wa jimbo la Ubungo na Watanzania wote waiokoe nchi yao na hatari ya machafuko kwa kuiondoa CCM madarakani.
Huku akisikilizwa na maelfu ya wananchi wa maeneo ya Mwembechai, Tandale, Manzese, Ubungo na Sinza, Lipumba alisema Watanzania watadumisha dhiki, njaa na mazingira mabovu kama wataendelea kuiweka madarakani CCM.
Alisema serikali ya CCM imekuwa rahisi kwake kuvunja nyumba za wananchi wa Kazi Mzumbwi na Nzasa kuliko kuweka mazingira ya Manzese katika hali ya usafi.
Alitoa mfano wa maji machafu na taka zisizozolewa ambazo zimefurika sehemu kadhaa za eneo hilo.
Alisema wakati barabara zimejaa madimbwi ya maji machafu, kinamama wanahangaika na ndoo kutafuta maji ya kutumia.
Akigusia hali ya maisha ya wakazi wa Manzese, Profesa Lipumba alisema hali ya maisha kwa wakazi wa maeneo hayo ni ngumu na ya kuhuzunisha.
Kuhusu elimu Prof. Lipumba alisema shule za wananchi wa hali za chini ndizo zinazoongoza kwa watoto kufeli darasa la saba.
Alisema vijana wanaofaulu maeneo hayo ni wachache sana kulinganisha na shule wanazosoma watoto wa viongozi.
"Tutaendelea na hali hii mpaka lini wakati CCM haina sera ya kuwakomboa wanyonge kielimu?", alihoji Prof. Lipumba huku umati wa wananchi ukimuitikia kuwa tumechoka na CCM.
Kauli ya Prof. Lipumba ilikuwa inajibu malalamiko aliyopewa na baadhi ya wakazi wa maeneo hayo kuwa vijana wao hukamatwa na kuwambiwa kuwa ni wazururaji wakati ambapo wamezaliwa na kukulia maeneo hayo.
"Waende wapi wakati serikali imeshindwa kuwaendeleza baada ya kumaliza darasa la saba, leseni za biashara wananyimwa kwa kutakiwa kulipa kodi ya mapato kabla ya kuanza biashara", alisema kwa masikitiko.
Kuhusiana na suala la Pasport, Prof. Lipumba alisema hiyo ni haki ya raia lakini serikali ya CCM imekuwa ikiivunja kipindi chote cha utawala wake.
Aliuambia umati huo kuwa wakati vijana wa nchi nyingine hujitafutia riziki nje ya nchi zao, serikali ya CCM imewanyima vijana elimu, ajira na haki ya kikatiba ya kuwa na Pasport.
Alitoa mfano wa vijana wengi wa Afrika Magharibi ambao hivi sasa ni madereva taxi Washington Marekani, kwa kusema kwamba hayo ni matokeo ya serikali zao kuwapa ruhusa wakajitafutie riziki mahali pengine.
Awali wakati wa ufunguzi wa matawi mapya ya CUF Prof. Lipumba alitoa pole kwa wakazi wa maeneo ya Mwembechai na Manzese kutokana na uvamizi uliofanywa na polisi mwanzoni mwa mwaka jana ambao ulisababisha kuuawa kwa watu zaidi ya wanne, majeruhi na wengine kadhaa kuwekwa rumande.
Prof. Lipumba aliwaambia wananchi wa Manzese na Mwembechai kwamba serikali yenye kuthamini wananchi wake isingekaa kimya hadi leo baada ya mauaji hayo.
"Vipi wananachi wauawe serikali ishindwe kutoa tamko rasmi, hizo ndizo sera za CCM?", alihoji.
Sambamba na ufunguzi wa matawi
katika jimbo hilo, wanachama wapya zaidi ya 3000 waliandikishwa.
--
|
|