'Lazima kupambana na dhalimu'
 

Na Mwandishi Wetu

NAJUZU dhalimu kuandamwa na ubaya wake kutangazwa awe dhalimu huyo ni mtu binafsi au serikali.

Hayo yamesemwa na mmoja wa Makhatibu wa Masjid Manyema Sheikh Abeid wakati akitoa khutba Ijumaa iliyopita.

Aidha, Sheikh Abeid amewakumbusha Waislamu juu ya wajibu wao wa kusimamia haki, kuondoa maovu katika jamii na kuzilinda mali za Waislamu.

Sheikh Abeid alikuwa akielezea dhulma iliyofanywa na Bw. Daniel kupitia mahakama ambapo Hakimu Natalia Kimaro alimpa Bw. Daniel haki ya kusimamia Mirathi ya hajat Aziza Omar kinyume na haki na sheria.

Aliwahimiza Waislamu watoe michango ili kuifufua kesi hiyo upya kwa matarajio kwamba haki itapatikana.

Masheikh ambao walishalizungumzia suala hili kwa uchungu kabisa na kuwaomba Waislamu waungane katika jambo hili ni pamoa na Sharifu Juneidy wa Masjid Kitumbini.

Awali katika khutba yake Sheikh Abeid aliwakumbusha Waislamu kwamba hakuna mtenganisho wa maisha ya dini na dunia au dini na siasa kwani Mtume (s.a.w.) pamoja na kuwa Imam, alikuwa amiri jeshi, mtawala na kiongozi wa dola.

Aidha, alisisitiza kwamba Mitume wote wamekuja na hukumu na sheria na kwamba wale wanaondesha maisha yao na kuhukumu kinyume na hukumu za Mwenyezi Mungu ni maasi, mafasiki na makafiri. Alinukuu aya za 44 na 47 za surat Almaida kutilia nguvu hoja zake.

Sheikh Abeid ambaye pia ni Imam wa Masjid Mwinyi, Ilala aliweka wazi kwamba Uislamu hautambui utenganisho wa dini na siasa. Akaeleza kuwa uharibifu mkubwa uliofanywa na watawala wa Kikristo ndio ulioleta dhana hizi potofu.

Alitoa mfano wa Mfalme wa Kiingereza zama hizo King James ambaye aliandika Biblia yake akiweka aya atakazo na kuondoa aya atakayo. Kazi hiyo aliifanya miaka mia nne iliyopita na sasa Biblia hiyo huitwa King James Authorised version.

Aidha, alisema hii leo Malkia ni kiongozi wa Kanisa huko Uingereza, lakini sheria za Kikhabithi kama zile za kuruhusu mambo ya Kaumu Lut hupitishwa bila yeye kupinga. Na akasisitiza kwamba kuyataja haya si kashfa.

Kwa muktadha huo Sheikh Abeid aliwatahadharisha Waislamu na dhana kama 'Usekula' na nyinginezo ambazo ni zao la uharibifu wa watawala Wakristo huko Ulaya. 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook