Hamkuwaelewa Masheikh wenu?
 

Na Abu Kalam
 

IMAM MALIK BIN ANAS
 

Imam Malik alizaliwa mwaka 93 A.H. Baadhi ya vitabu vimetaja pia mwaka 94 na 95 A.H.

Wazazi wa Imam Malik hutokana na familia ya kifalme ya Kiarabu toka Yemen ambayo ilihamia Madina. Wakati anazaliwa Imam Malik Dola ya Kiislamu ilikuwa chini ya uongozi wa Khalifa Walid bin Abd al-Malik na japo makao makuu ya Dola yalikuwa yamehamishiwa Damascus Syria; lakini Madina ulibakia mji mashuhuri na kitovu cha Elimu ya Uislamu.

Familia ya Imam Malik ilizungukwa na ndugu na jamaa wa karibu waliokuwa na elimu ya kutosha. Hivyo alianza kupata elimu yake katika mazingira ya nyumbani zaidi ya hapo alisoma kwa Waalimu wengine saba mashuhuri wa fani mbalimbali; miongoni mwao walikuwa Jafar al-Sadiq kitukuu cha Imam Hussein.

Pamoja na kujikusanyia elimu nyingi; umaarufu wa Imam Malik ulizidi kuvuma kutokana na unyenyekevu na ucha-Mungu wake. Watu walitoka masafa ya mbali kuja Madina kuhudhuria darsa za Imam Malik. Sehemu kubwa ya muda wake aliutoa kwa kufundisha na akiifurahia kazi hii.

Imam Malik alikuwa mtaalam mzuri ya Hadith; na mtu madhubuti na mwenye msimamo. Hakukubali kutolewa katika haki kwa hali yoyote iwayo. Wakati fulani alitoa fat'wa ambayo ilikuwa kinyume na matakwa ya Gavana wa Madina. Gavana alimuonya asitoe fat'wa hiyo hadharani. Lakini kwa kuridhika kuwa ndio haki. Imam Malik alitoa maoni yake hadharani. Kwa tendo hilo alichapwa viboko hadharani na serikali.

Katika kazi muhimu alizoziacha Imam Malik ni kitabu chake al-Muwatta chenye mjumuiko wa Hadith na mafundisho ya Mtume ya ibada na mas'ala mbalimbali ya Kiislamu.

Katika suala la mauaji ya Mwembechai Masheikh wengi wamepiga kimya wakiogopa kutoa maoni yao kinyume na msimamo wa serikali.

Wakiwa na waumini faraghani huilaani serikali kwa udhalimu wake katika masuala mbalimbali ikiwemo kuchomwa nyumba za wananchi Nzasa na kuuliwa Waislamu pale Mwembechai.

Lakini Masheikh hao hawathubutu kuyasema hayo kwenye mimbari zao wala kwenye hafla za maulid na shughuli mbalimbali.

Wakiwa faragha na waumini huwalaani baadhi ya viongozi wa serikali kwa kuwataja majina na kueleza ubaya wao, lakini wakiitwa na viongozi hao hao maofisini kwao au majumbani huenda mbio chai wakanywa na wakataka waongezwe kikombe cha pili. Na wakiwa hadharani watawasifu na kuwafanyia kazi zao za kisiasa. Wanaogopa kuisema haki mbele yao.

Je; Masheikh hawa hawakusoma historia ya Imam Malik; Je; hawasomi al-Muwattah? Je; hawakuwaelewa Masheikh wao? 
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook