Sheikh Jongo na agenda ya Makadhi
 

Na Abu Kalam

IMAM wa Msikiti wa Manyema uliopo Jijini Dar es Salaam Sheikh Hamid Jongo wiki iliyopita aliwahimiza Waislamu wenye sifa ya kuwa Makadhi wajaze fomu ili wapate mafunzo.

Wapi imeibukia agenda hii na malengo yake, si suala muhimu hivi sasa. Lakini je, Waislamu kuna mambo yetu yamekwama kwa vile hatuna Kadhi? Hatuna agenda nyingine muhimu zaidi? Zipi ni aula zetu.

Kwa mujibu wa sheria na taratibu za elimu nchini tumefikia mahali ambapo mtoto ambaye hakupitia shule ya awali inayotambulika hatokubaliwa kuanza darasa la kwanza shule ya msingi.

Waislamu kwa kulitambua hilo wamekuwa wakianzisha shule za awali katika Misikiti yao. Watoto wanaopitia shule hizi pamoja na kujua kusoma na kuandika kabla ya kuanza darasa la kwanza huwa wanapata elimu ya msingi juu ya Muumba wao na wajibu wao kwake. Aidha hupata msingi imara wa maadili mema.

Taarifa ambazo hazijawa rasmi zinabaini kwamba shule hizi hazitotambuliwa mpaka ziwe na waalimu wenye vyeti kutoka vyuo rasmi vinavyotambuliwa na serikali. Serikali yenyewe haina hata Chuo kimoja cha aina hiyo ila vilivyopo ni vile vya Kanisa.

Kwa kiongozi hasa Maimamu wa Misikiti wanaojua wanachokifanya kulingana na mahitaji ya jamii, hapana shaka malezi ya watoto itakuwa moja ya agenda zake muhimu. Hii ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha, kuwahimiza na kuwaongoza waumini wajenge na kuendesha shule bora za watoto.

Aidha, kuandaa utaratibu wa kupata waalimu wenye sifa ili Waislamu wasilazimike kuwasomeshea waalimu wao kutoka vyuo vya Kanisa. Haya ndiyo miongoni mwa matatizo ya msingi ya Waislamu. Na Sheikh au Imamu mwenye kujua afanyalo hili litakuwa miongni mwa agenda zake.

Kwa vile nchi hii inadai haina dini haiendeshwi kwa sheria za dini. Ila hutumika katika mambo binafsi na familia muhimu ikiwa ni ndoa na mirathi. Ndoa haihitaji Sheikh wala Kadhi ili iswihi kwani mwenye haki ya kuozesha ni walii ambaye ni Baba, kaka mtu, babu na wanaofuatia kwa daraja.

Halikadhalika mirathi ni suala la kuwapa Waislamu elimu hii ya msingi na wengi wamekuwa wakirithishana wenyewe bila kumuita Sheikh. Kwa hiyo kukosekana kwa Kadhi hakujawa ni tatizo kwa Waislamu.

Lakini leo ni tatizo kubwa ukienda shule za msingi na sekondari hakuna waalimu wa kuwasomesha wanafunzi Waislamu wakati wa vipindi vya dini. Watoto Waislamu wakati wenzao Wakristo wanasomeshwa watakuwa ama wanaimba tu kasida au kucheza. Katika baadhi ya shule hulazimishwa kuingia kipindi cha Kikristo ili wasiwasumbue wenzao.

Haya ndiyo matatizo ya kushughulikia. Kutafuta waalimu wenye sifa, vitabu na mishahara ili watoto wetu katika shule za msingi na sekondari wafundishwe Uislamu.

Leo Sheikh, Imam mnapotuletea agenda ya kusomesha Makadhi, unataka wakafanye wapi hiyo kazi ya Ukadhi maana hatuna mahakama zinazowatambua. Na hata kama ni suala la ndoa na talaka bado ni kichekesho kuibuka na agenda ya kusomesha Makadhi wakati sheria yenyewe ya nchi haitambui sheria ya ndoa na talaka ya Kiislamu (Tazama Sheria ya Ndoa 1972). Unaoa kwa Sheikh kuacha kwa 'Natalia Kimaro'.

Tungewaelewa Masheikh wenye tenda hii ya Makadhi kama wangekusanyana wakaibana serikali iifanyie marekebisho sheria ya ndoa ya 1972 na pili iondoe agenda yake ya kuwa na sheria moja ya mirathi nchini.

Moja ya sifa kuu ya Kadhi ni kuwa muadilifu na mkweli hata mbele ya Mfalme. Tunajaribu kuwaza ni Makadhi wa aina gani ambao mwalimu wao ni Hamid Jongo. Sheikh Hamid Jongo ambaye si tu kashindwa kusema ukweli wa yaliyowasibu Waislamu Mwembechai kwa kuuliwa na mama zao kudhalilishwa na polisi; lakini akaungana na Bw. Yusuf Makamba kuwalani wadhulumiwa.

Makadhi wa aina hii ni janga kwa ummah wa Waislamu. Sisi wenyewe tumawalii wa mabinti zetu na kama ni mirathi tutarithishana wenyewe. Aya na Hadith zipo wazi.

Vijana wa Kiislamu kwa maelfu kila mwaka wanaingia mitaani na mijini wakiwa hawana ajira toka darasa la saba na sekondari. Tunataka Maimamu na Masheikh watakaowaongoza Waislamu kutokana na zaka na sadaka zao wakaanzishe mipango ya kilimo, ufundi na biashara ya kuwasaidia vijana hawa. Kukosekana kwa mipango hiyo leo tuna tatizo kubwa la vibaka, changudoa na vijana wengi wa Kiislamu kuishia kuvuta bangi. Na kubwa zaidi kuupiga vita mfumo dhalimu uliowapora wao na wazazi wao haki ya elimu, ajira na haki ya kuwa huru katika mambo yao ya kidini.

Hata ukiweka Kadhi kwa kila kitongoji tatizo hili halitaondoka. Lakini vile vile hakuna binti leo kakwama kuolewa kwa vile hakuna Kadhi.

Kuwa kiongozi wa watu ni kuonyesha njia na huwezi kuonyesha njia kama wewe mwenyewe ni kipofu wa matatizo ya watu. Kiongozi ni lazima uzijue aula katika yale wanayoyataka watu.

Na hapa ni vyema kuzipongeza juhudi za Sheikh Jabir Katura na uongozi wa Msikiti Mkuu wa Mwanza kwa mipango yao ya Zakah na Sadaka ambayo imesaidia kuwasomesha baadhi ya vijana na kuwanunulia vyerahani baadhi ya mabinti na akina mama Waislamu.

Aidha, ni mahala pake kuzitaja juhudi za Taasisi ya Tanzania Muslim Hajj Trust (TMHT) chini ya Sheikh Nurdin Hussein Shadhly kwa kuanzisha mafunzo ya Kompyuta.

Matarajio ni kwa Taasisi nyingine za Kiislamu kuiga mifano hii.
--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook