Na Badru Kimwaga
WAZEE wa Mahakama za mwanzo wamelalamika kuwa kwa muda mrefu hawajalipwa posho zao za kusikiliza kesi hali inayowafanya wazee hao kuishi maisha ya dhiki na wengine kuacha kuhudhuria mahakamani na kufanya kesi nyingi kuahirishwa.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye mahakama ya Magomeni, Jijini wazee hao ambao waliomba majina yao yasitajwe walisema kuwa tangu kuingia madarakani kwa uongozi wa awamu ya tatu wazee wa mahakama wamekuwa wakisuswa na kusahauliwa jambo ambalo halikuwepo huko nyuma.
Mzee mmoja ambaye nguo zake na hali yake kiafya ni ya kusikitisha alisema kuwa hajui ni kitu gani kinachowafanya viongozi wa sasa kuwasahau wakati wanatambulika katika utendaji wao wa kazi.
Uchunguzi wa mwandishi wa habari hizi mahakamani hapo umeweza kugundua kuwa wazee wengi katika mahakama hiyo wamekuwa hawahudhurii kesi nyingi kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya kifedha na vile vile umri mkubwa ambapo katika mahakama hiyo yenye mahakimu sita na wazee 12 ni wazee wa baraza sita tu wanaohudhuria.
Mmoja wa Mahakimu wa mahakama hiyo Mheshimiwa Mlawa alisema kuwa tatizo la kukosekana wazee wa baraza limeshapelekwa kwenye Wizara ya Sheria kwa Waziri, Mh. Mwapachu, lakini hadi sasa hawajapata majibu, ambapo alipendekeza wateuliwe wazee wengine kuchukua nafasi za wazee waliopo sasa ambao umri wao ni kati ya miaka 70 hadi 90 jambo linalowafanya kushindwa kufika mahakamani.
Na Masoud Mohamed
JUMUIYA ya walimu wa Kiislamu Tanga (JUWAKITA) mwishoni mwa wiki iliyopita waliendesha semina ya siku mbili iliyofanyika shule ya Jumuiya.
Katika semina hiyo jumla ya mada saba ziliwasilishwa na wahadhiri mbalimbali kutoka Tanga na nje ya Tanga. Washiriki walikuwa ni walimu wa madrasa na shule za msingi kutoka baadhi ya maeneo ya wilaya zote za Tanga.
Matatizo mbalimbali yanayoukabili umma wa Kiislamu na hasa watoto wa Kiislamu yalijadiliwa kwa kina katika semina hiyo. Kwa upande mwingine mbinu kadhaa za kujinasua zilijadiliwa.
Mwisho wa semina hiyo mnamo siku ya Jumapili, wanasemina kwa pamoja walitoa tamko la kulaani magazeti yanayoitwa ya mitaani kwa juhudi zao kubwa za kupotosha jamii.
Magazeti hayo ambayo yalielezwa kuegemea kwenye mapicha ya uchi na maneno ya ovyo na ambayo ni mengi kuliko magazeti mengine ni kikwazo kwa walimu wa dini kuiadabisha jamii.
Semina kama hizo pia ziliazimiwa kufanyika mara kwa mara sambamba na utekelezaji wa matumizi ya mihtasari na vitabu ili kuwa na mfumo wa pamoja wa ufundishaji.
--
|
|