Na Mwandishi Wetu
BENKI Kuu (BoT) imetoa taarifa ya kuhuzunisha kuhusu kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kulinganisha na dola ya Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hivi sasa dola ya Kimarekani ni sawa na zaidi ya shilingi 700 za Tanzania. Hii ndiyo kusema kupanda kwa bidhaa na huduma kadhaa kutafuatia muda si mrefu.
Taarifa ya BoT iliandamana na maelezo kwamba wakati shilingi ya Tanzania ikiendelea kukosa thamani, shilingi za Uganda na Kenya zimeendelea kudumisha thamani zilizo nazo sasa ambapo tangu Januari mwaka huu zinaonyesha upungufu wa senti tano tu mbele ya dola ya Marekani.
Tofauti na shilingi hizo, shilingi ya Tanzania imekuwa ikishuka kwa kasi ya kuhuzunisha ambapo kuanzia Januari mwaka huu hadi leo imekuwa ikipoteza thamani ya senti 83 kila siku, shilingi 25 kila mwezi na shilingi 125 kwa miezi yote. Huku ni kushuka kunakoleta dhana kwamba tangu serikali ya awamu ya tatu ikamate usukani nchi imekuwa ikiangamia kiuchumi.
Zimetolewa sababu kadhaa kufuatia mshuko huo, miongoni mwa hizo ni kushuka kwa mauzo ya bidhaa za Tanzania nchi za nje kulikochangiwa na uchache wa bidhaa zinazopelekwa nje kwa ajili ya soko sambamba na kukosa ubora. Sababu nyingine ni kwamba zaidi ya robo tatu ya bidhaa zinazotumika hapa nchini huagizwa kutoka nje. Vile vile uzalishaji katika viwanda vyetu umeanguka na viwanda vingi kulazimika kufungwa. Kadhalika kukwama kwa mzunguko wa pesa.
Wataalam wa mambo ya uchumi, biashara na fedha wana maelezo ya kina juu ya hili, lakini la msingi hapa hali yetu kiuchumi ni mbaya sana. Na hatari zaidi ni kwamba kadri uchumi wa nchi unavyodorora ndivyo thamani ya pesa yetu inavyozidi kushuka mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka huu, kwa kasi hii ya muanguko, dola moja ya Tanzania huenda ikawa sawa na mapesa ya Tanzania yanayoweza kujaa kikapu.
Kwetu Watanzania, huu ni msiba katika mlolongo wa misiba iliyokulikumba Taifa letu tangu serikali ya awamu ya tatu iingie madarakani.
Kwa bahati mbaya sana, semina, midahalo na hotuba za viongozi hazionyeshi dalili wala uelekeo wa kuoikoa nchi kutokana na msiba huu wa kiuchumi unaoweza kuchochea machafuko ya wenyewe kwa wenyewe.
Cha kusikitisha ni kule kuongezeka kwa safari za nje na hotuba ndefu zenye misamiati ambayo bila shaka wananchi wengi hushindwa kuielewa.
Kama alivyopata kusema mchumi mmoja kwamba uchumi duni ni chanzo cha dhiki, njaa, maradhi, mazingira mabovu hatimaye vita na mauaji. Ni wazi kwamba hivi sasa nchi inaelekea huko.
Katika hali hii yule anayejifaragua kuelezea udhibiti wa mfumuko wa bei(Inflation) pekee bila ya kuwepo programu makini na zenye kutekelezeka, hawezi kuwasaidia Watanzania kuboresha maisha yao. Zaidi ya hivyo ni kwamba kukuwa kwa uchumi kwa kweli ni hali inayoweza kujieleza yenyewe mitaani badala ya viongozi kuhangaika kutafuta asilimia, uwiano, mizania na kadhalika kuwazuga wananchi wa kawaida.
Viongozi wetu waache mzaha, hali nzuri ya uchumi siyo kuteremka bei ya nyama inayouzwa Kariakoo. Kutoa mifano hiyo ni kujaribu kuchezea uhai wa wananchi.
Nyama imeshuka bei kwa sababu watu wanashindwa kununua kutokana na hali ya ufukara waliyonayo. Na hii imethibitishwa na taarifa ya Benki kuu kwamba uchumi wa nchi yetu umeporomoka na kusababisha shilingi yetu kushuka thamani.
Hali ya nchi yetu ni mbaya kiuchumi jahazi linaelekea kuzama. Wananchi tuihoji serikali ina mkakati gani kutuepusha na janga hili?
Kura ya mwananchi ni mkataba kati yake na serikali anayokusudia kuichagua na miongoni mwa maafikiano ya mkataba huo ni kuboreshwa hali za kijamii.
Kukiri kushindwa mkataba
ni ushujaa na kuepusha maafa. Na hiyo ndiyo desturi ya watu wenye kuheshimu
ahadi na maafikiano!
--
|
|