MAKALA
 
 
Agenda ya NATO Kosovo...
 

Na Said Rajab

KUSAMBARATIKA kwa siasa za Kikomunisti duniani kumeleta mahusiano mapya ya kimataifa. Hali ya vita baridi kati ya Ulaya Magharibi (mabepari) na Ulaya Mashariki (Wakomunisti) imetoweka. Maguvu yote ya kuendesha siasa za ulimwengu yamebaki kwa nchi za Magharibi. Nguvu pekee iliyolala inayowatia homa wa Magharibi ni Uislamu.

KWA kifupi, umoja wa kujihami wa nchi za Ulaya Magharibi (NATO) hautaki kuona jamii ya Kiislamu ikiibuka ndani ya Ulaya. Katika agenda hii NATO inaungana moja kwa moja na vitendo vya Waserbia dhidi ya Waislamu wa Kosovo. Mashambulizi ya anga yanayofanywa na majeshi ya NATO dhidi ya Yugoslavia si kwa ajili ya kuwanusuru Wakosovo wenye asili ya Albania.

Ingawa NATO inajifanya kuishambulia Yugoslavia kwa lengo la kumlazimisha Rais Milosovic asimamishe mauaji ya Wakosovo wenye asili ya Albania, lakini ukweli hauko hivyo. NATO bado ina agenda ya kuangamiza kabisa maguvu ya kijeshi yaliyobaki katika nchi zilizotawaliwa na Wakomunisti.

Ikumbukwe kwamba wakati dunia ilipokuwa inayumbishwa na matapo mawili yenye nguvu zinazolingana (Western bloc and Eastern bloc), tulishuhudia kipindi cha mashindano ya silaha kali za maangamizi kati ya matapo haya. NATO ikiongozwa na Marekani iliweka vituo vya kijeshi sehemu mbalimbali za dunia ili kujihami na nguvu za 'Warsaw pack'.

Nayo 'Warsaw pack' ikiongozwa na USSR waliweka vituo vya kijeshi maeneo mengi tu ya dunia ili kukabiliana na NATO. Moja ya vituo muhimu vya 'Warsaw pack' katika bara la Ulaya ilikuwa eneo la Balkan (Yugoslavia iliyosambaratika). Na katika bara la Amerika ya Kaskazini ni Cuba.

Inasemekana USSR iliweka nguvu kubwa za kijeshi na silaha nzito katika maeneo haya na ndiyo maana NATO haikuthubutu kabisa kuanzisha vita na 'Warsaw pack' hata pale Cuba ilipoishambulia Marekani kwa kombora mwaka 1962. Kusambaratika kwa Ukomunisti na 'Warsaw pack' kumeacha tishio la silaha hizi kwa nchi za Magharibi. Nchi za eneo la Balkan zisije zikaunda 'block' nyingine itakayopingana na mabeberu wa NATO kwa msaada wa silaha hizi.

Kwa hiyo tusishangae tunapoona kwamba mashambulizi ya anga ya NATO yanalenga zaidi Belgrade na siyo Kosovo. Mgogoro wa Kosovo ni kisingizio tu cha kuishambulia Yugoslavia.

Angalia jinsi walivyojiingiza kwa hila katika mgogoro huu kwa lengo la kutimiza azma yao. Walizikutanisha pande zinazopingana mjini Rambolliet Ufaransa. Nchi zinazounda NATO zilikuwa na agenda iliyokwishapIkwa ya kumkwamisha Milosovic katika mazungumzo ya amani. Walimlazimisha Milosovic akubaliane na mpango wao wa amani ambao umeitaka Serbia iiachie Kosovo. Jambo ambalo ni gumu kwa Milosovic. Wakosovo (KLA) walikubaliana na mpango ule kwa sababu ulikuwa unawasaidia na ndicho walichokuwa wanapigania

Milosovic alipewa sharti kwamba akubaliane na mpango ule wa amani la sivyo majeshi ya NATO yatamshambulia. Walijuwa Milosovic asingekubali na sababu ya kumshambulia ingepatikana na kisingizio pia.

Mashambulizi ya majeshi ya NATO dhidi ya Yugoslavia yaliongeza sana wimbi la wakimbizi waliokimbilia Macedonia na Albania na wengine kwenye makambi ya mpakani mwa Macedonia na Kosovo. Kuthibitisha kwamba NATO ilikuwa na agenda moja na Milosovic kuhusu kuwafurusha Waislamu wa Kosovo mjini Kosovo; walijaribu zoezi la kuwapatia hifadhi wakimbizi wa Kosovo katika nchi za Ujerumani, Uingereza na Marekani. Lakini hata hivyo jaribio hili liligonga mwamba. Cha msingi, NATO inaunga mkono kufukuzwa na kuuawa kwa Waislamu katika Kosovo. Mashambulizi yote hayo ya NATO dhidi ya Yugoslavia hayana uhusiano wowote na Waislamu wa Kosovo. Wakosovo wanatumika tu kama chambo cha kumpigia Milosovic.

Picha za kusikitisha za wakimbizi wa Kosovo waliokwama kwenye makambi ya wakimbizi zinaumiza sana. Watoto, wanawake, vikongwe, majeruhi. Huwezi kueleza bila ya kutokwa na machozi! NATO hawana huruma kabisa na viumbe hawa wa Mwenyezi Mungu. Wanachojali ni malengo yao tu. NATO na Milosovic wote ni wa kulaaniwa tu!

Marekani iliionya Urusi ilipoonyesha nia ya kuisaidia Yugoslavia. Urusi ilitaka kujiingiza katika mgogoro huu kwa sababu wanafahamu kitu gani NATO inatafuta Yugoslavia. Hata hivyo Urusi ilifyata baada ya mkwara wa Marekani kwa hofu ya kupoteza misaada ya kiuchumi na kuvuruga mahusiano yake na mataifa ya Magharibi. Isitoshe mgogoro wa Kosovo hauna manufaa makubwa kwa Urusi.

Mtu anaweza kujiuliza kwanini NATO na siyo UN katika mgogoro wa Kosovo? Sababu zinaweza kuwa nyingi lakini zilizo wazi kabisa ni kwamba wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuna wanaokubaliana na Yugoslavia kiitikadi. Kwa mfano China na Urusi zote zinafuata siasa za Kikomunisti. Wangetumia kura zao za 'veto' kupinga maazimio ya kuishambulia kijeshi Yugoslavia na lengo lisingetimia. Halafu tena, nia na madhumuni yaliyoundiwa NATO yalikuwa kupambana na nguvu za Wakomunisti. Kwa hiyo NATO ndiyo chombo muafaka cha kuishambulia Yugoslavia.

Watu wajue tu kwamba NATO haimpigi Milosovic kwa sababu ya kuwahami Waislamu wa Kosovo kama wanavyonadi. Hii siyo kazi ya NATO; na hawatafanya hivyo popote pale.

Waislamu wa ulimwengu mzima tujiulize, wenzetu wana NATO na UN za kuwalinda, sisi tuna nini? NATO haikusambaratika kama 'Warsaw pack' baada ya vita baridi. Na imetangaza kwamba: "Zimwi linalowatia hofu baada ya Ukomunisti ni Uislamu" Je, Waislamu tumechukua tahadhari gani?

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook