KUTOKA MAGAZETI YA ZAMANI
 
 
 
Sitanii nikisema Haikomisheni ife - Tumbo
 

Ngurumo, Jumanne Aprili 11, 1961

BWANA C. Kassanga Tumbo, Mwandishi Mkuu wa TRAU akiwa amerudi kutoka kwenye mkutano mkuu wa mwaka toka Dodoma, aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, "Labda wengine wanadhani natania, lakini nikisema hatuitaki Haikmisheni, maana yetu ni Haikomisheni ife kweli. Tena tutaendelea kuomba ife. Tumesema ife ife tu".

Akieleza yaliyozungumzwa kwenye mkutano mkuu huo alisema kulizungumzwa mengi lakini kulikuwa na mambo muhimu manne kuhusu Haikomisheni.

"Jambo muhimu ni kwamba mkutano umeamua kuwa chama kinasimama pale pale pa kugoma Haikomisheni isiendelee na isiwepo.

Kwa mambo yanayofanywa na Haikomisheni hata kwamba chama hakioni faida ya kuwapo hapa Tanganyika, Bw. Tumbo alisema kuwa tangu Haikomisheni ianze Waafrika wafanyakazi katika idara ya reli wako hali ile ile, wako nyuma kwenye vyeo na mishahara na wala hawapati mafunzo ya kuwawezesha wainuke.

Kama 1948

Bw. Tumbo alisisitiza kusema kwamba kama mpaka mwisho wa mwaka huu hakutakuwa na mafanikio yoyote kati ya madai ya chama kwa jumla, bila shaka kutakuwa na mgongano kati ya idara na wafanyakazi, tena safari hii itakuwa ni wafanyakazi wote si kama safari iliyopita.

"Tunataka Haikomisheni ife na badala yake ikiwezekana iwe kama ilivyokuwa mwaka 1948, yaani Tanganyika Railways & Harbours kabla ya hii Haikomisheni kuwapo.

Kwa ajili ya umoja na nchi nyingine kama vile Kenya na Uganda, Bw. Tumbo alisema unaweza kuwapo ushirikiano kabisa ikiwa upana wa reli hautabadilishwa. Yaani magari ya Tanganyika yaweze kufika huku na huko yafike huko. Hapa uwepo mkataba kamili wa kuaminisha.

Wakuu Waafrika

Akigusia Africanisation ndipo aliposema kuwa bila kuchelewa Waafrika wapewe vyeo katika idara. Ikawa Waafrika watakuwa wakuu wa idara basi hapo Africanisation ndipo itafanyika haraka. Wale wageni, ikiwa mtu ni makenika basi asishughulike na kuandika vyuma kweli. Akiajiriwa mgeni katika kazi za kuendesha idara awe mshauri tu na si mkuu.

"Hatutaki wageni wawe wakuu, na hatujali serikali au ni chama gani kitakachokuwa kinatawala idara ya reli, ilimradi isiwe Haikomisheni". Alipogusia taarifa ya Flemming alisema taarifa hiyo haina demokrasia wala siyo sosholist na chama mpaka sasa hakiitambui. Flemming haitambui kuwa mfanyakazi ni mfanyakazi na awe mweupe au mweusi. TRAU tuko tayari kuchukua hatua hivi karibuni ikiwa hakuna mabadiliko", alisema.

Walakini

Alipoulizwa kwamba T.F.L ina mawazo gani juu ya Flemming na kufa kwa Haikomisheni, Bw. Tumbo alisema T.F.L inazo walakini tano ambazo bila shaka mpaka sasa zingalipo. Akasema kuwa kuna vikaratasi vilivyotolewa na idara ya reli kwa wafanyakazi watie sahihi kwamba wao wanaikubali taarifa ya Flemming. "Huku ni kututisha bure, hata wafanye nini hatutishiki na sidhani kwamba watafanikiwa", aliongeza.

President Bw. Andrew Hussein alisema kuwa amepata habari kuwa wafanya kazi wameambiwa na idara kuwa wakiwa hawakutia saini vikaratasi hivyo mwisho tarehe 15 Aprili, au ikiwa hawakuvirudisha kabisa, idara itahesabu wamekubaliana na idara. Bwana Tumbo akasema hata wote watie saini au wasitie ikiwa yeye hakutia saini saini haisaidii kitu. "Mkataba bila chama kukubali si mkataba wala hautakuwa mkataba", aliongeza.

Mgogoro

Mwisho akasema hapo jana kampelekea Labour Commissioner barua kwamba wafanye maafikiano upesi na chama au laa kutakuwa na mgogoro kati ya wazima moto, watu wa afya na wengineo.


Barabara za Dar zang'aa kwa mapambo:
Mgeni wa heshima awasili leo
 

Uhuru, Alhamisi Novemba 10, 1966

MGENI wa heshima wa Taifa letu, Rais Modibo Keita wa Jamhuri ya Mali, anawasili leo mjini Dar es Salaam mnamo saa saba za mchana akiwa amefuatana na mkewe pamoja na wajumbe wengine. Atawasili muda mchache tu baada ya kuwasili Rais Mwalimu Nyerere kutoka Addis Ababa ambako wote wamekuwa wakihudhuria mkutano wa viongozi wa nchi huru za Kiafrika. Mwalimu atawasili mnamo saa sita na nusu za mchana.

Miongoni mwa maelfu ya wananchi watakaowalaki viongozi hawa wawili ni pamoja na Makamu wawili wa Rais wa Tanzania, Sheikh A.A. Karume na Bwana Rashid Kawawa. Sheikh Karume atawasili dakika chache tu kabla ya Mwalimu kuwasili kutoka Addis Ababa.

Baada ya kutua tu katika uwanja wa ndege wa Dar es Saaam, Rais Keita atalakiwa na Mwalimu pamoja na Makamu wake wote wawili baadaye atasimama kwenye jukwaa maalum na nyimbo za mataifa yote mawili, kwanza wa Mali na baadaye wa Tanzania zitapigwa.

Baadaye atakagua gwaride rasmi la heshima litakalofanywa na kikosi cha jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania na kurejea tena jukwaani ambapo nyimbo za mataifa yote mawili, kwanza wa Tanzania na baadaye wa Mali, zitapigwa. Mgeni wetu kisha atatambulishwa kwa viongozi mbalimbali wa TANU na serikali, mabalozi na watu wengine mashuhuri.

MAANDAMANO

Baada ya kumalizika shughuli za hapo kiwanjani, mgeni wetu akikutana na Mwalimu, wataondoka kwa motokaa ya serikali na kuongoza maandamano ya magari mpaka Ikulu kupitia mitaa ya Pugu, Buguruni, Uhuru, Railways, Azania, City Drive, Magogoni na kuingia Ikulu.

Mkuu wa wilaya ya Dar es Salaam, Bwana Mustapha Songambele amewaomba wananchi wa Dar es Salaam wajipange kwa wingi sana mabarabarani wakichanganyika na watoto wa shule kumshangilia mgeni wetu. Kadhalika kutakuwa na ngoma katika sehemu mbalimbali za njia hizo zote atakazopitia mgeni wetu.

Baada ya kuwasili Ikulu, mgeni wetu pamoja na Mwalimu watajipumzisha kwa muda mpaka hapo saa kumi na moja ambapo Rais Keita atatembelea ofisi ya Ubalozi wa Mali uliopo mjini Dar es Salaam. Saa tatu usiku kutakuwa na karamu rasmi ya kiserikali itakayoandaliwa na Mwalimu Nyerere kwa heshima ya mgeni wetu huko Diamond Jubilee.

Kesho 11/11/66 saa tatu asubuhi Marais wote wawili watakuwa na mazungumzo ya kiserikali. Saa saba mchana watakula chakula cha mchana. Mkewe nae wakati wa saa tatu za asubuhi atatembelea na kukagua kazi za mikono za kina mama, baadaye atatembelea hosteli ya U.W.T. Mnamo saa nne atatembelea shule ya vidudu ya Magomeni na baadaye atakwenda kutembelea Chuo Kikuu na Colito Barracks. Atarejea Ikulu saa sita mchana.

Mnamo saa tisa alasiri Rais Keita na ujumbe anaongozana nao atakwenda Zanzibar ambako amepangiwa kuhutubia mkutano wa hadhara.

Katika kiwanja cha ndege Rais Keita atapokelewa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Sheikh Abeid Amani Karume. Atakagua gwaride la heshima litakalofanywa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Zanzibar na Young Pioneers. Mawaziri wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Mapinduzi, Wakuu wa chama cha Afro-Shirazi na Watumishi wa Serikali watatambulishwa kwa mgeni huyu.


'TANU inajenga wengine wanabomoa'
 
 

Mwafrika, Jumatatu Oktoba 22, 1962
 

WAKATI wananchi wanashughulika na kazi za kujenga nchi na taifa, kuna baadhi ya viongozi wa vikundi va siasa (political factions) wanaojitahidi sana kubomoa na kuwashawishi wananchi warudi nyuma.

Habari hizi zimeelezwa na Katibu Mtoa Habari wa TANU, Dr. Willbert Kleruu.

Dr. Kleruu anasema, "Hakika Bwana Makaidi amewatobolea wananchi kwamba siasa yake na ya Kigrupu chake ni siasa ya kutunga maneno yasiyo kweli ili kuwapuuza wananchi.

"Mathalan, mpaka hivi leo Bwana Tumbo aliye mkubwa wa kigrupu cha P.D.P hajathubutu kuwatobolea wananchi sababu za kujiuzulu Ubalozi, mahali alipopata mapesa kemukemu na kusema mawaziri wetu wasilindwe.

"Hii ni kweli tupu, maana shughuli kubwa ya P.D.P imekuwa ni kutoa orodha ya vinung'uniko na vinung'uniko visivyo na msingi, juu ya mwenendo wa serikali yetu. Wakati umewadia kwa Bwana Makaidi na P.D.P yake kufahamu waziwazi kwamba kikundi cha siasa kinachotegemea vinung'uniko vitupu visivyo na ukweli ni kama kijumba kilichojengwa juu ya ardhi ya mchanga na wakati upepo uvumapo kijumba hicho huanguka chini.

Kujenga Taifa

"Isitoshe, Makaidi wa P.D.P badala ya kufanya kazi ya kujenga nchi na Taifa, anazidi kujibidisha na kutungatunga uongo na kukashifu watumishi wa TANU na hasa Dr. Kleruu.

"TANU inajenga nchi, haina nafasi ya kutukanana na kikundi chochote. Hivyo basi, Bwana Makaidi na kigrupu chake ni sharti waelewe barabara kwamba hata akiandika gazeti zima kumtukana, kumkashifu na kumharibia jina Dr. Klerruu hayo yote ni kama anajisumbua maana huyo Dakta hatikisiki wala hatageuza imani yake na TANU na juhudi za kujenga nchi na Taifa letu.

"Bwana Makaidi ingawa umeweza kuwanasa akina Masanja na Kidaha haiwezekani kamwe kumnasa Dr. Klerruu. Kwa vyovyote ni vigumu kwa Makaidi kumnasa Dr. Klerruu kuliko ngamia kuingia katika tundu la sindano.

Wameng'amua

"Kwa kifupi, wananchi wamekwisha ng'amua siasa ya Makaidi na P.D.P yake. Bila shaka hiyo siasa ya Makaidi inanuka ukoloni fuu!

Sisi wana TANU tunatimiza wajibu wetu wa kujenga nchi hii upesi iwezekanavyo, wale wanaobomoa na kupita mvunguni wanajisumbua tu. Mara nyingine tena tunamhakikishia Makaidi na P.D.P. yake kuwa hii si nchi ya waenda wazimu.


Blanketi na sinema bei iko juu
Bali kodi haibadiliki
 

Mwafrika, Jumatano Juni 12, 1963

UKIONDOA vitu kama blanketi, dongo Ulaya na vingine hakukuwa na nyongeza kubwa ya ushuru katika hotuba ya Waziri wa Fedha Bw. Bomani, jana usiku alipokuwa anaeleza makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za serikali kwa mwaka ujao.

Mambo makubwa yaliyokuwa yanawatisha watu kuwa huenda yakaongezwa yahakuwepo. Hivyo hakuna nyongeza ya sigara, sukari, vibiriti, pombe za kizungu au kodi.

Katika hotuba hiyo Bw. Bomani alitangaza kuongezeka kwa ushuru wa baadhi ya vitu vifuatavyo:

Blanketi kwa senti 5 kila yadi, mashati, singleti na nguo nyingine senti 15.

Motokaa kutoka pasenti 15 mpaka pasenti 25 au 30 ikitegemea aina ya motokaa hiyo; na pia spea pati zake.

Vyombo vingi vya ujenzi vitaongezeka ushuru kutoka pasenti.

Dongo Ulaya na michezo ya watoto kumi na mbili na nusu mpaka ishirini na tano.

Bwana Bomani alisema kwamba hanuii kuongeza kodi ya kichwa au ya mapato.

Kati ya kodi ambazo amezitaja ili kuleta fedha ya maendeleo ni kodi ya starehe nayo itakuwa shilingi moja kwa kila mtu anayeingia sinema au sehemu kama hizo isipokuwa kama ni michezo ya elimu.

Katika hotuba yake Bw. Bomani alisema kuwa mwaka huu umekuwa mzuri katika uchumi ukilinganishwa na miaka ya nyuma. "Mbele yetu", alisema, "kuna matumaini mema ya uchumi".

Hata hivyo, alidokeza "sipendi kuonyesha kuwa upo wakati na nafasi ya kutosheka na kupumzika, maadui zetu ujinga, umaskini na magonjwa bado tunavyo, na umoja na bidii vinatakiwa zaidi ili kuwaondoa".

Akimalizia hotuba yake Bw. Bomani alisema kuwa makadirio na mapato aliyoeleza yametengenezwa ili kupambana na vipingamizi vyote vilivyoko mbele. "Serikali inaweza kutengeneza mipango, lakini mwisho wake ni bidii ya watu wote watakaoleta mafanikio ya mipango hiyo", alisema.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook