CHAKULA NA LISHE
 
 
Maelezo ya TBS kwa Zanzibar si ya kisayansi
 

Na Mujahid Mwinyimvua
 

SHIRIKA la Viwango Tanzania kwa kifupi T.B.S limetoa maelezo kufuatia kauli ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyowataka wananchi wake wajihadhari na maji ya chupa aina ya "MASAFI".

Maelezo hayo ya TBS kama yalivyoripotiwa na gazeti la Kiingereza la "The African' la Mei 27, mwaka huu yametolewa na Mkurugenzi wa Shirika hilo la Umma, Daimon Mwakyembe.

Kwa kifupi TBS imesema kuwa imethibitisha (approved) maji ya chupa aina ya MASAFI na kwamba madai ya serikali ya Zanzibar kuwa maji hayo hayafai kwa matumizi ya binadamu hayana ushahidi wa kisayansi.

Zaidi ya hayo, shirika hilo la viwango nchini limesema kuwa kauli ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa maji ya "MASAFI" si safi kwa matumizi ya binadamu ni ya kisiasa. TBS imeyathibitisha (approved) maji hayo mwishoni mwa mwaka jana.

Mkurugenzi wa TBS aliendelea kusema kuwa anajua kinachoendelea Zanzibar kuwa kuna vita ya maji (Water war) baina ya maji ya chupa yanayotengenezwa visiwani humo na yale yanayotoka Bara.

Bwana Mwakyembe pia ameshangaa serikali ya Zanzibar kwa kusema kuwa, kama serikali hiyo ilikuwa na wasiwasi na viwango vya maji hayo, ingelisema jambo hilo tangu mwaka jana wakati visiwa hivyo hakikuwa na kiwanda cha kutengeneza maji.

Moja ya kazi ya chombo cha habari ni kuelimisha jamii. Wiki iliyopita nikiwa kama mtaalamu wa chakula na lishe, nilitumia gazeti hili kufikia azma hiyo.

Katika toleo hilo, nilijadili kadhia ya maji ya maji ya chupa (bottled water) aina ya "MASAFI" kwa hoja kuwa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeteleza katiak kuliendea jambo hilo.

Shirika la viwango Tanzania (Tanzania Bureau of Standards) limetoa kauli yake kuhusu kadhia hiyo ya maji ya "MASAFI" ili kuweka mambo sawa.

Hata hivyo, chombo hicho ambacho ni cha kitaalamu nacho 'kimeboronga' katika maelezo yake juu ya maji ya chupa aina ya "MASAFI" na kuiacha jamii ikijiuliza: Nani zaidi kati ya TBS na maabara ya mkemia mkuu wa serikali ya Zanzibar.

Kwa kuzingatia ukubwa wa msiba huo na athari yake kisiasa, kiuchumi na kijamii, nimeona nina wajibu tena kuwaelimisha 'wanaogombana', na wananchi kwa ujumla.

Ukiyasoma kwa makini maelezo ya TBS kwenye gazeti nililolinukuu hapo awali au ukiisoma tafasiri niliyoiandika hapo juu utaona wazi kuwa shirika letu la umma (TBS) nalo limetoa maelezo ambayo siyo tu si ya kisayansi bali pia ya majigambo (kibri). Kuna maeneo kadhaa yanayothibitisha hoja yangu.

Kwanza, TBS imesema kuwa madai ya serikali ya Zanzibar hayana ushahidi wa kisayansi. TBS ikiambiwa ithibitishe yake sidhani kama itakuwa rahisi kwake.

Hii ni kwa sababu, vyombo vya habari viliripoti kuwa kauli ya serikali ya Zanzibar imeegemea kwenye uchunguzi uliofanywa na ofisi ya mkemia mkuu wa serikali hiyo. Na wala haikuwa kauli tupu ya mtu wa serikali kutolewa kwenye vyombo vya habari.

Kwa maneno mengine inachosema TBS ni kuwa haikubaliani na uchunguzi uliofanywa na mkemia mkuu wa Zanzibar.

Kanuni ya sayansi inasema kuwa huwezi kukataa uchunguzi alioufanya mwenzio bila ya wewe nawe kufanya kwa njia zile zile alizozitumia mwenzako.

Kitendo cha TBS kutoa kauli ya kupinga uchunguzi wa mkemia mkuu bila ya kufanya uchunguzi nacho si cha kisayansi na maelezo yake yamejengwa katika misingi ya majigambo badala ya ushahidi wa kisayansi (Scientific facts).

Jambo lililotarajiwa kutoka TBS, ambalo ni la kisayansi ni kusema kuwa: Tumepokea kauli ya serikali ya Zanzibar kuhusu maji ya chupa aina ya "MASAFI" kwa mujibu wa vipimo vyetu vya mwishoni mwa mwaka jana, maji hayo ni safi kwa matumizi ya binadamu. Hata hivyo tutatuma timu yetu ya wataalamu kwenda Zanzibar kuchukua sampo (maji) ili tuchunguze na tuone hali ikoje kwa sasa, hasa kwa maji yale yaliyopelekwa huko Zanzibar.

Kabla ya kuendelea zaidi ni vyema tutazame swali moja ambalo huenda wasomaji wangu wameshajiuliza.

Swali hilo ni: Kwanini makala iliyopita ilikosoa serikali ya Zanzibar na makala hii inaonekana kuitetea?

Katika makala ya wiki iliyopita sikupinga uchunguzi wa mkemia mkuu. Nilichokosoa ni ule uamuzi wa serikali (afisa wa afya) kuacha kutoa maelezo ya kina kuhusu ripoti hiyo ya mkemia mkuu.

Nadhani tunajua kuwa kazi ya mkemia mkuu ni kufanya uchunguzi, lakini msemaji ni Wizara ya Afya (Serikali).

Leo tunachokitazama hapa ni kitendo cha TBS kukataa uchunguzi wa mkemia bila yenyewe kufanya uchunguzi wa hivi karibuni.

Pili, TBS imesema kuwa imeyathibitisha maji ya "MASAFI" kuwa ni masafi kwa matumizi ya binadamu mwishoni mwa mwaka jana (TBS approved of the water at the end of last year).

Hoja hii siyo tu si ya kisayansi bali pia inatia aibu kusemwa na afisa wa cheo cha juu wa shirika la umma.

Hii ni kwa sababu, tangu uchunguzi wa TBS mpaka tukio hili llilipotokea kwa uchache tunaweza kusema imepita miezi mitano. Katika kipindi hicho 'batch' ngapi za maji zimetengenezwa? Zote hizo ni safi?

Pia inafahamika kuwa inawezekana kabisa katika uzalishaji, maji yakawa safi, lakini mazingira ya usambazaji na kuyahifadhi (storage) yanaweza kuwa sababu ya kuharibika ubora wa maji hayo. TBS inalijua hili, kwa sababu wanautaratibu wa kupita madukani (na kwingineko kunakouzwa maji) ili kuchukua sampo (maji) na kwenda kuzipima. Lengo waone kama wananchi wanapata bidhaa bora kama vile zilivyotengenezwa viwandani.

Zaidi ya hayo, kampuni inayotengeneza maji ya "MASAFI" imewahi kuwatangazia wananchi kuwa kuna watu wanatumia chupa zake na kuweka maji ambayo siyo safi ya kwao. Kwa hiyo, wakawaomba wananchi wazipasue chupa baada ya kutumia maji yao.

Swali, TBS inaushahidi gani wa kisayansi kuwa Zanzibar hakuna maji yaliyotiwa kwenye chupa za maji aina ya "MASAFI" na watu wasiokuwa waaminifu?

Tukumbuke kuwa, maji hayo ya bandia si rahisi kuyagundua kwa mnywaji kwa sababu yana lebo na pia mifuniko yake ina 'seal' (imefungwa vizuri).

Tatu, TBS inahoji kwanini serikali ya Zanzibar haikuonyesha wasiwasi wake mwaka jana wakati haikuwa na kiwanda chake cha kutengeneza maji? Hoja hii nayo si ya kisayansi. Kwanini iwe na wasiwasi wakati uchunguzi wa mkemia mkuu (mwaka jana) ulisema kuwa maji hayo ni safi kwa matumizi ya binadamu?

Napenda kumalizia makala hii kwa maelezo yafuatayo: Kadhia hii ya "MASAFI" imeleta picha mbaya ndani na nje ya nchi. Vyombo viwili vya kitaalamu vinapolumbana kwenye vyombo vya habari, mwananchi wa kawaida atashika la nani?

Kwanini malumbano haya kama hayana budi kuwepo yasifanyike kwenye maabara ili wataalamu wenye ujuzi mdogo wajifunze kutoka kwa wenziwao? Kwanini hatupendani wakati nchi ni moja?

Baya zaidi, tayari baadhi ya wananchi wana dhana mbaya kuwa rushwa huenda imetembea ili kulinda biashara za watu.

Tunaomba, kama juhudi hazijafanywa, serikali ya Jamhuri na ile ya Zanzibar wawekeni chini TBS na ofisi ya mkemia mkuu wa serikali ya Zanzibar ili waondoe hitilafu zao na uchunguzi ufanywe tena, hata kwa kushirikisha ofisi ya mkemia mkuu wa serikali ya Jamhuri ili wananchi wajulishwe ukweli wa mambo.

Bado tunaimani kuwa, dhana ya ukweli na uwazi siyo ya Mheshimiwa Rais Benjamin Mkapa peke yake bali ni ya watendaji wote wa vyombo vya serikali na umma na wananchi kwa ujumla.

--

Juu RUDI


Bonyeza hapa
kushriki mjadala au kutoa maoni juu ya habari hizi na masuala mengineyo ya Kiislamu kwenye Baraza ya Wasomaji

   Kutoa maoni yako kuhusu ukarasa huu: Bonyeza hapa
Au
Andika barua  kwa: webmaster@islamtz.org
 
An-nuur Home | Ukurasa wa Mwanzo | Islam Tanzania 
Links | Matoleo Yaliyopita | Sign our Guestbook