Cheka na langu shairi
Cheka na langu shairi, siasa
zitafakari,
Uzichunguze habari, sera
nyingi ni za shari,
Ubabe uko dhahiri, hadharani
si kwa siri,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Cheka na langu shairi, tulia
utafakari,
Dhulma imekithiri, si wakati
wa zumari,
Acha karata, golori, bao
lifunge kufuri,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Cheka na langu shairi, akilini
ufikiri,
Vipi haki isafiri, wakati
huna habari,
Wewe kweli ni mahiri, wa
kujipa uhodari,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Cheka na langu shairi, nyimbo
miziki ghururi,
Utaleweshwa chakari, ushindwe
kutafakari,
Hutoweza kufikiri, kuzipembua
habari,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Cheka langu shairi, pande
tupige viburi,
Tuchukue tahadhari, tuchore
na mstari,
Watambue si vizuri, ubabe
na ukahari,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Cheka na langu shairi, unafiki
si mzuri,
Ukatumiwa kwa siri, kuchota
zetu habari,
Ufanyayo ya hatari, kutumikia
kafiri,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Cheka na langu shairi, yangu
maneno sukari,
Usifanye uhodari, kusema
kila habari,
Zingine ufanye siri, ziweke
uzisitiri,
Cheka na langu shairi, tumo
katika hatari.
Idd Kikong’ona,
Morogoro.
Haki
Sineni nao wazee, namba vijana
mliko,
Leyo niwadokezee, akili
zifanye shiko,
Kila siku mutetee, vyenu
visende kusiko,
Uwatapo haki yako, nani
akuokotee?
Akuokotee nani, uwatapo haki
yako,
Kutwa wajifanza duni, hewala
tamko lako,
Huwo ni uhayawani, chunga
sana bongo lako,
Uwatapo haki yako, nani
akuokotee?
Huwa haiombwi haki, leyo
mufanye zinduka,
Hutwaliwa kwa mikiki, ya
juu hwendewa huko,
Bora wambwe balamaki, kuata
ni dhara kwako,
Uwatapo haki yako, nani
akuokotee?
Tetea kwa kulla hali, sihofu
misukosuko,
Namba kwa mwene akili, aso
na mawazo koko,
Kuporwa usikubali, kubali
ufe kwa chako,
Uwatapo haki yako, nani
akuokotee?
Mtu hakiyo afite, afite kwene
mfuko,
Asiitike umwite, aondoke
kwa katiko,
Bora teke mkung’ute, ende
kefu aendapo,
Uwatapo haki yako, nani
akuokotee?
Ni amri ya Sattari, M’mi
si langu tamko,
Kutwaa siyo dosari, haki
kwa huku twendako,
Kaditamati shairi, nakoma
hili andiko,
Uwatapo haki yako, nani
akuokotee?
“Kuhani Mkuu”,
Iddi M. Mwassa (Pilato),
S.L.B. 15789,
Dar es Salaam.
Bismillahi baswiyru, mbora
wa walimwengu,
Vibaya kumkufuru, Muumba
wa saba mbingu,
Nyingine sifa bashiru, si
mwingine bali Mungu,
Acheni kujichubua, tamaduni
yapotea.
Tamaduni yapotea, acheni
kujichubua,
Ngozi zenu mwasumbua, kwa
yenu hiyo tabia,
Weupe jitafutia, mudhaniwe
Waasia,
Acheni kujichubua, tamaduni
yapotea.
Shindanoni Namibia, nani
asoshuhudia?
Ushindi jitafutia, wengi
walijichubua,
Mweusi alichukua, mkorogo
walilia,
Acheni kujichubua, tamaduni
yapotea.
Rangi nyeusi ni yetu, Mola
katujaalia,
Yeye kapendeza kwetu,
asili tambulisha,
Tunaupoteza utu, tusipojivunia,
Acheni kujichubua, tamaduni
yapotea.
Weupe mukishapata, madharae
mwayaona,
Ajali ikiwakuta, ni vigumu
kuwashona,
Tena zaidi matata, nyuzi
ngozi inachana,
Acheni kujichubua, tamaduni
yapotea.
Ndugu zangu kwaherini, kalamu
naweka chini,
Shairi mulishikeni, tena
lizingatieni,
Yalosemwa ni yakini, amini
usiamini,
Acheni kujichubua, tamaduni
yapotea.
Said Mkama,
Box 65,
Mtwara.
Kufunga swala shingoni
(jibu)
Assalaamu alaykum, ewe ndugu
Isilamu,
Leo nina kubwa hamu, kukupa
jibu adhimu,
Kwa kauli ya karimu, Mola
wa yote kaumu,
Kufunga swala si nguzo,
ni Sunna twatekeleza.
Kufunga swala shingoni, au
mikono achia,
Au kufunga tumboni, kifua
hujakosea,
Jiondoe mashakani, fanya
ulilozowea,
Kufunga swala si nguzo,
ni Sunna twatekeleza.
Usemapo neno swala, yapo
yake ya lazimu,
Kwanza iwe na twahara, na
wakati ufahamu,
Jambo jingine sitara, na
Qibla ukufahamu,
Kufunga swala si nguzo,
ni Sunna twatekeleza.
Swala ina zake nguzo, kumi
na saba bayana,
Kati ya zote hizo, kufunga
swala hamna,
Usijezuka mzozo, na watu
kufarakana,
Kufunga swala si nguzo,
ni Sunna twatekeleza.
Mtume mfano mwema, kiigizo
cha dunia,
Mikono hakuachama, kifuani
kashikia,
Ndugu yangu muadhama, Mtume
fuatilia,
Kufunga swala si nguzo,
ni Sunna twatekeleza.
Kuna mengi malumbano, mijini
na vijijini,
Wengine waseme tumbo, na
wengine kifuani,
Iondoke minong’ono, sira
irejeeni,
Kufunga swala si nguzo,
ni Sunna twatekeleza.
Tamati nimefikia, naweka
yangu kalamu,
Jambo hili zingatia, ndugu
yangu Isilamu,
Kufunga swala sikia, ni
jambo lisolazimu,
Ni Sunna ya
Muhammadia, si ya Shekhe wala Imamu.
Zuhura Uwesu Mashaka,
P.O. Box 55105,
Dar es Saalam.
Yafaa? Na. 1
Enyi wajuzi wa mambo, werevu
ulowajaa,
Watofautisha shombo, la
samaki na dagaa,
Ninawauliza jambo, munambe
kama yafaa,
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
Watongozi tongoweni, tujuwe
dowa na waa,
Kwa mja muasi dini, kusali
alokataa,
Haya nambeni yakini, kumuombeya
duwaa,
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
Sikuwaumba majini, na binadamu
lwaa,
Kasema niabuduni, mnena
haya Shufaa,
Mja anapo jihini, kusali
aseme kaa,
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
Kaishi kwenye duniya, toka
kuzaliwa ng’aa,
Kala na kujilaliya, waa
kaona bidaa,
Yaswih akijifiya, kumsaliya
jamaa?
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
N’jibuni “shaziliya”, msipoteze
wasaa,
Nawadhehebu la “Shiya”,
ka’tu msije bung’aa,
Nambeni “Ahamadiya”, mfaa
huyu si kinyaa!
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
Wa Kadiriya dhehebu, nyuma
msije zubaa,
Mtu mchapa sharabu, kunwa
bia na chang’aa,
Afapo naye wajibu, kumsaliya
jamaa?
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
Kalamu haiandiki, naibwaga
tini pwaa,
Waja mlosoma fiq, hususan
Ulamaa,
Haya kamateni biki, munipe
hii fatwaa,
Kumsaliya yafaa, mja mfu
asosali?
“Kuhani Mkuu”,
Iddi M. Mwassa (Pilato),
P.O. Box 15789,
Dar es Salaam.
--
|
|